Habari za Punde

HESLB YAONGEZA MUDA WA KUOMBA MKOPO HADI AGOSTI 23

Na Mwandishi Wetu
Alhamisi, Agosti 15, 2019
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza kuongeza muda wa kuomba mkopo kwa njia ya mtandao kwa siku tano hadi Ijumaa,Agosti 23, 2019 ili kuwapa fursa waombaji ambao hawajakamilisha maombi yao kutumia muda ulioongezwa kufanya hivyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru (pichani) amesema jijini Dar es salaam leo (Alhamisi, Agosti 15, 2019) kuwa HESLB ilianza kupokea maombi ya mkopo Julai 1 mwaka huu na tarehe ya mwisho ilikua Agosti 15, 2019.

Kwa mujibu wa Badru, HESLB imepokea maombi kutoka kwa baadhi ya waombaji mikopo ambao hawajakamilisha maombi yao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kukosa nyaraka muhimu.

“Ingawa hadi leo (Agosti 15, 2019) tumeshapokea maombi zaidi 74,821 yaliyokamilika kwa njia ya mtandao, tumepokea pia maombi kutoka kwa wateja wetu wakitaka kuongezewa muda ili wakamilishe nyaraka muhimu kama nakala za vyeti vya vifo vya wazazi wao, barua kutoka kwa wadhamini wao na nyaraka nyinginezo … tumewasikiliza na kuongeza muda,” amesema Badru.

Mkurugenzi Mtendaji huyo amewataka waombaji mkopo ambao hawajakamilisha maombi yao kutumia muda ulioongezwa kukamilisha maombi yao kwa kuwa HESLB haitaongeza muda zaidi baada ya tarehe 23 Agosti mwaka huu.

“Tunasihi waombaji wetu watumie muda huu ulioongezwa kukamilisha maombi yao kwa kuwa hatutaongeza tena. Baada ya Agosti 23, tutaanza kufanya uchambuzi wa maombi tuliyopokea ili tuwapangie mikopo wenye sifa kwa wakati na tupeleke fedha za mikopo vyuoni kabla vyuo havijafunguliwa,” amesema Badru.

Katika kipindi kilichoongezwa cha hadi Agosti 23, Badru amesema dawati la huduma kwa wateja la HESLB klitakuwa wazi ili kutoa ufafanuzi kwa waombaji mkopo pale utakapohitajika. Dawati hilo linapatikana kuanzia saa 2:30 asubuhi – saa 11:30 jioni kupitia:

Simu:                         0736 665533 au 0738 66 55 33 au 022 5507910
Barua pepe:         adcp@heslb.go.tz au info@heslb.go.tz

Taarifa hii pia inapatikana kwenye tovuti ya HESLB www.heslb.go.tz

Imetolewa na:
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu,
DAR ES SALAAM

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.