Habari za Punde

Balozi Seif Amewatahadharisha Umma Idadi ya Watu Wanaoendelea Kupata COVID -19 Inaweza Kushuka Iwapo Kila Mwana Jamii Atachukua Tahadhari ya Kujikinga.


Na.Othman Khamis Ame.OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameutahadharisha Umma kwamba idadi ya Watu wanaoendelea kupata Virusi vya Corona {COVID-19} inaweza kushuka iwapo kila mwana Jamii atachukuwa tahadhari kubwa ya kujikinga na adui huyo asiyeonekana ambaye hushambulia bila ya kujali rangi, umri au jinsia ya Mtu.
Alisema Jamii endapo itazingatia katika kufuata miongozo na maelekezo yanayotolewa na Viongozi, Wataalamu wa Afya likiwemo Shirika la Afya Duniani {WHO} inaweza kuusambaratisha kabisa Ugonjwa unaosababishwa na Virusi hivyo ambavyo hadi sasa bado havijapatiwa Dawa wala Kinga.

Akifunga  Mkutano wa 18 wa Baraza la Tisa la Wawakilishi huko Chukwani Nje kidogo ya Jiji la Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alionya kwamba Wataalamu wa Afya wanakadiria kuwa Mataifa ya Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania Watu wapatao Elfu 10,000 watakuwa wameambukizwa Virusi vya Corona hadi ifikapo Mwezi ujao wa Mei Mwaka huu.

Alisema Taifa hivi sasa liko katika mapambano makali dhidi ya Virusi vya Corona ambavyo vimeshaathiri Mataifa kadhaa Duniani kwa kupoteza Wananchi wao nyengine zikifikia viwango vya Watu 800 hadi zaidi ya 2,000 kwa saa 24 wakati Mataifa hayo yana vifaa, zana za kisasa na Wataalamu wa Afya waliobobea lakini tayari zimezidiwa.

Balozi Seif  ameendelea kuwaomba Wananchi kutafakari hali hii ili wapate kuelewa ukubwa wa adui wanaopambana nae vyenginevyo watashtukia wameshakuwa mateka wa Adui huyo na mategemeo yatayobakia ni kusubiri kiwango kikubwa cha vifo vya Watu.

“ Ukipambana na adui wa aina hii ambae humuoni anayeshambulia kila Mtu, unatakiwa kuwa makini na kuchukuwa tahadhari kubwa vyenginevyo utajishtukia umeshakuwa mateka. Nchi pamoja na wewe mkishawekwa mateka na adui huyu shuhudieni vifo vya Watu wengi”. Alisisitiza Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewakumbusha Viongozi wa ngazi zote kushirikiana na Wananchi katika kuzisimamia taratibu zilizowekwa katika kupambana na Virusi vya Corona vinavyosababisha Mafua na Homa Kali za Mapafu.

Alisema wakati umefika kwa Wananchi baadhi yao kuacha ukaidi na dharau kwa kufuata maagizo ya Wataalamu wa Afya pamoja na Viongozi wao kwani Afya ndio Rasilmali inayotegemewa kupitia Falsafa ya Afya isemayo Kinga ni bora zaidi kuliko Tiba.

“Sisi Waswahili tumekuwa tukisemwa sana kwa ukaidi na dharau, lakini wahenga wamesema mkaidi hafaidi mpaka siku ya Iddi, si hivyo tutadhurika sisi wenyewe, Familia na Jamii inayotuzunguuka kwa ukadi na dharau zetu”. Alitanabahisha Balozi Seif.

Alifahamisha kwamba Taifa la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Bara na Zanzibar limekuwa katika tahadhari mara Moja baada ya Virusi vya Corona kuripotiwa kuibuka Nchini China Mwezi Disemba Mwaka 2019 ili kujaribu kuwakinga Wananchi wake.

Alieleza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzu Dr. Ali Mohamed Shein wamechukuwa hatua mbali mbali za ya kusimamia mapambano ya Janga hilo ikiwemo kuzuia Ndege kutua Nchini kutoka Mataifa ambayo yamekumbwa na Virusi hivyo.

Alisema Ijitimai ya Kimataifa, Mkutano wa Kimataifa wa Wawekezaji na Kongamano kubwa la Kilimo yalizuiliwa kufanyika Nchini, hatua zote hizo zikiwa na lengo Moja la kuwakinga Wananchi wote na Maambukizo ya Vurisi vya Corona.

“Rais wetu wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi tayari ameshatoa maagizo ya kujengwa kwa Maabara ya Kisasa ndani ya Miezi Mitatu katika eneo la Binguni ili kuchunguza na kutafiti maradhi mbali mbali ikiwemo Virusi vya Corona “ Alisema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Balozi Seif  amewapongeza Viongozi hao Wakuu kwa juhudi zao za dhati walizozichukuwa za kusimamia mapambano dhidi ya kuenea kwa Virusi vya Corona na Wananchi hawanabudi kuzithamini jitihada hizo kwa kufuata maelekezo yao na yale yanayotolewa na Wataalamu wa Afya.

Aidha Balozi Seif aliwapongeza Watumishi wote wa Sekta ya Afya  Unguja, Pemba na Tanzania Bara ambao wamejitolea kupambana kwa hali na Mali ili kuokoa Maisha ya Wananchi wote.

Alisema Watumishi hao ndio askari wa Taifa kipindi hichi, hivyo Serikali zote Mbili kwa upande wao zitahakikisha zinawapatia Vifaa vinavyohitajika vya kujikinga na Maradhi yanayotokana na Virusi vya Corona ili wafanye kazi zao bila ya kuambukizwa.

Akizungumzia Mradi mkubwa wa kuondoa Maji ya Mvua katika Maeneo mbali mbali ya Jiji la Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali Kuu imelazimika kutumia Fedha nyingi kugharamia ujenzi wa Misingi iliyolengwa katika Mradi huo.

Alisema Misingi iliyopo Mitaa ya Chumbuni, Jang’ombe, Mwanakwerekwe- Sebleni- Mikunguni, Lumumba  hadi Kwampiga Duri tayari imeshakamilika ujenzi wake na imenza kufanya kazi ya kuondoa tatizo la maji ya Mvua katika maeneo mengi ya Jiji la Zanzibar.

Balozi Seif ametoa wito kwa Wananchi wote kuendelea kushirikiana na Serikali kupitia Taasisi zilizopewa jukumu la kusimamia usafishaji wa Misingi hiyo katika kuitunza ili iendelee kutumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa kwa muda mrefu zaidi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alionya kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kamwe haitamvumilia Mwananchi ye yote atakayejaribu kuunganisha misingi hiyo na Bomba lake la Maji Machafu kutoka Nyumbani kwake kwani hilo ni kosa  na atalazimika achukuliwe hatua za Kisheria.

Kuhusu Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {TASAF} Awamu ya Tatu Sehemu ya Pili utaotekelezwa katika kipindi cha Miaka Minne Balozi Seif alisema Serikali zote Mbili ile ya Jamuhuri na ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeshaanza hatua kadhaa za matayarisho ya Kitaalamu ya Utekelezaji wa Mpango huo.

Alisema Utekelezaji wa Mpango huo uliozinduliwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano Dr. John Pombe Magufuli  Tarahe 17 Mwezi Febuari Mwaka 2020 unategemewa kuvifikia Vijiji vyote kwa upande wa Tanzania Bara wakati jumla ya Shilingi Bilioni 21.5 pekee zitatumika kwa Mwaka kwa  Shehia zote zilizopo upande wa Tanzania Zanzibar.

Aliwaomba Watendaji na wahusika wote kufanya Kazi kwa uadilifu, juhudi na uaminifu ili kuendeleza sifa nzuri iliyojikusanyia Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika utekelezaji wa Mradi wa Tasaf uliopelekea Watu kutoka Mataifa mbali mbali nje ya Tanzania kufika kujifunza namna unavyotekelezwa kwa ufanisi.

Katika Mkutano huo wa 18 wa Baraza la Tisa la Wawakilishi Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar walipata fursa ya kupokea na kujadili Miswada Minane pamoja na Ripoti Sita zilizowasilishwa kutoka Wizara mbali mbali za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Miswada hiyo ni Mswada wa Sheria ya Kufuta Sheria ya mambo ya Rais Nambari 5 ya Mwaka 1993 na kutunga Sheria ya mambo ya kuweka Masharti bora zaidi kuhusiana na mambo mengine yanayohusiana na hayo, Mswada wa Sheria ya kuanzisha Sheria ya masuala ya Diaspora na Mambo mengine yanayohusiana na hayo.

Mengine ni Mswada wa Sheria ya kufutana kuandikwa Upya Sheria ya vileo na kuweka Masharti ya kuzuia, kudhibiti na kusimamia uagizaji, kuhifadhi kwenye maghala, uuzaji, usambazaji na unywaji, vileo na mambo mengine yanayohusiana na hayo, Mswada wa Sheria wa Vipimo Nambari 4 ya Mwaka 1983  na kuanzisha Sheria ya Wakala wa Viwango na Mambo mengine yanayohusiana na hayo pamoja na Mswada wa Sheria ya kuanzisha Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Zanzibar na Mambo mengine yanayohusiana na hayo.

Aidha Miswada mengine ni ule wa kufuta Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Nambari 8 ya Mwaka 2012 na kutunga Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Zanzibar na Mambo mengine yanayohusiana na hayo, Mswada wa Sheria ya Usajili na Usimamizi wa Wataalamu wa Maabara za Tiba na Mambo mengine yanayohusiana na hayo na ule mswaada wa Sheria ya kuanzisha Taasisi ya Utafiti wa Afya Zanzibar na Mambo mengine yanayohusiana na hayo.

Baraza la Wawakilishi halkadhalika likapokea, kujadili na kupitisha Ripoti za Wizara za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, juu ya Utekelezaji wa Maagizo ya Kamati za Kudumu za Baraza la Wawakilishi kwa Mwaka 2019/2020.
Baraza la Wawakilishi Zanzibar limeahirishwa hadi Jumatano ya Tarehe 6 Mei Mwaka 2020.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
17/04/2020.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.