RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein ameungana pamoja na
Wapiganaji wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama walioshiriki katika Maadhimisho ya sherehe
za kutimiza miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar katika chakula maalum cha mchana
alichowaandalia.
Chakula hicho maalum
cha mchana aliwaandalia kutokana na ushiriki wao kwenye sherehe hizo za miaka 56
ya Mapinduzi zilizofanyika Januari 12 mwaka huu 2020 huko katika uwanja wa Amaan,
Mjini Unguja.
Hafla hiyo ya chakula
maalum ilifanyika leo katika viwanja vya
Polisi Ziwani Jijini Zanzibar, ambayo ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakiwemo Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif
Ali Idd, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, Jaji Mkuu wa
Zanzibar Omar Othman Makungu.
Wengine ni Katibu wa
Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee,
Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Said Hassan Said, Mawaziri, Manaibu Mawaziri,
Washauri wa Rais wa Zanzibar.
Aidha, viongozi
wengine pamoja na Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama vya Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Maafisa
na Wapiganaji na wanahabari kutoka
vyombo mbali mbali vya habari nao walihudhuria.
Katika shukurani zake Rais
Dk. Shein kwa Wapiganaji hao zilizotolewa kwa niaba yake na Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Issa Haji Ussi Gavu alitoa
pongezi kwa Wapiganaji hao kwa kushiriki kikamilifu katika sherehe hizo adhimu
za kutimiza miaka 56 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Waziri Gavu alimpongeza
Rais Dk. Shein kwa uongoziz wake madhubuti uliopelekea kuwepo kwa salama,
amani, umoja na mshikakamno na utulivu mkubwa ambao umezaa matunda ya maendeleo
hapa Zanzibar.
Aliendelea kutoa
shukurani kwa Rais Dk. Shein kwa muendelezeo wake wa kuwaandalia chakula maalum cha mchana ambao ni
utamaduni aliouweka kila mwaka baada ya kumaliza sherehe za Mapinduzi hatua ambayo
inaonesha wazi jinsi alivyokuwa na upendo pamoja na imani kubwa na wananchi
wote anaowaongoza.
Alieleza matumaini
makubwa yaliopo kuwa kila uchao sherehe hizo zitaendelea kuwa nzuri na
kuvishukuru Vikosi hivyo kwa kufanikisha sherehe hizo huku akitumia fursa hiyo
kuvipongeza kwa kuendelea kutimiza wajibu wao wa kulinda amani, utulivu na
mshikamano uliopo.
Waziri Gavu alitoa
shukurani za dhati kwa vikosi hivyo kwa kuadhimisha kwa hali ya juu kilele cha
miaka 56 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya Januari 12, 1964.
Sambamba na hayo, Waziri
Gavu alieleza kuwa sherehe hizo za Januari 12, 2020 zilivutia sana ambazo
zilikuwa ni kielelezo cha kutosha cha Mapinduzi ya Januari 12.1964 yaliyowakomboa
Wazanzibari wote ambayo yataendelea kulindwa, kuenziwa na kutunzwa daima.
Nae Mkuu wa Brigedi ya
Nyuk Zanzibari, Brigedia Jenerali Fadhil Omar Nondo ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na
Usalama alitoa shukurani na pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa kuendelea kuvijali na
kuvithamini vikosi vya Ulinzi na Usalama.
Alimpongeza Rais Dk.
Shein kwa kuendeleza utamaduni wake huo aliouweka wa kila mwaka ambapo mara
baada ya sherehe za Mapinduzi matukufu huwandalia chakula maalum cha mchana Wapiganaji
na Maafisa hao na kula nao pamoja.
Brigedia Jenerali
Nondo alitumia fursa hiyo kumkaribisha Rais Dk. Shein pamoja na viongozi na
wageni wote katika eneo hilo la viwanja vya Polisi Ziwani na kueleza kuwa hatua
hiyo anayoifanya Rais Dk. Shein inawachochea
kuwa na ari ya utekelezaji wa ulinzi wa nchi, wananchi wake pamoja na kuyalinda Mapinduzi ya
Januari 12, 1964.
Pia, Bregedia Jenerali
Nondo alieleza namna ya maandalizi ya gwaride yalivyofanyika hadi kufanikisha
sherehe hizo na kutoa shukurani kwa Rais Dk. Shein pamoja na Serikali kwa
kusaidia kufanikisha maandalizi yote ya gwaride hilo na kutoa pongezi na
shukurani kwa niaba ya Wapiganaji wote walioshiriki katika hafla hiyo adhimu.
Ni utamaduni aliouweka
Rais Dk. Shein wa kuwaandalia chakula cha mchana Vikosi vya Ulinzi
vinavyoshiriki katika gwaride la sherehe za Mapinduzi pamoja na vijana na
Wanafunzi ambao hushiriki sherehe hizo kwa kila mwaka.
Hapo kesho Rais Dk.
Shein amewaandalia chakula cha mchana vijana
na wanafunzi walioshiriki katika maadhimisho
ya Sherehe za kutimiza miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar hapo hapo katika
viwanja vya Polisi Ziwani Jijini
Zanzibar.
Katika hafla hiyo pia,
Kikundi cha Taarab ‘Island Super Star’ maarufu Wajelajela kutoka kikosi cha
Mafunzo kilitumbuiza kwa nyimbo zake mwanana zikiwemo zile za kuhamasisha
kuyaenzi na kuyalinda Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964 pamoja na
Brassband ya Jeshi la Polisi ambayo nayo ilitumbuiza katika hafla hiyo.
Rajab
Mkasaba, Ikulu
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment