Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Mhe. Ummy Mwalim (mwenye kitambaa kichwani) akiomgea na Waandishi
wa Habari wa vyombo mbalimbali vya habari leo alipotembelea Jengo la Tatu
la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA),
kukagua namna walivyojiandaa kudhibiti maambukizi ya virusi vya Corona
vinavyosababisha homa ya mapafu, vilivyoanzia nchini China.
Na
Bahati Mollel,TAA
WAZIRI
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,
Ummy Mwalim amesema wataomba kibali cha kuongeza watumishi wa afya kwa ajili ya
Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), ambapo kumekuwa na
abiria wengi wanaotoka nje ya nchi.
Mhe. Mwalim aliyasema hayo leo wakati alipotembelea jengo la tatu
la abiria – TB3, wakati wa mchana muda wa kuwasili abiria kutoka nchi
mbalimbali Duniani, ikiwa ni moja ya lengo la kukagua utayari wa watumishi wa
afya na kiwanja hicho kwa ujumla wa kudhibiti homa ya mapafu inayosababishwa na
virusi vipya vya Corona 2019.
“Nimejionea abiria ni wengi sana na wataalam wetu ni wachache
inahitajika waongezwe kwa haraka ili waweze kuwahudumia kwani wengi wanawasili
kwa wingi kwa ndege za mchana kunakuwa na msongamano usiokuwa wa lazima”
alisema Mhe. Mwalim.
Pia amesema ameweza kukagua maeneo ambayo abiria atakayebainika
kuwa na homa hiyo ya mapafu na kugundua kwa sasa chumba kipo kimoja na
hakitoshelezi jinsia zote mbili, hivyo anaangalia uwezekano wa kupatikana kwa
chumba kingine cha pili.
“Ninaishukuru Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania kwa
kushirikiana vyema na Kitengo cha afya cha hapa JNIA, maana wameweza kuweka
vifaa muhimu ikiwemo dawa maalum ya kunawa mikono kwa abiria anapowasili tu, na
endapo atakuwa na virusi hivyo vinakuwa vimedhibitiwa kwa kiasi fulani,”
amesema.
Ila ameagiza sasa kutengwe eneo maalum patakapowekwa vifunika pua
na mdomo (masks) kabla ya abiria kutoka eneo la kiwanja cha ndege na baadaye
vikatekelezwe kwa moto, kwa kuwa abiria wanakuwa wamesafiri navyo kwa safari
ndefu wawapo ndani ya ndege hadi wanapowasili.
Halikadhalika ameagiza fomu maalum za kujua maelezo mbalimbali ya
abiria sasa zijazwe ndani yandege ili kuepuka msongamano wa abiria katika eneo
wanalotumia kujazia.
Akizungumzia hali ya homa hiyo kwa Tanzania, amesema hakuna
mgonjwa aliyegundulika kuwa na virusi hivyo, kwa mipaka yote ambayo inaingiza
watu wa mataifa mbalimbali wakiwemo Watanzania wenyewe.
Hatahivyo, Mhe. Mwalim ametoa angalizo kwa wananchi kuwa wakiona
dalili za ugonjwa huo ambazo ni kukohoa, homa kali, nimonia, kupumua kwa tabu,
kutapika na kuharisha wawahi vituo vya afya kupima afya zao kabla hali haijawa
mbaya zaidi kwani virusi vinadumu kwa siku 14 na dalili kuanza kuonekana.
Naye Kaimu Meneja wa TB3, Mhandisi Barton Komba amesema
watatekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Mhe. Waziri kwa kushirikiana na
wadau wengine wanaohusika na abiria yakiwemo mashirika ya ndege na kitengo cha
afya kilichopo kiwanjani hapo.
“Kama mlivyoona Mhe. Waziri wa afya amekuja kutembelea na kuja
kuangalia miundombinu ya viwanja vya ndege kwa kuwa ni moja ya mipaka japokuwa
kuna changamoto za hapa na pale na sisi tutatekeleza, tutaongeza maboresho
yote,” Amesema Mhandisi Komba.
Mbali na China ulipoanzia ugonjwa huu nchi nyingine zilizoathirika
na homa hii ni pamoja na Thailand, Australia, Marekani, Singapore, Malaysia,
Japan, Korea Kusini, Ufaransa, Canada, Vietnam, Ujerumani, Nepal, Sri-lanka na
Cambodia. Hata hivyo, kasi ya maambukizi ya virusi vya Corona sasa ni tishio
hadi Barani Ulaya.
Corona ni kundi kubwa la aina ya virusi, ambavyo huweza kumuathiri
binadamu na wanyama, ukubwa wa maambukizi unahusisha homa za kawaida pamoja na
homa kali na wakati mwingine matatizo katika mfumo wa upumuaji.
Namna mtu anavyoambukizwa homa hii ni pamoja na kugusana moja kwa
moja bila kinga na muathirika; kushika kwa mkono vifaa vya muathirika na
baadaye kushika mdomoni au puani, ambapo virusi husambaa kwa kasi.
No comments:
Post a Comment