Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi MheDk. Ali Mohamed Shein Amefanya Uteuzi wa Viongozi Mbalilmbali Katika Taasisi za SMZ Leo.RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo amefanya uteuzi wa viongozi katika taasisi mbali mbali za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Walioteuliwa ni Ali Khamis Juma kuwa Mkurugenzi wa Jiji la Zanzibar katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ.

Mwengine ni Khadija Khamis Rajab ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu katika Wizara ya Biashara na Viwanda, Hanifa Ramadhani Said ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Msaada wa Kisheria katika Wizara ya Katiba na Sheria.

Masoud Ali Mohamed ameteuliwa kuwa Ofisa Mdhamini Pemba katika Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mattar Zahor Masoud ameteuliwa kuwa Ofisa Mdhamini Pemba katika Wizara ya Katiba na Sheria.

Aidha, Rais Dk. Shein amemteua Dk. Haji Ali Haji kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Mkonga wa Mawasiliano wa Zanzibar katika Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji.

Pia, Rais Dk. Shein amemteua Shukuru Awadh Suleiman kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Mkonga wa Mawasiliano wa Zanzibar katika Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji.

Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari  na kusainiwa na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, uteuzi huo umeanza rasmi leo tarehe 6 Agosti, 2019.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.