Baadhi
ya watumishi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wakila kiapo cha
Uadilifu katika utumishi wa Umma mele ya Katibu Mkuu na Msemaji Mkuu wa
Serikali Dkt. Hassan Abbasi baada ya kupata Semina elekezi kutoka Ofisi ya
Rais, Sekretariat ya Maadili ya Viongozi wa Umma iliyofanyika Februari 07, 2020
jijini Dodoma ikiwa ni sehemu ya kikao kazi cha watumishi wa Wizara hiyo.
Na Eleuteri
Mangi-WHUSM, Dodoma
Katika hali ya
kawaida mtu anapofanya vizuri hupongezwa kwa kazi nzuri aliyoifanya ndio maana
waswahili husema “Chanda chema huvikwa pete”, maana yake mtu anayefanya mema
hulipwa mema.
Maneno hayo
yanasadifu usemi aliousema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Pombe Magufuli alipokuwa anawaapisha viongozi mbalimbali February 3, 2020 Ikulu
Jijini Dar es Salaam akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo Dkt. Hassan Abbasi Said.
Rais Dkt. Magufuli alitanabaisha
utendaji wa Dkt. Abbasi kwa kusema ni mchapakazi anayefanya kazi nzuri ya
kuisemea vizuri Serikali bila kuchoka kwa kufuata miongozo mizuri ya Waziri wa
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe na viongozi wengine
kwenye Wizara hiyo.
"Ningependa
aendelee kuwa Msemaji wa Serikali, lakini mahali mtu anapotakiwa kupata
promosheni usimnyime kwa sababu ni “Motivating Agent” ndio maana tumemteua kuwa
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, na kwa sasa hivi ataendelea kuwa Msemaji wa
Serikali mpaka tutakapopata mwingine, na sasa atakuwa anasema akiwa mkubwa
zaidi" alisema Rais Magufuli.
Mara baada ya
Kuapishwa Dkt. Hassan Abbasi amesema kipaumbele chake ni kufanya mageuzi katika
Wizara hiyo kwa kuwa anazifahamu vizuri sekta za Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo.
“Nimeaminiwa tena na
Mhe. Rais namshukuru sana ninamuahidi yeye binafsi, Watanzania wote, wadau wa
hizi sekta pamoja na wafanyakazi wenzangu pale Wizarani, kwamba tunaenda
kuendeleza mageuzi, sio kuanzisha, kwa sababu watangulizi wangu niwashukuru
wameanza kazi kubwa, mimi kazi yangu pale itakuwa ni mageuzi katika Wizara ya
Habari watu wasubiri mageuzi makubwa.” alisema Dkt. Abassi.
Mara baada ya kwasili
wizarani hapo, Dkt. Abbasi alianza kazi kwa kukabidhiwa ofisi na Naibu Katibu
Mkuu Dkt. Ally Possi ambaye alikuwa akikaimu nafasi hiyo baada ya aliyekuwa
Katibu Mkuu Suzan Mlawi kustaafu.
“Nimekuta watumishi
wazuri sana Wizara hii, nimepata ushirikiano mzuri katika utendajikazi wangu,
ni timu nzuri lazima tuiboreshe. Hakika kazi yako ya kuisemea Serikali
umeifanya kwa weledi na mapinduzi makubwa sana katika Idara ya Habari ambayo
unaendelea kuwa Msemaji wa Serikali, umeipeleka Idara pazuri sana” alisema Dkt.
Possi.
Februari 7, 2020 Dkt
Abassi alikutana na watumishi wote wa Wizara hiyo waliopo Jijini Dodoma na kubainisha
mtarajio yake kwa watumishi hao na kuwahamasisha waendelee kuchapakazi kwa
weledi kwa kuzingatia taaluma zao badala ya kuendekeza uvivu, utoro,
uchelewaji, majungu, uzandiki na ubazazi.
“Natarajia mtakuwa
waadilifu na wazalendo, muipende wizara yenu na nchi yenu na msiruhusu hujuma
ya aina yeyote” Alisema.
Natarajia mtakuwa
wabunifu katika kazi zenu, mtindo wa kufanyakazi kwa mazoea bila ubunifu hauna
nafasi ni vema mtumie taaluma zenu ipasavyo ziwe na tija kwa wadau wetu na nchi
yetu” alisisitiza Dkt. Abassi
Katika kuyafikia
malengo ya Wizara na ya Serikali, Katibu Mkuu huyo aliainisha siri sita za
kusukuma mbele gurudumu la wizara hiyo kwa kuongozwa falsafa yake ya “Timu
Tunatekeleza” inayosimamia kuweka malengo katika kazi na kuyasimamia. Malengo
ni dira, bila kuweka malengo huwezi kujua hata unataka kwenda wapi wala utafika
lini na kwa njia ipi.
Siri nyingine ni
kuweka malengo makubwa, kutekeleza malengo hayo na sio maneno matupu, kuwa na
mawasiliano madhubuti ndani na nje ya wizara ili kuyafikia malengo hayo, kuwa
na ushirikiano baina ya menejimenti, watumishi na wadau wa taasisi pamoja na
kuamini nguvu ya Mungu katika kufikia malengo tunayojiwekea kwa kuwa yapo mambo
ambayo yanazidi uwezo wa mwanadamu na hapo nafasi ya Muumba ni ya muhimu.
Awali akimkaribisha
Katibu Mkuu Dkt. Abbasi kuongea na watumishi hao Mkurugenzi wa Utawala na
Rasilimaliwatu Macelline Patrick alisema lengo la kikao hicho ni kutambulishana
pamoja na kutoa ahadi ya uadilifu kwa viongozi na watumishi kwa Kiongozi na
Mtendaji Mkuu wa Wizara.
Pia aliongeza kuwa Wizara
hiyo ina idadi ya watumishi 224 ambao miongoni mwao wapo Makao Makuu jijini
Dodoma na wengine wapo jijini Dar es salaam pamoja na Chuo cha Maendeleo ya
Michezo cha Mallya kilichopo mkoani Mwanza.
Kwa upande wake
Katibu wa Chama cha Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini (TAGCO) Abdul
Njaidi amesema kuwa wamefurahishwa na uteuzi wa Dkt. Abbasi kushika wadhifa
Katibu Mkuu kwa kuwa ataendelea kuwa nao katika tasnia ya Habari.
“Ataifanya TAGCO
iende hatua za juu zaidi kwa sababu anaijua, siku zote amekuwa akisimamia
taaluma na kutaka watu wafanye kazi kwa matakwa ya taaluma zao ili kufikia
malengo ya Serikali ya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo 2025”
alisema Njaidi.
Aidha, Baada ya
kuteuliwa na Rais Ijumaa Januari 31, 2020, baadhi ya wadau wa sekta ya habari
wakiwemo Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini pamoja na Wizara na Taasisi
mblimbali walitoa pongezi na maoni yao kupitia jukwaa la “WhatsApp” kuhusiana
na uteuzi huo.
Baadhi waliandika
pongezi zao kwa Katibu Mkuu Dkt. Abassi ambapo Theodos Komba anasema “Hongera
Dkt., Mungu aendelee kukubariki katika utekelezaji wako wa majukumu mapya.
Tunafuraha kuwa tunaendelea kuwa pamoja”; Nteghejwa Hosea anasema “Hongera Dkt.,
Mungu ataendelea kukuongoza hata hapo unapoenda sasa;”
Wengine waliotoa
maoni yao ni Mtamike Omary anasema “Hongera Dkt., Mwenyezi Mungu azidi
kukujaalia hekima na busara nyingi zaidi wakati wote wa uongozi wako, hakika umekuwa
nahodha bora sana kwetu;” Peres Muhagaze anasema “Hongera sana Dkt. Hassan
Abbas!! Umeitumikia Serikali na Umma kwa ueledi wa hali ya juu ukiwa
Mkuruggenzi wa Idara ya Habari MAELEZO na
Msemaji Mkuu wa Serikali, umeacha alama, tunakuombea ufanye zaidi katika
ofisi yako mpya ya Katibu Mkuu wa Wizara na kuendelea ili kutimiza adhma yako ya ndani ya kuwatumikia Watanzania
katika masuala mbalimbali. Mwenyezi Mungu akutangulie katika maukumu mapya”
Aidha, pongezi hizo
kwa Katibu Mkuu Dkt. Abassi pia zimetolewa na Wizara na Taasisi mbalimbali
ikiwemo Wizara yake anayoiongoza, Wizara ya Maji, Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),
Kampuni ya Magazeti ya serikali Tanzania (TSN) na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi
wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA).
Akiwashukuru wadau hao
kupitia jukwaa hilo kwa kumpongezi zao, Katibu Mkuu Dkt. Abassi anasema “Team,
Kimsingi sina la kusema kwa imani hii kubwa ambayo Mhe. Rais ameendelea
kuniamini. Namhuskuru sana sana na zaidi nawashukuru wote kwa salaam.
Ni faraja kwamba bado
tuko wote katika sekta ya Habari. Tuanzie hapo tulipoishia. Hii ni Wizara
iliyobeba soft power zote za nchi. Nawatakia kasi na utekelezaji mwema wa pale
tulipoishia. Nitabaki kuwa mlezi wenu mujarabu. Hakika mmenilea, mmenishauri,
mmenisikiliza, mmenivumilia na tumepiga kazi, basi na kazi iendelee. Nyie ni
TeamTunatekeleza Tuendelee na kazi Mungu Awabariki.”
Dkt. Abbasi anakuwa
Katibu Mkuu wa 26 kuingoza Wizara hiyo akitanguliwa na Makatibu Wakuu 25 tangu nchi
yetu kupata Uhuru mwaka 1961 ambapo mnamo mwaka 1964 Rais wa Kwanza wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mwl. Julius Nyerere aliunda Wizara ya Habari na Utalii
ilidumu hadi 1971 ilipoundwa Wizara ya Habari na Utangazaji. Mwaka 1980
Serikali iliunganisha majukumu ya sekta ya Habari na Utamaduni na kuunda Wizara
ya Habari na Utamaduni.
Aidha, mwaka 1984
majukumu ya sekta ya Habari na Utamaduni yalihamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu na
Makamu wa Pili wa Rais na na mwaka 1995 hadi 2005 majukumu ya Sekta ya Habari
yapohamishiwa tena Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mara baada ya
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, Sekta ya Habari, Utamaduni na Michezo
ziliunganishwa pamoja na kuunda Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo na baada
ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Serikali iliunda Wizara Mpya ya Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo. Mwaka 2016 Serikali ya Awamu ya Tano iliunda Wizara ya
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michzo ambayo inafanya kazi hadi sasa.
Makatibu Wakuu
waliohudumu katika Wizara hii ni pamoja na Bw. A. K. Tibandebage, Bw. B. J.
Mkate, Bw. Bernard Mulokozi, Bibi Zahra Nuru, Dkt. Ben Moses, Bw. Daniel Mloka,
Mhandisi Paul Mkanga, Bw. Paul Sozigwa, Bw. Wilfred Mwabulambo, Bw. Silvano
Adel, Bw. Elly Mtango, Bibi Rose Lugembe, Bw. Raphael Mollel, Bw. Silvanus
Odunga, Bw. Abubakari Rajabu, Bw. Kenya Hassan, Bw. D. Sepeku, Bw. Raphael Mhagama, Bibi Kijakazi Mtengwa, Dkt.
Florens Turuka, Bw. Sethi Kamuhanda,
Bibi Sihaba Nkinga, Prof. Elisante Ole Gabriel na Bibi Suzan Mlawi.
Dkt Hassan Abbasi
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa
Serikali, ameshika wadhifa wa Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji
Mkuu wa Serikali tangu Agosti 5, 2016 hadi kuteuliwa kwake kushika wadhifa huo
Januari 31, 2020 na kuapishwa Februari 03, 2020 Ikulu jijini Dar es Salaam.
Alizaliwa wilayani
Korogwe, Tanga mwaka 1978 na kupata elimu yake ya msingi katika Shule ya Msingi
Hale kati ya mwaka 1988 na 1994. Alimaliza akiwa mmoja wa wanafunzi waliofanya
vizuri mkoani humo na kujiunga na Sekondari ya wanafunzi wenye vipaji maalum ya
Tabora Wavulana (Tabora School) mwaka 1995 kwa masomo ya sekondari.
Kati ya mwaka 1997 na
1998 alihamia katika Sekondari ya Azania, Dar es Salaam ambapo alimaliza kidato
cha nne na kati ya mwaka 1999-2001 alijiunga na Shule ya Sekondari Lindi kwa
masomo ya kidato cha tano na sita.
Kati ya mwaka 2002 na
2006 alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo alichukua shahada ya
kwanza ya sheria (LL.B). Akiwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu pia aliajiriwa kama
mwandashi wa habari wa kujitegemea katika kampuni ya Business Times na baadaye
kushika nafasi mbalimbali kuanzia mwandishi mwandamizi, mhariri msaidizi hadi
mhariri Mkuu katika magazeti ya Majira na Kulikoni.
Mwaka 2005 akiwa bado
mwanafunzi, alichaguliwa kuwa Mhariri Mkuu wa Jarida liitwalo “Nyerere Law
Journal” linalochapishwa na Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Kati ya mwaka 2007 na
2008 alihudhuria masomo ya uandishi wa habari ndani na nje ya nchi ikiwemo
makao makuu ya Reuters, London, Uingereza na Chuo Kikuu cha Maine nchini
Marekani.
Mwaka 2010 aliajiriwa
Serikalini akiwa Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano katika Mpango wa
Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) tawi la Tanzania, programu iliyoko
chini ya Wizara ya Mambo ya Nje, ambapo kabla ya mwaka 2014 alikuwa Meneja
Mawasiliano katika Ofisi ya Rais, Kitengo cha Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Aidha, ana taaluma ya
Sheria ambapo ana hadhi ya Wakili wa Mahakama Kuu tangu mwaka 2011, Dkt. Abbasi
pia ana diploma ya uzamili katika usimamizi wa mahusiano ya kimataifa (PGD-MFR)
kutoka Chuo cha Diplomasia cha Msumbiji na Tanzania, Kurasini, shahada ya
uzamili katika mawasiliano kwa umma (MA Mass. Comm., SAUT) na shahada ya
uzamivu katika mawasiliano kwa umma (Ph.D Mass. Comm., SAUT).
No comments:
Post a Comment