Habari za Punde

VIJANA MKOANI RUVUMA WACHANGAMKIA FURSA YA MAFUNZO YA UJASIRIAMALI

Katibu Mtendaji wa Balaza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Bi. Beng’I Issa akizungumza na Vijana wa Mkoa wa Ruvuma kuhusu Programu ya Mafunzo ya Ujasiriamali na Usimamizi wa Biashara wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo katika Mkoa wa Ruvuma, Agosti 10, 2019.
Baadhi ya vijana wanaojishughulisha na shughuli za kiuchumi wakifuatilia maelezo ya Katibu Mtendaji wa Balaza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Bi. Beng’I Issa (hayupo pichani) alipokuwa akielezea kuhusu Programu ya Mafunzo ya Ujasiriamali.

Na; Mwandishi Wetu
Vijana Mkoa wa Ruvuma wamefurahia fursa ya mafunzo ya ujasiriamali na usimamaizi wa biashara yaliyotolewa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo yatawawezesha vijana hao kukuza na kurasimisha shughuli zao za kiuchumi.
Akifungua Mafunzo hayo Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bi. Beng’I Issa alieleza kuwa mafunzo hayo ya ujasiriamali ni muhimu sana na yanalenga kuwawezesha vijana wanaomiliki biashara wanapata mbinu za kuendeshaji na kusimamia biashara zao.
“Mafunzo haya ya ujasiriamali yameleta tija kwa vijana na wameweza kujiajiri kwa kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi zenye faida,” alisema Issa
Alieleza kuwa vijana wanapaswa kuchangamkia fursa hizo zinapojitokeza ili waweze kuunganishwa na fursa za mitaji na mitandao ya huduma za biashara, pia kuwajengea uwezo wa kufanya shughuli zao za kiuchumi kwa kujiamini na kuweza kuweza kupata faida.
“Vijana mnapaswa kutambua ninyi ndio nguvukazi ya Taifa, hivyo kuwa wabunifu ni jambo la msingi katika biashara zenu mkitambua fursa mlizonazo ili muweze kushindana katika biashara,” alisema Issa
Akibainisha aina ya mafunzo ya ujasiriamali watakayopatiwa vijana hao yakiwemo masuala ya uchambuzi wa masoko, dhana ya ujasiriamali, uchambuzi wa mahitaji ya mteja, kutambua ushindani wa soko, mkakati na uendeshaji biashara, utambuzi wa masoko, usimamizi wa fedha, vihatarishi vya biashara na namna ya kuvikabili, usimamizi wa biashara na rasilimali watu, urasimishaji wa biashara na vyanzo vya mitaji.
Aliongeza kuwa Programu hii ya mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana itawawezesha kutambua mapungufu waliyonayo na kutumia mwanya huo kuangalia fursa walizo nazo katika ushindani wa biashara zao.
“Ni muhimu vijana mkawekeza katika biashara mnazozimudu kimtaji, kiusimamizi kwa ushindani na kufanya maamuzi sahii,” alieleza Issa
Alieleza kuwa kila Mkoa una fursa zinazoweza kutumiwa na wajasiriamali katika kujiendeleza kiuchumi, vijana wanatakiwa kuchangamkia fursa hizo ili waweze kunufaika kwa njia mbalimbali.
Alifafanua kuwa Ofisi yake imekuwa ikiendesha mafunzo ya aina hii kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Taasisi za Umma, Wadau wa Mendeleo, Sekta binafsi na jamii kwa ujumla.
“Zaidi ya Vijana 10,000 wameweza kufikiwa na programu mbalimbali za mafunzo ikiwemo Kijana jiajiri, Ajira yangu, Kliniki ya vijana wahitimu wa vyuo vya elimu ya juu, mifuko ya uwezeshaji na watoa huduma,” alisema Issa
Aidha, alitoa shukrani zake kwa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuona haja ya kuwekeza kwa vijana kwa kuwapatia ujuzi ili waweze kujiajiri, kuajiri na kuchangia katika pato la taifa.
Kwa Upande wake, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Bw. Hakimu Mafuru amewahimiza vijana wa Mkoa huo kuchangamkia fursa za mafunzo kama hayo yanayotolewa na Serikali pamoja na wadau mbalimbali kwa kuwa yatawawezesha kujitambua na kujisimamia wenyewe na kuongeza tija kwenye biashara zao.
Mmoja wa Vijana walioshiriki katika Mafunzo hayo, Bi. Pudencia Msangawale alieleza kuwa mafunzo hayo yatajibu changamoto ambazo wamekuwa wakikumbana nazo kama wajisiriamali ikiwemo masuala ya ujuzi, maarifa, kurasimisha biashara, namna bora ya kuhudumia wateja na utafutaji wa masoko.
“Ninawashukuru Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwa elimu waliyotupatia yametuwezesha kujitambua, kuwa wabunifu, waaminifu na kuweza kujisimamia katika biashara,” alisema Msangawale.
Mafunzo hayo yanaratibiwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo yatafanyika katika Mikoa nane (8) ya Tanzania Bara ikiwemo Dodoma ambapo tayari yamekisha fanyika, Ruvuma, Geita, Mwanza, Lindi, Mbeya, Tanga na Arusha.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.