Habari za Punde

Balozi Seif azungumza na jumbe wa Viongozi Waandamizi kutoka Jimbo la Zhejing Nchini Jamuhuri ya Watu wa China

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kushoto alisema akipokewa na Ujumbe wa Viongozi Waandamizi wa kutoka Jimbo la Zhejing  Nchini China katika Hoteli ya Park Hayart Shangani kwa Mazungunzo.
 Balozi Seif kati kati akiuongoza Ujumbe wa Zanzibar katika mazungumzo na Ujumbe wa Viongozi Waandamizi wa kutoka Jimbo la Zhejing  Nchini China katika Hoteli ya Park Hayart Shangani
  Balozi Seif akisisitiza jambo wakati akiendelea na mazungumzo na Ujumbe wa Viongozi Waandamizi wa kutoka Jimbo la Zhejing  Nchini China, kushoto yake ni Waziri wa Biashara Balozi Amina Salum Ali.
 Kiongozi wa Ujumbe huo wa Viongozi Waandamizi  kutoka Jimbo la Zhejing  Nchini China  ambae pia ni Mwenyekiti wa Jimbo hilo Bibi Ge Huijun  akielezea azma ya Wawekezaji wa Jimbo lake kutaka kufungua milango ya Uwekezaji Visiwani Zanzibar.
Balozi Seif kulia akimpatia zawadui ya Kasha Mwenyekiti wa Jimbo la Zhejing  Nchini China Bibi Ge Huijun mara baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika Park Hayart Shangani Mjini Zanzibar.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Zanzibar inahitaji Utalii wa daraja la kwanza utakaokwenda sambamba na miundombinu ya Viwanda katika muelekeo wake wa kuimarisha Uchumi utakaoustawisha maisha ya Wananchi na kuongezeka kwa Mapato ya Taifa.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliamua kuelekeza nguvu zake katika sekta hizo ili kuondokana na utegemezi wa zao moja la Karafuu lililotegemewa kwa karne kadhaa zilizopita ambapo liliwahi kutetereka katika soko la Dunia ndani ya Miaka ya Tisini.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa Kauli hiyo wakati akizungumza na Ujumbe wa Viongozi Waandamizi kutoka Jimbo la Zhejing Nchini Jamuhuri ya Watu wa China ukiongiozwa na Mwenyekiti wake Bibi Ge Huijun hapo katika Ukumbi wa Hoteli ya Park Haryat  Shangani Mjini Zanzibar.
Alisema Sekta ya Utalii Zanzibart tayari imeanza kuleta matumaini makubwa kutokana na kukuwa kwa Uchumi na Mapato ya Taifa sambamba na kustawisha Maisha ya Wananchi kunakotokana na ongezeko la Watalii wanaotembelea Visiwa vya Zanzibar.
Balozi Seif alisema ujio wa Viongozi hao Waandamizi wakiwemo Wakurugenzi wa Taassisi tofauti pamoja na Makampuni ya Miradi ya Kiuchumi ya Jimbo hilo utaongeza chachu kwa Watalii wa Nchi hiyo la Bara la Asia kupanga ratiba zao za matembezi Visiwani Zanzibar.
Alisema zipo Fukwe adimu kupatikana katika maeneo mengine Duniani, vivutio vya Utalii, Rasilmali za Baharini pamoja na Utamaduni wa asili vinavyotoa ushawishi kwa muwekezaji ye yote kuitumia fursa hiyo ya soko la Utalii katika Kuwekeza Miradi ya Hoteli.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliipongeza China kwa uamuzi wake wa kushirikiana na Mataifa ya Bara la Afrika katika azma ya kusaidia kunyanyuwa hali za Kiuchumi za Mataifa hayo yaliyobarikiwa kuwa na Rasilmali nyingi am,bazo bado hazijatumika ipasavyo.
Balozi Seif  alisema  Makampuni na Taasisi za Uwekezaji za Majimbo mbali mbali Nchini China yanaweza kulitumia Soko la Afrika Mashariki na Mataifa yaliyopo Mashariki na Kusini mwa Bara la Afrika  katika kuwapatia huduma za msingi Wakaazi wake wanaokaridiwa kufikia Milioni Mia Tatu.
Alisema hilo soko la pamoja la Afrika Mashariki lakini bado halijeweza kukidhi yale mahitajio halisi kutokana na kukosekana kwa Taalamu na mbimu kwenye masuala ya Uwekezaji Vitega Uchumi na matokeo yake baadhi ya bidhaa hadi sasa zinatoka nje ya maeneo hayo.
Mapema Kiongozi wa Ujumbe huo wa Viongozi Waandamizi  kutoka Jimbo la Zhejing  Nchini China  ambae pia ni Mwenyekiti wa Jimbo hilo Bibi Ge Huijun  alisema Rasilmali ya Asili inayopatikana Visiwani Zanzibar inawahamasisha Wawekezaji wa Jimbo lake kutaka kuwekeza Zanzibar.
Bibi Ge Huijun alimueleza Balozi Seif  kwamba Wawekezaji wa Jimbo lake wako tayari kuwekeza Miradi yao katika mfumo wa kubadilishana uzoefu katika Miradi ya Kiuchumi na Biashara katika dhana ya kuimarisha uhusiano wa miaka mingi uliopo kati ya China na Tanzania na Zanzibar kwa jumla.
Alisema katika mikakati miyo itayoanza kufanyiwa kazi mara moja Sekta ya Uitalii itapewa msukumo wa kipekee na kutiliwa mkazo utakaowahusisha Watalii kutoka China kufanya ziara za kimatembezi moja kwa moja hadi Tanzania na Zanzibar.
Mwenyekiti huyo wa Jimbo la Zhejing alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba China kupitia mpango wake wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Biashara na Afrika itaendelea kuongeza nguvu kadri mazingira yatavyoruhusu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Ujumbe huo wa Viongozi 15 Waandamizi kutoka Jimbo la Zhejing Nchini Jamuhuri ya Watu wa China ukiongiozwa na Mwenyekiti wake Bibi Ge Huijun upo Nchini Tanzania kwa ziara ya Siku Nne kutembelea maeneo mbali mbali ya Kiuchumi Historia na Biashara.
Jamuhuri ya Watu wa China imekuwa mshirika mkubwa wa Tanzania katika nyanja mbali mbali tokea Miaka ya 60 mara baada ya kupatikana kwa Uhuru wa Tanganyika na Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.