Habari za Punde

Maandalizi ya Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar Uwanja wa Amaan Zanzibar. Yakamilika

Wajumbe wa Kamati ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa Zanzibar wakiongozwa na Mwenyekiti wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakipokea saluti kutoka kwa Vikosi vya Ulinzina Usalama Uwanja wa Amani Mjini Zanzibar.
Kikosi cha Bendera kikiongoza Wapiganaji wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama wakati wa wimbo wa Taifa ukipigwa kwenye Matayarisho ya Mwisho ya Gwaride la Kilele cha Maadhimisho ya kutimia Miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar huko Uwanja wa Aman.
Kikosi cha Chuo Mafunzo miongoni mwa Vikosi vtakavyoshiiki Kilele cha Maadhimisho ya Miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar kikifanya vitu vyake wakati wa matayarisho ya mwisho ya Gwaride la Maadhimisho hayo.

Kikosi cha Makomandoo wa JWTZ wakitoa Saluti mbele ya  Mwenyekiti wa  Kamati ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi pamoja na Wajumbe wake hapo Uwanja wa Aman.
Picha na – OMPR – ZNZ.      
Na.Othman Khamis.OMPR.
Wakati harakati za kusherehekea Maadhimisho ya Miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar zikiendelea kupamba moto katika maeneo mbali mbali Nchini kwa uzinduzi na uwekaji wa mawe ya Msingi ya Miradi tofauti ya Maendeleo na Kiuchumi zaidi ya 63 ile Siku adhimu ya Kilele cha Sherehe hizo Tarehe 12 Januani imewadia ifikapo Jumapili ya Wiki hii.
Takriban matayarisho yote yaliyokusudiwa kufanywa kupamba Maadhimisho hayo ambapo Kilele hicho kinatarajiwa kufikia katika Uwanja wa Michezo wa Aman Mjini Zanzibar tayari yamefikia ukingoni yakitoa taswira halisi ya kumbukumbu ya Historia ya Zanzibar iliyoleta Ukombozi wa Waafrika.
Gwaride Rasmi la Vikosi vya Ulinzi na Usalama vitakavyopamba Maadhimisho ya Sherehe hizo limekamilisha matayarisho yake yaliyoshuhudiwa na Wajumbe wa Kamati ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa Zanzibar ikiongozwa na Mwenyekiti wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Wapiganaji wa JWTZ, Polisi, KMKM, Mafunzo,JKU, VALANTIA na ZIMAMOTO wameonyesha ukakamavu mkubwa wakati wakiwa kwenye mwendo wa pole na wa haraka wakati wa zoezi hilo la mwisho mazingira yakionyesha wazi muelekeo mzuri wa kufana kwa sherehe hizo zinazotimiza Miaka 56.
Sambamba na Gwaride hilo la aina yake Sherehe hizo kama kawaida yake zinatarajiwa pia kujumuisha Maandamano ya Wananchi kutoka Mikoa Mitano ya Zanzibar, Vikundi vya Utamaduni, ikiwemo Maonyesho ya Vikosi vya Ulinzi vya Makomandoo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania {JWTZ} na kile cha Polisi cha Tarbushi.
Wakifanya Tathmini ya Maandalizi ya mwisho katika Ukumbi wa Watu Mashuhuri {VIP} wa Uwanja wa Amani, Wajumbe wa Kamati ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa wameonyesha wazi furaha yao kwa hatua iliyofikiwa ya mafanikio ya maandalizi hayo.
Pamoja na mambo mengine baadhi ya Wajumbe hao walishauri umuhimu wa kuimarisha zaidi huduma za Afya katika Kilele cha Maadhimisho hayo kulingana na hali halisi ya Kiangazi iliyoambatana na joto kali kipindi hichi ambayo inaweza kuleta hitilafu hasa kutokana na Maelfu ya Wananchi watakaojumuika kwenye eneo hilo.
Akitoa nasaha zake Mwenyekiti wa Kamati ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikumbusha umuhimu wa kuzingatia wakati kwa Washiriki wote watakaohudhuria Sherehe hizo.
Balozi Seif alisema Shereha za Mwaka huu ambazo zitakuwa za mwisho kwa Uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa Awamu ya Saba utakuwa na mambo mengi yatakayohitajika kufanywa kwa wakati ili kumalizika katika muda uliopangwa wa sherehe hizo.
Kilele cha Sherehe za Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar cha Januari 12 kitatanguliwa na Mkesha wa Maadhimisho hayo utakaojumuisha ngoma za Utamaduni zitakazoambana na urushwaji wa Fash Fash katika Viwanja vya Maisra Suleiman Unguja na Tibirinzi Chake Chake Pemba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.