Habari za Punde

MAJALIWA: MUUNDO WA HALMASHAURI YA JIJI LA DODOMA UKAMILISHWE


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe wakati alipozindua Mpango Kabambe wa jiji la Dodoma kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, Februari 13, 2020. Kulia ni Spika wa Bunge, Job Ndugai na kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama Mpango Kabambe wa jiji la Dodoma baada ya kuuzindua kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipozindua Mpango Kabambe wa jiji la Dodoma kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, Februari 13, 2020.
 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ameiagiza Ofisi ya Rais–TAMISEMI ishirikiane na mamlaka nyingine, zihakikishe zinakamilisha mchakato wa muundo wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Pia, Waziri Mkuu ameitaka Halmashauri ya Jiji la Dodoma iongeze kasi ya upimaji wa viwanja pamoja na kusimamia kikamilifu udhibiti wa uendelezaji holela wa makazi. “Hatuhitaji kuona Jiji la Dodoma likiwa na makazi yasiyopimwa na holela.” 

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Alhamisi, Februari 13, 2020) wakati akizindua mpango kabambe wa jiji la Dodoma katika ukumbi wa Hazina jijini Dodoma.

Waziri Mkuu amesema Serikali haitaki kuona jiji la Dodoma likiwa na makazi yasiyopimwa na holela kwani kasi ndogo ya upimaji wa viwanja kwa halmashauri ya jiji ndiyo itakayosababisha wananchi kujenga makazi holela yasiyopimwa.

Amesema wananchi hawawezi kuisubiri halmashauri bali halmashauri ndiyo inapaswa kuendana na kasi ya mahitaji ya wananchi. “Tayari katika baadhi ya maeneo wananchi wameanza na wanaendelea kujenga bila kufuata taratibu zinazotawala masuala ya ujenzi mijini.”

Waziri Mkuu ameongeza kuwa upimaji wa maeneo uende sambamba na uendelezaji wa miundombinu na huduma muhimu katika maeneo, ikiwemo maji na barabara. “Kasi ya uboreshaji barabara za mitaa iongezwe.”

Pia, Waziri Mkuu amesema halmashauri ya Jiji la Dodoma iweke utaratibu mzuri wa ufuatiliaji, utekelezaji na tathmini ya Mpango Kabambe ili kuhakikisha mpango huo unatekelezwa kikamilifu. 

“Hili ni takwa la kisheria kwa mujibu wa kifungu namba 14(3) cha Sheria ya Mipango Miji ya Mwaka 2007 ambacho kinaitaka kila mamlaka ya upangaji kutoa taarifa ya utekelezaji wa Mpango Kabambe kila mwaka katika maeneo yao ya upangaji kwa Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi.”

Hata hivyo, Waziri Mkuu ameiagiza halmashauri ya Jiji la Dodoma ianzishe mchakato wa kutambua nyumba zote zilizojengwa kwenye barabara kwa lengo la kujua idadi kamili, uhalali wao kuwepo au kama ni wavamizi na baadaye kuandaa utaratibu wa fidia kwa wananchi wanaostahili.

Kadharika, Waziri Mkuu ametoa wito kwa viongozi wa Mkoa wa Dodoma, Wizara, Halmashauri, Taasisi, sekta binafsi, Jumuiya za Kimataifa, wananchi na wadau wengine kuendelea kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa Mpango Kabambe ili kufikia malengo ya kuwa na jiji bora, lenye mandhari ya kuvutia na litakalokidhi mahitaji ya kijamii na kiuchumi ya sasa na ya baadae.

Uamuzi wa kuhamishia shughuli za Serikali Dodoma ulifanyika mwaka 1973 ikiwa ni maelekezo ya Chama cha TANU kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa utawala wa awamu ya kwanza chini ya Uongozi wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
S. L. P. 980,
41193 Dodoma,                       
ALHAMISI, FEBRUARI 13, 2020.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.