Habari za Punde

BARAZA LA VIJANA ZANZIBAR LATOA VIFAA VYA KUJIKINGA NA CORONA

Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Zanzibar Khamis Rashid Kheir akimkabidhi ndoo na sabuni  Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Wilaya ya Magharibi “B”Hassan Ali Nassor  kwa ajili ya matumizi ya kujikinga na maradhi ya Corona huko katika Jengo la Baraza la Vijana Mwanakwerekwe .  
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Zanzibar Khamis Rashid Kheir akitoa maelezo kwa vijana kuhusu jinsi ya kijiepusha maambukizi ya maradhi ya Corona kulia ni Katibu Muhtasi wa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Wilaya ya Magharibi “B“ Khadija Nassor Khamis.
Baadhi ya Vijana kutoka Wilaya za Unguja wakimsikiliza Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Zanzibar Khamis Rashid Kheir ambae hayupo pichani huko katika Ukumbi wa Baraza la Vijana Mwanakwerekwe. 
Picha na Khadija Khamis -Maelezo Zanzibar.

Na Khadija Khamis –Maelezo Zanzibar  30/03/2020
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Zanzibar Khamis Rashid Kheir amewataka vijana kuunga mkono serikali kwa kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya katika kukabiliana na maradhi ya mripuko ya Corona
Hayo aliyasema wakati alipokuwa akigawa vifaa mbali mbali vya kujikinga na maradhi Corona huko Baraza la Vijana Mwanakwerekwe. 
Aliwataka vijana kuwa makini katika kupambana na maradhi hayo kwani hivi sasa yamekwisha sambaa duniani kote
‘Nyinyi ndio taifa la kesho hivyo wekeni tahadhari kujikinga na maambukizo kwa kufuata 
taratibu na miongozo ya serikali inayotolewa na  Wizara husika na kuacha kufanya mzaha 
tatizo ni kubwa,” alisema Mwenyekiti huyo.
Aliwataka vijana hao kuacha kusikiliza taarifa zisizothibitiishwa na kutolewa na serikali zote mbili  kwani kufanya hivyo kutawajengea hofu.
Aliwafahamisha vijana hao kutumia fursa ya kuzungumza ugonjwa wa Corona katika maeneo  yao  na kuielimisha jamii jinsi ya kujikinga kwa lengo la kuepuka kusambaa zaidi .
Aliwaelekeza vijana kutumia vifaa vya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona ili maradhi hayo yaishe na kuwafanya watu waendelee na shughuli zao za  kiuchumi.
 Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazee Zanzibar Kombo Mohamed Khamis amesema mashirikiano ya Baraza la Vijana na Jumuiya hiyo itasaidia kushajihisha vijana kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya katika kujikinga na janga la Corona . 
Dunia hivi sasa inakabiliwa na janga kubwa la maambukizi ya maradhi ya corona yanayotokana na virusi vya aina ya COVID -19 ambayo yalianzia nchini China katika Mji wa Wuhan September 2019 mwaka jana na kusambaa nchi mbali mbali ulimwenguni.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.