RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein,
akizungumza na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira
Mhe. Mussa Azzan Zungu, alipofika Ikulu Jijini Zanzibar. Kujitambulisha na
kufanya mazungumzo.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akimsikiliza Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Mussa Azzan Zungu alipofika Ikulu
Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha leo 14-2-2020.
RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amemuhakikishia kumpa
mashirikiano makubwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Rais, Muungano na
Mazingira Mussa Azzan Zungu ili aweze kutekeleza vyema majukumu yake hasa yale
yanayohusu Muungano.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo, Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Rais, Muungano na Mazingira Mussa Azzan Zungu ambaye
ameteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John
Pombe Magufuli ili kushika wadhifa huo.
Katika maelezo yake
Rais Dk. Shein alimueleza Waziri huyo kuwa yeye mwenyewe pamoja na viongozi
wote wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakiwemo Mawaziri wake watahakikisha
wanampa mashirikiano makubwa Waziri huyo ili aweze kutekeleza vyema kazi zake.
Rais Dk. Shein alimueleza
kiongozi huyo kuwa miongoni mwa majukumu yake makubwa aliyonayo moja wapo ni
kuhakikisha jitihada za waasisi wa Taifa hili Hayati Mzee Abeid Amani Karume na
Hayati Julius Kambarage Nyerere za kuleta Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
zinaendelezwa na zinadumishwa.
Aliongeza kuwa
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umeleta mafanikio makubwa hasa ikizingatiwa
kwamba walioungana ni wananchi wa pande mbili ambao wana udugu wa asili na
historia ya muda mrefu.
Aidha, Rais Dk. Shein
alieleza matarajio yake makubwa aliyonayo kutokana na utendaji kazi na uzoefu
alionao Waziri huyo ukiwemo uzoefu wa utumishi Serikalini pamoja na ule wa ndani ya Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Pamoja na hayo Rais
Dk. Shein alieleza kuwa mapenzi udugu wa wananchi wa pande mbili za Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ni vyema ukaimarishwa na kudumishwa sambamba na kuendeleza
mashirikiano yaliopo ya kihistoria.
Nae Waziri wa Nchi
Ofisi ya Makamo wa Rais, Muungano na Mazingira Mussa Azzan Zungu alitoa shukurani kwa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli pamoja na Rais wa Zanzibar Dk.
Ali Mohamed Shein kwa kupata uteuzi huo ambao aliahidi kuufanyia kazi kwa
ufanisi pamoja na kuutendea haki.
Waziri Mussa Azzan
Zungu ambaye alikuwa amefuatana na Mkurugenzi wa Muungano Balozi Mbarouk Nassor
Mbarouk, alimueleza Rais Dk. Shein kuwa atahakikisha umoja, mshikamano, upendo
na udugu uliopo kati ya Serikali, wananchi na viongozi wa Zanzibar na Tanzania
Bara unadumishwa na kuendelezwa kwa manufaa ya Taifa lao.
Sambamba na hayo,
Waziri Mussa Azzan Zungu alimuhakikishia
Rais Dk. Shein kuwa atahakikisha changamoto ndogo ndogo zinazowasumbua wananchi
hususan wafanyabiashara zinafanyiwa kazi changamoto ambazo husababishwa na
baadhi ya watendaji.
Alimuhakikishia Rais
Dk. Shein kuwa atahakikisha anaendeleza na kuzidisha mashirikiano yake na
viongozi wakiwemo Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kuhakikisha
majukumu yake anayatekeleza vyema kwa azma ya kupata mafanikio katika pande
zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Waziri Mussa Azzan
Zungu ambaye pia, ni Mbunge wa Ilala aliteuliwa na Rais John Magufuli mnamo
Januari 23 mwaka huu wa 2020 kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Rais,
Muungano na Mazingira huku aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo George Simbachawene
akiteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani.
Waziri George
Simbachawene amechukua nafasi ya Kangi Lugola ambaye uteuzi wake ulitenguliwa
na Rais John Pombe Magufuli.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment