Habari za Punde

Dk. Shein Amewataka Maafisa Wadhamini Pemba Kufanyakazi ya Kukabiliana na Maafa Kwenye Maeneo Ambayo Wananchi Wameathirika Hasa Ikizingatiwa Kwamba Kazi Hiyo Haina Afisa Maalum Bali Wote Wanatakiwa Kuwajibika.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Maofisa Wadhamini wa Wizara Pemba wakati wa ziara yake, mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Ikulu Ndogo Chakechake Pemba. 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewataka Maafisa Wadhamini kisiwani Pemba kufanya kazi ya kukabiliana na maafa kwenye maeneo ambayo wananchi wameathirika hasa ikizingatiwa kwamba kazi hiyo haina Afisa maalum bali wote wanatakiwa kuwajibika.

Rais Dk. Shein aliyasema hayo leo huko Ikulu ndogo, Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba, wakati alipofanya mazungumzo na Maafisa Wadhamini wa Wizara za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wanaofanya kazi zao Pemba ikiwa ni miongoni mwa ziara yake ya siku tatu kisiwani humo.

Rais Dk. Shein aliwasisitiza viongozi hao kuzifanyia haraka tathmini za maafa kwa kila Wilaya yakiwemo maeneo ya vijijini ili kujua nani anatakiwa kusaidiwa ili shughuli hizo zifanyike ipasavyo na kwa muda muwafaka.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein aliwataka viongozi hao kuwa mstari wa mbele katika kushirikiana na Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar ikiwa ni pamoja na kupambana na maradhi yanayosababishwa na virusi vya Corona.

Dk. Shein aliwapongeza viongozi hao kwa kufanya kazi nzuri ya kupambana na maradhi yanayosababishwa na virusi vya Corona kwa kushirikiana na Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar na kusisitiza kuwa hilo ni jukumu la sekta zote za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Alieleza kuwa jukumu la kupambana na maradhi yanayosababishwa na virusi vya Corona si la Wizara ya Afya pekee, bali ni la taasisi zote na kueleza kuwa kazi ya kupambana na maradhi hayo inafanywa vizuri na viongozi wa Pemba hivyo, ni vyema wakaendelea na mfumo huo.

Kwa upande wa maafa yaliyosababishwa na athari za mvua za Masika zinazoendelea, Rais Dk. Shein alieleza kuwa mvua ni neema ila kuzidi kwake kiwango ndiko kulikopelekea maafa hayo ikiwa ni pamoja na kuanguka kwa nyumba za wananchi na kuwataka viongozi hao kufanya kazi kwa kusaidia kwani hiyo ni kazi ya jamii na wote wanahusika.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein aliwataka Maafisa hao Wadhamini kutokaa maofisini tu na badala yake waendee katika maeneo yao ya kazi kwa maslahi ya wananchi na serikali kwa jumla.

Aidha, alisema kuwa  hali ya nchi ni nzuri na ina utulivu mkubwa ambapo Serikali zote mbili zinaendelea kusimamia vyema amani na utulivu pamoja na kulinda mipaka yake na kuvipongeza vikosi vya ulinzi na usalama kwa kulisimamia hilo.

Aliongeza kuwa maendeleo yaliopatikana hapa nchini yanatokana na amani na utulivu mkubwa uliopo hivyo, ni lazima yasimamiwe kwa ari na kasi kubwa na kueleza  matumaini yake kuwa amani  iliyopo nchini itaendelea kulindwa kwa nguvu zote.

Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kueleza hatua zinazochukuliwa na Serikali zote mbili katika kukaabiliana sambamba na kupambana na maradhi yanayosababishwa na virusi vya Corona. 

“Matumaini yetu maradhi haya yanayosabahishwa na virusi vya Corona yatamaliza kwani juhudi zetu pia zinahitajika na Mwenyezi Mungu atatusaidia........hakuna dhiki wa dhiki bali baada ya dhiki ni faraji”, alieleza Dk. Shein

Aidha, Rais Dk. Shein aliendelea kusisitiza kuwa hofu ni mbaya sana hivyo, aliwataka viongozi hao kuwaondoa hofu wananchi pamoja na kujiondoa hofu wao wenyewe.

Alisema kuwa katika kupambana na maradhi hayo hakuna haja ya kuvunjana moyo na wale wote waliougua na wanaoendelea kuugua maradhi hayo wapewe faraja na wasinyanyapaliwe.

Alieleza kuwa ni vyema wananchi wakaendelea kumuomba Mwenyezi Mungu kuyapeperusha maradhi hayo sambamba na kuendeleza juhudi za kupambana nayo.

Aidha, Rais Dk. Shein alisema kuwa maradhi yanayosababishwa na virusi vya Corona yameleta changamoto ikiwemo maradhi yenyewe sambamba na changamoto ya kiuchumi hapa nchini na dunia nzima kwa jumla.

Rais Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haijatetereka kiuchumi licha ya kuwepo kwa maradhi hayo na kila lililopangwa linatekelezwa ipasavyo kwa azma ya  Serikali ya kuwahudumia wananchi wake wote.

Akitolea mfano ujio wa watalii ambao husaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha uchumi kwa kuingiza asilimia 80 ya fedha za kigeni, Rais Dk. Shein alisema kuwa hivi sasa haupo na kile kilichokuwa kikipatikana hakipo lakini Serikali ipo na inaendelea kufanya kazi zake kama kawaida.

Aliongeza kuwa Serikali haijafunga mikono na inafanya kazi na inakwenda vyema na shughuli zinafanywa na kila mmoja anapata haki yake ya msingi. “tunaendelea na shughuli zetu na serikali inaendelea kufanya shughuli zake za maendeleo”.

Aidha,Dk. Shein alieleza  kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea na  ujenzi wa jengo jipya la uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume (Terminal III), na wajenzi wake wanaendelea kulipwa na miradi yote ya Maji na Usafi wa Mazingira (ZUSP) Unguja na Pemba inaendelea vizuri sambamba na ujenzi wa maduka makubwa Michenzani ambayo yanatarajiwa kukamilika hivi karibuni.

Aidha, alieleza kuwa miradi yote ya ujenzi wa barabara, mipango uya ujenzi wa bandari ya Mpiga Duri, bandari ya mafuta na gesi Mangapwani sambamba na ujenzi wa Uwanja wa ndege wa Pemba iko pale pale ambapo katika bajeti ijayo ya fedha imepangwa kuanza utekelezaji wa ujenzi wa uwanja huo wa ndege wa Pemba.

Rais Dk. Shein aliongeza kuwa Mipango ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu 2020 uko pale pale na Tume ya Uchaguzi itatangaza tarehe wakati utakapofika.

Alieleza kuwa wapo baadhi ya wananchi waliodhania kuwa uchaguzi umeaghirishwa jambo ambalo halipo na kusisitiza kuwa uchaguzi upo na utatangazwa na Tume husika wakati utakapofika ndani ya mwaka huu mnamo mwezi wa Oktoba.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alisema kuwa bado Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inajiweza na kwa yeyote aliyekuwa na nia ya kuisaidia anakaribishwa lakini bila ya kuiwekea masharti Serikali kwani haiko tayari kusaidiwa kwa masharti.

Aidha, Rais Dk. Shein aliwaeleza viongozi hao kuwa miezi iliyobaki kabla ya uchaguzi mkuu mwaka huu ni miezi ya kuzidisha utendaji wa kazi na sio kufanya kazi kwa mazoea na kuwataka kufanya kazi kwa juhudi na maarifa pamoja na kuwasimamia  wale wote wanaowaongoza.

Dk. Shein alisisitiza kuwa Bajeti ijayo ni lazima ifanywe vizuri kwa kusimamia kwa kasi mipango itakayopangwa na Serikali na kuwataka viongozi hao kuondoa muhali na kujuana katika utendaji wa kazi kwani kwenye kazi hakuna udugu wala urafiki.

Aliongeza kuwa katika kazi hakuna muhali na kusisitiza kuwa asiyefanya wajibu wake ipasavyo ashughulikiwe kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za kazi bila ya kuwaonea wafanyakazi.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein aliwakata viongozi hao kusimamia kazi na kuondokana na tabia ya kulaumiana na kushutumiana na badala yake wafanye kazi kwa kushirikiana kwa azma ya kufikia malengo yaliokusudiwa.

Aliwataka viongozi hao kujenga utaratibu wa kuambizana ukweli katika vikao vyao na kuvitumia vikao hivyo kama ni sehemu ya usuluhishi wa changamoto zinazojitokeza katika maeneo yao ya kazi kwani huo ndio utawala bora.

Aliwataka viongozi hao kuzifahamu Sheria za Utumishi wa Umma sambamba na Kanuni zake huku akiwataka kuendelea kuwa wamoja na kuwa na mapezi miongoni mwao.

Rais Dk. Shein aliwataka viongozi hao kusimamia maadili ya viongozi wa Umma ikiwa ni pamoja na kupambana na rushwa na uhujumu wa uchumi.

Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwakumbusha viongozi hao maagizo ya muda mrefu aliyoyatoa ambayo yamechelewa kutekelezwa katika maeneo mbali mbali kiswani humo na kutoa muda maalum yawe tayari yamekamilika.

Aliongeza kuwa hakuna mbadala wa kazi hivyo, aliwataka viongozi hao kufanya kazi kwa bidii, maarifa na ubunifu mkubwa ili Zanzibar iendelee kupata maendeleo endelevu.

Nao viongozi hao walitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa hatua yake hiyo ya kufanya mazungumzo nao na kuahidi kuwa maelekezo aliyowapa watayafanyia kazi sambamba na kuzidisha kasi ya uchapaji kazi.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.