RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein amemtumia salamu za
pongezi Rais wa Djibout, Ismail Omar Guelleh kwa kutimiza miaka 42 tokea Taifa
hilo kupata uhuru wake.
Salamu hizo zilieleza kuwa wananchi wa Zanzibar
wanaungana na ndugu zao wa Djibout katika kusherehekea siku hii adhimu kwa Taifa hilo.
“Kwa niaba yangu binafsi, watu wa Zanzibar na Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar natumia fursa hii kukupongeza wewe pamoja na wananchi wote
wa Djibouti kwa kutimiza miaka 42 ya uhuru”, ilieleza sehemu ya salamu hizo
alizotuma Dk. Shein.
Aidha, katika salamu hizo, Dk. Shein alimuhakikishia
Rais Guelleh kuwa Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano mkubwa uliopo
kati yake na Djibout sambamba na kuimarisha maeneo mapya ya mashirikiano kama
walivyokubaliana na Rais huyo wa Djibout wakati wa ziara yake aliyoifanya mnamo
mwaka 2017.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein katika salamu
hizo alieleza kuwa miaka 42 ya uhuru wa Taifa hilo inaimarisha zaidi
mashirikiano kati ya nchi mbili hizo pamoja na watu wake.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alitumia nafasi hiyo
kumtakia uongozi mwema Rais Ismail Omar Guelleh pamoja na kusherehekea vyema
siku hii adhimu kwa Taifa hilo sambamba na kuendelea kuliongoza kwa amani na
utulivu mkubwa kwa maendeleo endelevu ya wananchi wa Djibout.
Djibout ilipata uhuru wake mnamo tarehe 27 Juni
mwaka 1977 kutoka koloni la Ufaransa chini ya Jemedari wake Hassan Gouled Aptidon
ambaye alikuwa Rais wa kwanza wa Djibout.
Wakati huo
huo, Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein amemtumia
salamu za pongezi Rais wa Msumbuji, Felipe Nyusi kwa kutimiza miaka 44 tokea
kupata Uhuru kwa Taifa hilo.
Salamu hizo zilieleza kuwa kwa niaba yake Dk.
Shein, wananchi pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wanaungana pamoja
na ndugu zao wa Msumbuji katika kusherehekea siku hiyo adhimu ya uhuru wa Taifa
hilo.
Aidha, katika salamu hizo, Dk. Shein
alimuhakikishia Rais Nyusi kuwa Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano
mkubwa uliopo kati yake na nchi hiyo sambamba na kuimarisha udugu uliopo kati
ya wananchi wa pande mbili hizo.
Pia, salamu hizo zilieleza namna ya Zanzibar
itakavyoimarisha ushirikiano uliopo kati yake na Msumbuji kwa kukuza uhusiano
mwema wa kikanda na kimataifa.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alitumia fursa hiyo
kumtakia Rais Nyusi afya njema yeye na familia yake na kumtakia maisha marefu
yenye furaha pamoja na sherehe njema ya siku hiyo adhimu ya uhuru wa Taifa hilo
kwa amani, utulivu na upendo kwa maendeleo endelevu ya wananchi wa Msumbiji.
Msumbiji ilipata uhuru wake Juni 25 mwaka 1975
kutoka kwa koloni la Ureno chini ya Jemedari wake Samora Machel.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address:
2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment