SERIKALI
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
zinaendelea kuchukua hatua za kisera na za kimkakati katika ujenzi wa uchumi wa
viwanda ili Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ifikie hadhi ya nchi ya uchumi wa kati.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.
Ali Mohamed Shein, ameyasema hayo leo katika ufungaji wa Maadhimisho na
Maonesho ya Nne ya wiki ya Viwanda ya Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa
Afrika (SADC) hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa
Julius Nyerere, jijini Dar-es-Salaam.
Katika hotuba yake, Rais Dk. Shein alisema kuwa utekelezaji
wa miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo miradi ya umeme, barabara, reli, bandari
na viwanja vya ndege unalenga katika kujenga misingi imara ya ukuaji wa sekta
ya viwanda na biashara ambazo muhimu katika kutatua changamoto za ajira na
kuongeza kasi ya uchumi.
Aliongeza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania
na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zinaendelea kuimarisha sekta binafsi kwa
lengo la kuhakikisha kwamba inaongeza fursa za ajira kwa vijana wanaomaliza
masomo yao kwa ngazi zote.
Alieleza kuwa maonesho hayo aliyoyafunga yamesaidia na
yatakuwa na mchango mkubwa katika utekelezaji wa mipango na mikakakti iliyopo
ya kuleta mageuzi makubwa ya uchumi wa viwanda katika nchi zote 16 wanachama wa
SADC.
Alisema kuwa taaluma, ujuzi na maarifa yaliyopatikana
katika maadhimisho na maonesho hayo itatumika katika kukuza ubunifu wa
kuendeleza viwanda, utafutaji wa masoko pamoja na kukuza uhusiano baina ya
wazalishaji, wanunuzi, wasafirishaji na watumiaji bidhaa zinazozalishwa na
viwanda vya nchi wanachama wa SADC.
Rais Dk. Shein alisema kuwa kauli mbiu ya Maadhimisho na
Maonyesho ya SADC mwaka huu 2019 ambayo
imeweka msisitizo katika mazingira ya viwanda inakwenda sambamba na juhudi
zinazochukuliwa za kuimarisha viwanda na Serikali zote mbili.
Alieleza matumaini yake kwamba maazimio yote yaliyofikiwa
kwa pamoja katika vikao hivyo yatafanyiwa kazi na Sekretarieti ya SADC kwa
kushirikiana na nchi wanachama na yawe msingi na kichocheo cha mafanikio ya
utekelezaji wa Mpango Mkakati wa kikanda na nchi wanachama.
Alisema kuwa kazi iliyo mbele hivi sasa ni kuhakikisha
kwamba kila mmoja anaunga mkono utekelezaji wa maazimio yaliyopitishwa katika
vikao vilivyofanyika pamoja na mikakati ya Serikali zote ya kuendeleza viwanda
kwa kununua na kuzipenda bidhaa za viwanda vya ndani ya nchi za SADC.
“Tujenge utamaduni
wa kuwapenda na kuwatumia wataalamu wetu wa ndani na tuondokane na utegemezi wa
wataalamu wa nje, sambamba na kujenga misingi imara ya kuendeleza teknolojia
yetu wenyewe”,alisema Dk. Shein.
Aidha, alisema kuwa kufanya hivyo ni kutafsiri kivitendo
ile dhamira ya nchi wanachama wa SADC kuunda umoja wa SADC kwa ajili ya
kuongeza fursa ya masoko na ajira.
Rais Dk. Shein alisema kuwa nchi wanachama wa SADC wataweza
kuongeza masoko ya ajira ikiwa zitanunua bidhaa zinazozalishwa na wataalamu
wazalendo.
Kwa msingi huo Rais Dk. Shein alisisitiza haja na umuhimu
wa kuzingatia falsafa na hekima za Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, Rais wa
Kwanza wa Zanzibar kwa kuzingatia maneno aliyoyasema kwamba ”Tukuza kilicho chako
hadi usahau cha mwenzako”.
“Wakati umemfika wa kuhakikisha kwamba tunapenda kuzitumia
bidhaa zinazozalishwa na viwanda vyetu wenyewe”,alisisitiza Dk. Shein.
Vile vile, Rais
Dk. Shein alitoa shukurani za dhati kwa wanahabari wa vyombo vyote ambao kwa muda
wa wiki nzima walikuwa wakifanya kazi muhimu sana ya kuwapa habari wanachi kwa
kutangaza na kuhamasisha wananchi kuhusu matukio yote muhimu ambayo yalikuwa
yakifanyika katika viwanja hivyo.
Dk. Shein pia,
alitoa shukrani wka wenye viwanda katika nchi za Jumuiya ya SADC kutokana na
juhudi kubwa wanazizifanya katika kuongeza utengenezaji wa bidhaa za viwandani
ikiwa ni pamoja na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo,mifugo, uvuvi, uchimbaji
madini na utengenezaji wa mashine na mitambo ya ain azote.
Alisisitiza
kuwa fursa ya kuimarisha ushirikiano waliyoipata katika maadhimisho na maonesho
hayo lazima iendelezwe katika nyanja zote za kiuchumi na kijamii, ili kuifanya
Jumuiya ya SADC kuwa imara zaidi na yenye nguvu kubwa katika masula muhimu ya
kikanda na Kimataifa.
Dk. Shein alilipongeza
wazo la kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa ni miongoni mwa lugha rasmi za
mawasiliano katika majukwaa ya SADC kwani ni hatua muhimu katika kuimarisha
umoja na mshikamano kwa Wanachama wa Jumuiya hiyo.
Sambamba na
hayo, Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwaalika washiriki wa mkutano huo wa
SADC katika maonyesho makubwa yaualii ya Zanzibar “Zanzibar Tourism show”
yatakayofanyika mwishoni mwa mwezi wa Septemba, 2019.
Rais Dk. Shein
alisisitiza haja kwa wanachama wan chi za SADC kutochukua muda wa kukutana
kwani hatua hiyo inapunguza nguvu za hamasa ya kuwa pamoja kidugu katika
shughuli za Jumuiya hiyo kwa maslahi ya nchi hizo na bara zima la Afrika.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment