Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali.Mohamed Shein akihutubia Wanadiaspora wakati wa Ufunguzi wa Kongamano la Sita la Diaspora Tanzania lililofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Verde Mtoni Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein ameahidi kwamba atahakikisha anapomaliza muda wake wa Urais suala la Diaspora limeshakaa sawa
kimkakati, kisera pamoja na kisheria kwa upande wa Zanzibar.
Rais Dk. Shein
aliyasema hayo leo huko katika ukumbi wa Hoteli ya Verde, Mtoni Mjini Zanzibar
wakati akifungua Kongamano la Sita la Diaspora.
Katika maelezo yake
Rais Dk. Shein alisema kuwa anaamini kwamba kutakuwa imeiwekea mazingira mazuri
uongozi wa Awamu inayofuata ya Nane katika kulisimamia vizuri suala hilo.
Hivyo, Rais Dk. Shein
alimuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ahakikishe
kwamba anasimamia kwa karibu utayarishaji na kukamilika kwa rasimu ya sheria ya
Diaspora ili iweze kuwasilishwa katika Baraza la Wawakilishi kabla ya mwezi Mei, 2020.
Aliongeza kuwa kuwepo
na kutumika kwa Sera ya Diaspora iliyoizindua rasmi mwaka jana tarehe 09 Mei,
2018 kumerahisisha juhudi zinazoendelea kuchukuliwa hivi sasa za kutayarisha
Sheria ya Diaspora na amefurahishwa na matayarisho yaliyofikiwa.
“Katika mazungumzo
yangu niliyoyafanya na baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wiki
iliyopita, tarehe 7 Disemba, 2019, walinieleza kwamba wao wanapenda inakuwa
rahisi kwao kujadili na kupitisha sheria kwa masuala ambayo tayari
yameshatungiwa Sera”,alisema Dk. Shein.
Rais Dk. Shein alisema
kuwa katika kuhakikisha masuala ya kuuimarisha ushirikiano wa Wanadisapora na
nchi yao ya asili unakuwa endelevu, aliagiza Ofisi yake kutenga fedha kila mwaka katika bajeti ya Serikali,
kwa ajili ya kufanya makongamano hayo ambapo hapo mwanzo yalikuwa yakitegemea
michango ya wafadhili.
Aidha, Rais Dk. Shein
alieleza kufurahishwa kwake na Wanadisapora kwa kuzipokea vizuri juhudi
zinazochukuliwa na Serikali zote mbili za kuanzisha Diaspora kwani wamekuwa
wakishiriki vizuri katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo.
Kwa upande wa
Zanzibar, Rais Dk. Shein alitoa shukurani maalum kwa Wanadispora kwa kuishiriki
kikamilifu katika kuimarisha Sekta za Afya na Elimu hasa ikizingatiwa kwamba
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba imeweka mkazo katika kuziimarisha
sekta hizo.
Alitoa shukurani kwa
timu ya Wataalamu ya Wanadiaspora walioshiriki katika kuanzisha masomo ya Uzamivu
(PHD) ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), ambapo
mafanikio yake yamekuwa makubwa na hivi sasa wanafunzi 39 wanafanya (PHD) ya
Kiswahili chuoni hapo.
Rais Dk. Shein alitoa
wito kwa Wanadiaspora kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha
sekta ya elimu na kusomesha wataalamu wazalendo kama walivyoanza ambapo pia,
aliwahimiza Wanadiaspora kila watakapopata nafasi wajiendeleze kwa kupata elimu
zaidi hasa katika maeneo ambayo yanahitaji wataalamu.
Pamoja na hayo, Rais
Dk. Shein aliwatoa hofu Wanadiapora kwamba Jamhuri ya Muunganao wa Tanzania,
ikiwemo Zanzibar iko salama na inaendelea kuwa salama wakati wote hivyo,
wasiakhirishe matembezi ya kuja nchini na wala wasitaharuk kutokana na uchaguzi
ujao.
Alieleza kwamba mara
nyingi katika baadhi ya nchi duniani, uchaguzi huandamwa na changamoto mbali
mbali zinazopelekea hali ya amani na utulivu kutetereka hivyo, aliwaeleza
katika uchaguzi ujao wa hapa nchini vurugu hazina nafasi.
Aliwaleeza kuwa kwa
upande wa Zanzibar imeendelea kupokea wageni kutoka mataifa mbali mbali duniani
ambao wao hawana hofu na idadi yao imekuwa ikiongezeka kila mwaka sasa haoni sababu
kwa Wanadispaora kuwa na hofu kuja kutembea nchini mwao.
Rais Dk. Shein
aliwaeleza Wanadiaspora hao kwamba Serikali zote mbili zitayafanyia kazi
mapendekezo na maazimio yatakayopitishwa katika Kongamano hilo alilolizindua.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein alitoa nasaha juu ya masuala mbali mbali ikiwa ni pamoja na pale
inapotokea hali ya maisha kuwa ni magumu katika nchi wanazoishi, wasione tabu
kuja kuendelea na maisha hapa nyumbani.
Vile vile, aliwahimiza
kuzitumia vizuri taaluma zao na mitaji waliyonayo katika kuwekeza nyumbani
licha ya wengi wao kukumbana na changamoto ya usimamizi wakati wanapowekeza
hivyo, aliwataka watafute wasimamizi waaminifu na wenye ujuzi na uzoefu katika
mambo wanayoyawekeza ili waepukane na ghilba.
Aliwasisitiza kuzitumia
vizuri Ofisi zao za Kibalozi na kutafuta ushauri, nasaha na misaada kila
wanapohisi wanauhitaji msaada huo, huku akitoa pongezi maalum kwa Ofisi za
Kibalozi za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika nchi mbali mbali kwa kufanya
kazi kwa karibu na kwa kushirikiana na Wanadiaspora katika nchi hizo.
Rais Dk. Shein alitoa
pongezi kwa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Wizara ya
Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kuandaa Kongamano
hilo.
Mapema akimkaribisha
Rais, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Issa
Ussi Haji Gavu alieleza jinsi ya washiriki wa Kongamano hilo wanavyoongezeka
kila mwaka na kumpongeza Rais kwa juhudi alizozichukua katika kuhakikisha sula
la Diaspora linaimarika hapa nchini.
Nae Mwenyekiti wa
Baraza la Diaspora la Watanzania Duniani (TDC Global) Norman Jasson alitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein pamoja na
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli kwa kuendelea
kuwaletea maendeleo Watanzania wote bila ya kujali itikadi, dini au hali zao za
kijiografia.
Alitoa salamu za
upendo na pongezi kutoka kwa Balozi Dk. Willibrod Slaa Balozi wa Tanzania
nchini Sweden, nchi za Nordic, Baltic States na Ukraine ambaye ndiye mlezi wa
Baraza hilo.
Mwenyekiti huyo alieleza
umuhimu wa kuwepo kwa Sera ya Diaspora huku akieleza changamoto inayokikumba
vizazi vya Diaspora vyenye nasaba ya Kitanzania ambavyo vimetawanyika duniani
kote kutokana na Watazania kuolewa na kuoa mataifa mengine na pia Wataznania
wenye kuoa au kuolewa wakiwa tayari wamebadilisha uraia.
Alieleza kuwa kizazi
hicho ni muhimu sana kwa taifa hilo hata hivyo, kwa sasa wanakuwa na changamoto
moja kubwa ambayo wanapokuwa ughaibuni wanahesabika kama ni wageni na
wanaporudi nyumbani Tanzania ambako wazazi wao ndipo walipotokea napo wanakuja
kama wageni.
Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Makamo wa Rais Muungano na Mazingira George Simba Chawene kwa niaba ya
Waziri wa Mmabo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamangamba
Kabudi alieleza hatua zilizofikiwa katika mchakato wa Sera ya Diaspora kwa
upande wa Tanzania Bara.
Wakati huo huo, Rais
Dk. Shein alipata fursa ya kutembelea maonyesho ya Wajasiriamali mbali mbali
katika viwanja vya hoteli hiyo pamoja na sehemu maalum ya jengo la hoteli hiyo.
Katika Kongamano hilo
mada mbali mbali zimetolewa na Wanadiaspora ikiwemo mada inayohusu Urejeshaji
wa Taka za plastiki iliyotolewa na Johnas Singo Diaspora kutoka nchini Norway.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment