Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akizungumza na Waziri anayeshuhulikia Mashirika yanayomilikiwa na Serikali ya Indonesia Bibi.Rini M.Soemarno (wa pili kulia) leo alipofika Ikulu Mjini Zanzibar akiwa na ujumbe wake.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein ameipongeza azma ya Serikali ya Indonesia ya kuja kuekeza
Zanzibar kupitia Makampuni na Mashirika yake ya Umma kutokana na fursa zilizopo
hapa nchini.
Rais Dk. Shein
aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya
mazungumzo na Waziri anayeshughulikia Mashirika yanayomilikiwa na Serikali ya
Indonesia Bi Rini Mariani Soemano.
Bi Rini Mariana amefuatana
na ujumbe wake wa watu 30 akiwemo Balozi wa Indonesia katika Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dk. Ratlan Pardede na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
nchini Malaysia ambaye pia, anaiwakilisha Tanzania nchini Indonesia Balozi Dk.
Ramadhan Kitwana Dau.
Katika maelezo yake, Rais
Dk. Shein alimueleza Waziri Soemarno kuwa azma hiyo ya Serikali ya Indonesia ni
hatua moja wapo ya kukuza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano ulioasisiwa na waasisi
wa Mataifa hayo akiwemo Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati
Soekarno Hatta Baba wa Taifa la Indonesia
Rais Dk. Shein
alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kushirikiiana na
Makampuni na Mashirika yote ya Umma ya Indonesia yalioonesha azma ya kuja
kuekeza hapa Zanzibar katika sekta mbali mbali za maendeleo.
“Sisi ni wamoja na
tuna urafiki na udugu wa damu ulioasisiwa na viongozi wetu hao ambao ni waasisi
wa Mataifa hayo hivyo, ni vyema tukauimarisha kwa nguvu zetu zote uhusiano wetu
na ushirikiano tulionao licha ya kuwa tuko mbali lakini bahari ya India ‘Ocean’
isitugawe”,alisema Dk. Shein.
Aidha, Rais Dk. Shein
aliipongeza Serikali ya Indonesia kwa kuendeleza uhusiano na Ushirikiano huo
uliodumu kwa miaka 55 hivi sasa, na kueleza kuwa Zanzibar ina fursa nyingi za
uwekezaji sambamba na mazingira mazuri yaliyowekwa na Serikali kwa ajili ya
wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Rais Dk. Shein
alimueleza kiongozi huyo kuwa hatua hiyo pia ni miongoni mwa matunda na
mafaniko yaliyotokana na ziara yake aliyoifanya nchini Indonesia mwezi Agosti
mwaka jana 2018 ambapo alipata fursa ya kuzungumza na mwenyeji wake Makamo wa
Rais wa nchi hiyo Muhammad Jussuf Kalla masuala mbali mbali ya maendeleo.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein alieleza kuwa ujio wa Waziri Bi Rini Soemarno unaonesha mwanzo mzuri
wa mashirikiano hayo katika kuendeleza sekta mbali mbali za maendeleo zikiwemo
uwekezaji, biashara, utalii, kilimo, miundombinu na nyengienzo.
Rais Dk. Shein
alieleza haja ya kuimarisha ushirikiano katika sekta ya utalii hasa
ikizingatiwa kuwa nchi hiyo imepiga hatua kubwa katika masuala ya utalii huku
akieleza jinsi watalii kutoka Indonesia wanaokuja kutalii Zanzibar
wanavyongezeka kila mwaka.
Dk. Shein aliunga
mkono mazungumzo ya Waziri huyo alieleeza jinsi Serikali yake itakavyoangalia
suala zima la kuwepo kwa usafiri wa ndege kati ya Indonesia na Zanzibar kupitia
Madagasca hatua ambayo pia, itakuza sekta ya utalii na biashara baina ya pande
mbili hizo.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein alieleza haja ya kuimarisha sekta ya biashara baina ya pande mbili
hizo hasa ikizingatiwa kuwa Zanzibar na Indonesia zina historia ya biashara
ikiwemo biashara ya zao la karafuu.
Dk. Shein pia,
alitilia mkazo suala zima la kuimarisha uhusiano na ushirikiano kwa njia ya
kutembeleana kwa azma ya kupanua wigo wa kimaendeleo kati ya viongozi na
watendaji mbali mbali jambo ambalo limekuwa likienda vizuri hadi hivi leo.
Mapema Waziri
anayeshughulikia Mashirika yanayomilikiwa na Serikali ya Indonesia Bi Rini
Mariani Soemano alimueleza Rais Dk. Shein azma ya Serikali ya Indonesia ya
kuleta Kampuni na Mashirikia yake kuja kuangalia fursa za kuekeza hapa
Zanzibar.
Waziri Soemarno
alieleza kuwa mazingira ya Zanzibar yameshabihiana na yale ya Indonesia hivyo
ni rahisi kuja kuekeza hasa ikizingatiwa vivutio kadhaa vilivyopo hapa Zanzibar
sambamba na hatua zinazochukuliwa na Serikali kwa wawekezaji.
Waziri huyo alieleza
kuwa Makampuni na Mashirika ya nchini Indonesia yamevutiwa zaidi na jinsi ya
viongozi wa Serikali ya Mapinduzi wanavyowajali
wageni wakiwemo ndugu zao wa Waindonesia jambo ambalo limewapa faraja
kubwa.
Aidha, Waziri huyo
alitumia fursa hiyo kumpa Rais Dk. Shein salamu kutoka kwa Rais wa Indonesia Joko
Widodo na kusisitiza kuwa nchi hiyo
itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza na kuimarisha sekta za
maendeleo.
Waziri Soemarno ambaye
amefuatana na ujumbe wa watu 30 wakiwemo viongozi wa Mashirika mbali mbali ya
Umma yanayoshughulikia masuala ya reli, huduma za viwanja vya ndege, mafuta na
gesi asilia, benki, fedha na sekta ya miundombinu alimueleza Rais Dk. Shein
kuwa Serikali yake ina hamu katika kutekeleza jambo hilo.
Pia, Waziri huyo
alimueleza rais Dk. Shein kuwa katika ziara yake ya siku mbili hapa Zanzibar
atakutana na viongozi mbali mbali wa Serikali ambao watajadiliana masuala mbali
mbali ya ushirikiano katika sekta kadhaa zikiwemo miundombinu, fedha, Wakala wa
Maji na Nishati (ZURA), kukutana na Waziri wa Fedha Balozi Mohammed Ramia
Abdiwawa pamoja na kutembelea eneo linalotarajiwa kujengwa bandari ya mafuta na
gesi huko Mangapwani.
Pamoja na hayo, Waziri Soemarno alimueleza Rais Dk. Shein
jinsi Serikali yake itakavyoliangalia kwa umakini zaidi suala la kukuza ushirikiano
katika usafiri wa anga kati ya nchi hiyo na Zanzibar hasa ikizingatiwa kwamba
tayari kuna safari za ndege kati ya Indonesia na Madagasca.
Waziri Soemarno
alieleza kuwa Serikali ya Indonesia inathamini juhudi za waasisi wa Mataifa
hayo na kuahidi kuwa uhusiano na ushirikiano utaendelezwa katika sekta mbali mbali
za maendeleo ikiwemo za kiuchumi baina ya pande mbili hizo na kusukuma mbele maendeleo
kwenye sekta ya bandari, fedha, viwanda, usafiri na miundombinu.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment