Habari za Punde

Balozi Seif mgeni rasmi katika maulidi ya Uzawa wa Nabii Muhammad {SAW} Temeke

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akihutubia Waumini wa Dini ya Kiislamu kwenye Maulidi ya Uzawa wa Nabii Muhammad {SAW} yaliyoandaliwa na Uongozi wa Msikiti wa Majumat Islamia uliopo Temeke Jijini Dar es salaam.
 Balozi wa Comoro Nchini Tanzania Bwana  Ahmed Said Badwi akisoma Mlango wa Kwanza wa Barzanj  kwenye Maulidi ya Uzawa wa Nabii Muhammad {SAW} yaliyofanyika Temeke Jijini Dar es salaam.
 Baadhi ya Maelfu ya Waumini wa Dini ya Kiislamu waliohudhuria Maulidi ya Uzawa wa Nabii Muhammad {SAW} yaliyofanyika Temeke Jijini Dar es salaam na kuandaliwa na Uongozi wa Masjid Majumat Islamia.
 Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Aboubakar Zubeir Ali akitoa chakula cha Moyo kwa Waumini wa Dini ya Kiislamu waliohudhuria Maulid ya Uzawa wa Nabii Muhammad {SAW}  hapo Temeke  Jijini Dar es salaam.
Mlezi wa Msikiti wa Ijumaa wa Majumat Islamia Temeke Jijini Dar es salaam Rais Mstaafu wa Tanzania Awamu ya Pili Mzee Ali Hassan Mwinyi akitoa salamu zake kwenye hafla hiyo ya Maulidi Temeke Mjini Dar es salaam.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania  inajivunia maendeleo makubwa ya Kiuchumi  yaliyopatikana Bara na Zanzibar kutokana na Sababu kubwa ya uwepo wa Amani na Utulivu unaowapa Waanchi kuwajibika ipasavyo katika harakati zao za kila siku.
Alisema Kikundi au Mtu ye yote atakayejaribu kuhatarisha Amani na utulivu huo wa Taifa, Mshikamano wa Jamii na Umoja wa Wananchi lazima ieleweke kwamba huyo  ni adi na inapaswa kupambana dhidi yake  kwa nguvu zote za Umma.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo katika hafla ya Maulidi ya uzawa wa Kiongozi wa Umma wa Dini ya Kiislamu Duniani Mtume Muhammad {SAW} yaliyofanyika Temeke Jijini Dar es salaam.
Alisema Watanzania wote wanapaswa kumshukuru Mwenyezi Muungu kwa nguvu zake zilizowezesha kupatikana kwa neema ya Amani inayoendelea kusimamiwa vyema na Viongozi wake Wakuu Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein.
Balozi Seif alisema juhudi za Viongozi hao katika usimamizi wa ujenzi wa Taifa chini ya kivuli cha Amani ziko wazi zikionekana kuipaisha Tanzania katika Heshima kubwa  Kimataifa.
Alitanabahisha kwamba Viongozi wa aina hii waliojitolea nguvu na nafsi zao kwa wale wanaowaongoza, kamwe hawatakosa upinzani na maadui ambao daima hawatakuwa tayari kuridhia juhudi hizo za kuing’arisha Dola la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akiendelea kukemea kila mara vitendo vya udhalilishaji, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwakumbusha Waumini hao waliohudhuria maulidi ya Uzawa wa Mtume Muhammad {SAW} kwamba kila mmoja abebe dhima ya  kuwa mchunga wa mwenzake dhidi ya kupiga vita vitendo hivyo viovu.
Alisema Vitendo vya udhalilishaji ikiwemo ubakaji, kutelekezwa kwa Watoto na Talaka zisizofuata utaratibu wa Kiislamu vinakwenda kinyume na maamrisho ya Mwenyezi Mungu pamoja na mwenendo mzima wa Kiongozi Mkuu wa Waumini wa Dini ya Kiislamu Nabii Muhammad {SAW}.  
Balozi Seif alifahamisha kwamba kila Muumini aendelee kumsifu na kumtukuza Mtume Muhammad {SAW} kwa kukemea na kukataza vitendo vyote vya udhalilishaji katika Jamii nzima ikiwemo biashara haramu na mbaya kabisa ya Dawa za kulevya zinazovuruga nguvu kazi ya Taifa ambayo ni Vijana.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwakumbusha Wananchi kwamba Mwaka 2019 unamalizika na kuingia Mwaka 2020 wakielewa kuwa ndio Mwaka wa Uchaguzi Mkuu kwa Watanzania wote ambao ni haki ya Kidemokrasia ya kila Mwananchi aidha kwa kuchagua au kuchaguliwa.
Balozi Seif aliwataka wajiandae vyema na Uchaguzi huo huku wakifuata maelekezo ya Tume zote mbili ile ta Taifa { NEC} na ile ya Zanzibar {ZEC} wakiweka dhamira moyoni mwao ya kuhakikisha Uchaguzi unafanyika na kumalizika kwa salama, huru na Haki.
Alisema ni vyema wakati wa Kampeni utakapowadia wafuasi na Viongozi wa vyama vya Siasa wakazingatia Kampeni za kistaarabu zitakazoepuka matusi na vurugu ili hatiame kura zipigwe kwa salama huku wananchi wakisubiri matokeo kwa amani na hatimae kupokelewa kwa furaha na utulivu.
“ Tumuombe Mwenyezi Mungu atuzidishie upendo, Umoja na Mshikamano katika Taifa letu bila ya kujali, rangi, kabila au dini ya Mtu au kikundi cha Watu”. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisisitiza kwamba Uchaguzi utakuja na kupita, lakini maisha bado yataendelea baadae wakati Tanzania bado itaendelea kuwepo.
Akigawa chakula cha moyo kwa Waumini waliohudhuria Hafla hiyo ya Maulidi Imam wa Msiki wa Mtoro Jijini Dar es salaam Sheikh Othman Khamis alisema Nabii Muhammad {SAW} ameiacha Jamii ya Waumini wa Dini ya Kiislamu katika nuru iliyotukuka katika Maisha ya Dunia na Akhera.
Sheikh Othman Khamis alisema Jamii ya wakati huo wa Maisha ya Mtume Muhammad  {SAW} ilishiba Malezi na tabia njema hazina ambayo kwa Kizazi cha sasa imepotea kabisa.
Imam Mkuu huyo wa Msikiti wa Ijumaa wa Mtoro alisisitiza na kutanabahisha kwamba endapo Jamii na Wananchi wote watakubali kushiba Maadili, Serikali pamoja na Taasisi zake kama Polisi, Mahakama hazitakuwa na kazi ya kufanya baada ya kukosa kuwashughulikia watu wenye vitendo viovu wanapoamua kurejea katika uwanja wa Maadili mema.
Mapema Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Aboubakar Zubeir Ali alisema Waislamu wakati wote lazima waige kigezo na mwenendo wa Nabii Muhammad {SAW} wa ufasaha uliopambwa na ucheshi katika muda wa maisha yake aliyoishi ya kila siku.
Mufti Mkuu Zubeir alisema ghadhabu ni jambo baya lililoepukwa muda wote na Kiongozi huyo wa Umma wa Kiislamu akiwa na tabia ya upole, aliyeshiba subra sifa zinazopaswa kutawaliwa katika matendo ya kila siku ya Waumini wote wa Kiislamu.
Shekh Zubeir aliwaasa Viongozi wa Dini kuwa na tahadhari wakati wanapokuwa na wafuasi wao hasa kwenye mihadhara na Madara yanayohitaji umakini mkubwa utakaowapelekea kwenda kwenye njia sahihi.
Alisema wapo baadhi ya Viongozi wa Dini hutumia majukwaa kwa kukashifu Viongozi wenzao pamoja na madhehebu mengine kitendo ambacho hakipaswi kufanywa na ni vyema wakaendelea kuiga mfumo wa Nabii Muhammad {SAW} wakati alipokuwa na wasaidizi pamoja na wafuasi wake.
“ Hekima na busara ndani ya Mdarasa na Mihadhara lazima itawale ili kwenda sambamba na Amani ya Taifa inayotoa fursa pana kwa Waumini kuendelea kufanya Ibada zao kwa Utulivu na furaha”. Alisisitiza Mufti Mkuu huyo wa Tanzania Sheikh Zubeir.
Maulidi hayo ya uzawa wa Nabii Muhammad {SAW} Kiongozi wa Waumini wa Dini ya Kiislamu Duniani yameandaliwa na Uongozi wa Msikiti wa Majumat Islamiya wa Temeke Jijini Dar es salaam chini ya Mlezi wake Rais Mstaafu wa Tanzania Awamu ya Pili Mzee Ali Haasan Mwinyi ambaye naye alikuwepo kwenye shughuli hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.