Habari za Punde

Mafunzo ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka UNICEF

Na.Rahma Khamis na Ali Issa Maelezo –Zanzibar.  
Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mgeni Hassan Juma amesema watoto wanahaki ya kutoa Maoni yao mbele ya Wazazi wao na Viongozi wa kitaifa ili kuweza kuwatatulia changamoto zinazowakabili ndani ya familia zao.
Amesema hayo katika Ukumbi wa Baraza la wawakilishi Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar wakati walipokuwa wakipewa mafunzo na baraza la vijana na watoto la UNICEF kanda ya Zanzibar yaliotolewa na shirika hilo la kimataifa kuhusiana na mkataba wa haki za watoto nchini.
Amesema watoto wanahaki ya kuzungumzia masuala yanayowahusu wao binafsi kwa lengo la kurekebishwa baadhi ya mambo yanayowakwaza ikiwemo kunyimwa haki zao za kimsingi ,elimu,afya na malezi ili kupatiwa ufumbuzi.
Aidha amefahamisha kuwa mara nyingi baraza la Wawakilishi wanapokutana na  wajumbe hujadili mambo mbalimbali pasipo na kushirikishwa watoto, hivyo kwa nafasi hiyo ya kukutana na vijana hao itasaidia kuibua matatizo yanayowakumba hapa Zanzibar na Tanzania kwa jumla.
Naibu Mgeni  ameeleza kuwa takwimu zinaonesha takriban asilimia 40 ya wa Zanzibar ni watoto walio na umri wa miaka 18 (sensa ya mwaka 2012) na hao ndio watoto wanaowakilishwa kusemewa Barazani, hivyo wanahaki ya kusikilizwa na kufanyiwa kazi mawazo yao.
Nae Bi Usia Ledama kutoka UNICEF amesema kuwa haki za watoto zina misingi mikuu minne ambayo ndio dira ya mkataba wa haki za watoto,haki hizi ni pamoja na maslahi ya watoto,haki za maendeleo ya watoto, maswala yanayowahusu watoto, ulinzi na ushirikishwaji.
Amesema mkataba wa haki hizo unaelezea kuwa mtoto apatiwe haki zote ikiwemo malezi,elimu na afya bora.
Nae Nabiha kassim mtoto aliokua akitoa mawazo yake kwaniaba ya watoto wenzake waliofika hapo baraza la Wawakilishi waliomba Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kutobadilisha mfumo  wa elimu mara kwa mara kwani inapelekea watoto kupungua kiwango cha ufaulu kutokana na muda mfupi unapobadilishwa mtaala hiyo ikiwa karibu na mitihani.
Aidha wamefahamisha kua katika kuwafanya watoto kukua vizuri na kupata haki zao ni vyema Serikali kutengeneza miundombinu ilioyobora zaidi katika kitengo cha afya mama na mtoto ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kuhusu mlo bora kwa watoto wachanga ili waweze kuwa na afya na uwezo wa kuibua mambo.
Nae Abdullatif Hassan akizungumzia masuala ya maambukizi ya virusi vya ukimwi na unyanyapaa ameiomba Serekali ya Mapinduzi ya Zanzibar washirikiane na taasisi nyengine ikiwemo ZAPHA PLUS  kwa kutunga sheria za watoto waliothirika na maradhi hayo kua  pamoja na wasioathirika katika kitengo cha Ustawi wa jamii  ili kuondoa unyanyapaa na udhalilishaji kwa watoto hao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.