Habari za Punde

Balozi Seif aendelea na ziara kisiwani Pemba

 Moja kati ya Mabwawa 12 ya kufugia samaki na Kaa ya  Wanaushirika wa  Siri Farm and Fish Kijiji cha Pujini ambayo yanakabiliwa na ukosefu wa Vifaranga vya Samaki
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiutembelea Ushirika wa Ufugaji Samaki na Kaa wa Kijiji cha Pujini ndani ya Wilaya ya Mkoani Kisiwani Pemba.
 Mkuu wa Miradi wa Kikundi cha Ufugaji wa Samaki na Kaa cha Pujini Bwana Nassor Rashid Kombo akimpatia maelezo Balozi Seif aliyefika kuutembelea Mradi wao
 Muonekano wa Bara bara Mpya ya Ole hadi Kengeja yenye urefu wa Kilomita 35 inayojengwa katika kiwango cha lami ambayo tayari imeshafikia Kilomita  17 na kubakisha Kilomita 18
  Balozi Seif akiusisitiza Uongozi wa Wizara ya Ujenzi, mawasiliano na Usafirishaji kufanya jitihada za ziada kuikamilisha bara bara ya ole – Kengeja katikia kipindi kisichopindukia mwezi Januari Mwakani ujao wa 2020.
 Wanafunzi wa Skuli ya Sekondari ya Mtambile wakimlaki Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliyefika kukagua ujenzi wa Jengo la Ghrofa kwenye Skuli hiyo linalojengwa kwa nguvu za Wananchi wenyewe.
 Mhandisi wa Ujenzi wa Skuli ya Sekondari ya Mtambile Bwana Hussein Maulid Hamad akimpatia maeleo Balozi Seif jinsi ya ujenzi wa Jengo hilo la Ghorofa Mbili.

Muonekano wa Jengo la Ghorofa la Skuli ya Sekondari ya Mtambile likiwa katika hatua ya msingi, litakapokamilika litakuwa na ghorofa Mbili.
  Balozi Seif na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Riziki Pembe Juma wakipata maelezo kutoka kwa Mjenzi wa Jengo la Dakhalia ya Skuli ya Sekondari ya Mohamed  Juma Pindua liliopo Wilaya ya Mkoani Pemba.
 Balozi Seif akielezea faraja yake kutokana na umakini wa ujenzi wa Dakhalia hiyo ambao unaonekana kukidhi vigevyo stahiki vya Majengo ya Taasisi za Umma.

Muonekano wa ndani wa Jengo la Dakhalia ya Wanaume katika Skulki ya Sekondari ya Mohamed Juma Pindua Mkoani Kisiwani Pemba.
Picha na –OMPR – ZNZ

Na Othman Khamis, OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Serikali itachukuwa hatua na kufanya juhudi katika  kuunga mkono Miradi mikubwa iliyoanzishwa na Wananchi ambayo imetoa ajira  ili kuondoa au kupunguza changamoto inayoikabili Miradi hiyo katika uendeshaji wake.
Alisema Ilani ya Chama cha Mapinduzi  imeweka wazi namna ya kuunga mkono Miradi ya kujetegemea muongozo ambayo Serikali ina kila sababu ya kuisimamia katika utekelezaji wake.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Baridi Shehia ya Dodo  huko Pujini mara baada ya kukagua Shamba la Ufugaji wa samaki na Kaa la Kikundi cha Ushirika cha  Siri Farm and Sailt kilichoanzishwa mnamo Mwaka 2,000 kikiwa na Wanachama 11.
Alisema juhudi za Wananchi zinazochukuwa gharama kubwa katika uendeshaji wa Miradi yao ya kiuchumi lazima iungwe mkono ili kuwapa matumaini ya kuiendeleza Miradi yao iweze kudumu katika kipindi kirefu  kustawisha maisha yao.
Balozi Seif aliwapongeza Wananchi hao wa Kijiji cha Baridi, Dodo Pujini kwa uwamuzi wao wa kujiletea maendeleo katika mpango wa kuanzisha Miradi ya Kiuchumi.
Aliwahakikishia Wananchi hao kwamba Serikali imelipokea ombi lao la kusaidia Miundombinu ya Ujenzi wa Ukuta wa Kuzuia nguvu ya Maji ya Bahari yanayokuwa na nguvu baadhi ya wakati  na kuharibu Mbwaya yao ambao unahitaji gharama kubwa.
Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwatahadharisha Wanaushirika hao kuwa makini na muenendo wa Uendeshaji wa Ushirika wao kwa vile baadhi ya Watu ndani ya Ushirika wanakuwa na maamuzi binafsi yanayopelekea kwenda kinyume na matumizi ya Fedha.
Mapema akitoa maelezo ya Mradi huo wa Ufugaji wa Samaki na Kaa wa Ushirika wa Siri Farm and Salt Mkuu wa Miradi Bwana Nassor Rashid Kombo alisema Mabwawa hayo zamani yalikuwa yakizalisha Chumvi lakini kutokana na athari za kimazingira wakaamua kubadilisha mradi mwengine.
Alisema Mradi wa ufugaji wa samaki ulianza Mnamo Mwaka 2,000 ukiwa na Mabwawa 12 chini ya ushauri na utaalamu kutoka Idara ya Uvuvi na mazao ya Baharini.
Bwana Nassor Rashid Kombo alimueleza Balozi Seif  kwamba mradi huo hivi sasa unakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa Vifaranga pamoja na kasi ya maji ya bahari yanayovuka kwenye Tuta maalum ambalo haliwezi kudhibiti maji hayo.
Alisema endapo Mabwawa yao yangepata vifaranga vya Samaki yana uwezo wa kufuga samaki wanaokadiriwa kufikia Tani Mia Moja na Hamsini za Samaki kwa Mwaka ambapo samaki mmoja hufikia uzito wa wastan wa Kilo Tatu akiwa tayari ameshafikia kiwango cha kuvuliwa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliendelea na ziara yake kwa kukagua maendeleo ya ujenzi wa Jengo Jipya la Skuli ya Sekondari ya Mtambile lililobuniwa na Wananchi wenyewe pamoja na Jengo la Dakhalia la Skuli ya Sekondari ya Mohamed Juma Pindua ndani ya Mkoa wa Kusini Pemba.
Majengo yote mawili yamebuniwa kwa mawazo ya Viongozi, Wazazi na kungwa mkono ya Washirika wa Sekta ya Elimu ili kuondosha changamoto za ufinyu wa Madarasa na Dakhalia zilizokuwa zikiwakwanza Wanafunzi wa Maeneo hayo.
Akiwasalimia Wananchi, Wazazi, Walimu pamoja na wanafunzi wa Skuli hizo katika mikutano tofauti Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipongeza wazo la Wananchi kwa jitihada zao za kuanzisha michango iliyoibua mwanzo wa Ujenzi wa Majengo hayo.
Balozi Seif alisema mawazo hayo ni busara ambazo Serikali Kuu imeunga mkono kwa kudhamiria kuimarisha Sekta ya Elimu ili kuwajengea mazingira bora Wanafunzi ikiwemo vikalio yatakayowawezesha kumudu vyema masomo yao.
Aliwapongeza Wanafunzi waliomaliza masomo yao ya Kitato cha Sita mwaka uliopita kwa kufanya vyema kwenye mitihani yao jambo ambalo limeleta faraja kwa Wazazi na Serikali kwa ujumla.
Alisema Heshima ya Zanzibar katika ufaulu wa Wananafunzi iko mikononi mwa Wanafunzi wenyewe  kwa asilimia 80% na ile iliyobakia ya asilimia 20% inatokana na jitihada za walimu pamoja na Wazazi.
Aliwataka Wanafunzi waendelee kusoma kwa bidii hasa masomo ya sayansi ili kuongeza Wataalamu wa kutosha katika fani ya uhandisi ambayo inaonekana kuendelea kukumbwa na upungufu.
Naye Mwakilishi wa Jimbo la Mkoani ambae pia ni Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Mh. Mmanga Mjengo Mjawiri alisema ifikapo Mwaka 2020 Ilani ya CCM pamoja na ahadi zilizotolewa ndani ya Jimbo hilo zitakuwa zimekamilika.
Mh. Mmanga alisema kwa sasa tayari asilimia 99% ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM pamoja ana ahadi imeshafikiwa na juhudi zinakamilishwa katika ujenzi wa Kisima cha Maji safi na salama katika Skuli ya Sekondari ya Mohamed Juma Pindua ili kuwahudumie Wanafunzi wa Skuli hiyo pamoja na Wananchi jirani wanaoizunguuka Skuli hiyo.
Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliikagua Bara bara inayojengwa katika kiwango cha Lami iliyoanzia katika Kijiji cha Ole hadi Kengeja yenye urefu wa Kilomita 35 ambayo tayari imeshafikia Kilomita 17 sasa.
Afisa Mdhamini Wizara ya Ujenzi mawasiliano na Usafirishaji Pemba  Nd. Ahmed Baucha alisema Bara bara hiyo iliyoanza mchakato wake Mwaka 2009 2014 na ujenzi rasmi ukaanza Mwaka 2016  na kubakisha Kilomita 18.
Nd. Baucha alisema  kuchelewa kwa mradi huo kunatokana na uhaba wa vifaa vya ujenzi jambo ambalo kwa sasa limeshapatiwa ufumbuzi na Serikali na harakati zimeongezeka na kufikia Kilomita  21 katika usafishaji mbapo kwa utandikaji wa Kifusi umeshafikia Kilomita 19.
Alisema mradi huo umekisiwa kukamilika Mwezi Juni mwaka ujao wa 2020 na kuondosha kabisa usumbufu waliokuwa wakiupata Wananchi wa Vijiji vilivyomo ndani ya Wilaya ya Chake chake, Wete na Hata Mkoani.
Akitoa sukrani zake kwa jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na wahandisi Wazalendo wa ujenzi wa Bara bara hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  amesisitiza umuhimu wa kujengwa kwa Bara bara ya kiwango kwa vile tatizo la uhaba wa Vifaa limeshapitiwa ufumbuzi wake na Serikali Kuu.
 Balozi Seif alisema hata hivyo licha ya uwepo wa Vifaa hivyo lakini bado Wizara ya Ujenzi inapaswa kuzingatia muda wa Mradi. Hivyo Uongozi wa Wizara hiyo usione uzito kukodi magari kwa ajili ya kuongeza nguvu hasa katika suala la umwagaji wa kifusi ili zoezi hilo la muda mrefu liweze kuwahi wakati.
Aliagiza ulipwaji wa fidia kwa wale wenye mali na vipando vyao  ni lazima ukazingatiwa vyema  wakati na busara ili kuondosha malalamiko ambayo baadae huwasilishwa Serikalini wakati bajeti ya kufanya hivyo imeshapitwa na wakati.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.