Habari za Punde

Naibu Waziri Nyongo Awataka viongozi wa vijiji kushiriki kutoa elimu ya uwekezaji katika sekta ya madini kupunguza migogoro


Mkurugenzi wa Kampuni ya Busolwa Mining LTD, Baraka Ezekiel akielezea jambo kwa ujumbe ulioambatana na Naibu Waziri Nyongo wakati wa ziara ya kukagua kusikiliza na kutatua changamoto za mwekezaji huyo.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kushoto) akiambatana na ujumbe wake wakati wa ziara katika mgodi wa uchimbaji wa kati wa madini unaomilikiwa na Kampuni ya Busolwa Mining LTD. Kulia ni Mkurugenzi wa mgodi huo, Baraka Ezekiel akielezea namna mitambo iliyosimikwa katika eneo hilo itakuwa ikifanya kazi mara baada ya ujenzi wake kukamilika
Mkurugenzi wa Kampuni ya Busolwa Mining LTD, Baraka Ezekiel akielezea jambo kwa ujumbe ulioambatana na Naibu Waziri Nyongo wakati wa ziara ya kukagua kusikiliza na kutatua changamoto za mwekezaji huyo. (Picha na Wizara ya Madini).



Na Nuru Mwasampeta, WM

NAIBU Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo ameutaka uongozi wa Kijiji cha Buhunda maarufu kama Lushokela kilichocho wilayani Misungwi mkoani Mwanza kutoa elimu ya uwekezaji kwa wananchi wake ili kuwa na uelewa juu ya masuala ya uwekezaji katika sekta ya madini.




Naibu Waziri Nyongo alitoa maelekezo hayo Aprili 12, 2020 alipotembelea mradi mpya wa uchimbaji wa madini unaomilikiwa na Kampuni ya Busolwa Mining LTD uliopo katika Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, baada ya kuelezwa ugumu wa mwananchi katika kupisha mradi kwa mwekezaji huyo na kudai naye anataka kuchimba
katika eneo hilo.



“Hapa ni suala la uelewa tu, elimu ya uwekezaji katika sekta ya madini inatakiwa kwa wananchi, na watoaji wa elimu wa kwanza ni ninyi viongozi wa Serikali za vijiji na mitaa.



"Mchimbaji akiomba na kupewa leseni mmiliki wa ardhi anapaswa kulipwa fidia na kupisha eneo hilo ili kupisha shughuli za uchimbaji,"Nyongo alisisitiza.



Kufuatia changamoto ya utoaji wa mizigo bandarini, Naibu Waziri Nyongo ameahidi kufanya mazungumzo na uongozi wa Shirika la Taifa la Usafirishaji (TASAC) kuhakikisha inaharakisha taratibu za  utoaji wa mizigo bandarini ili vifaa hivyo vitolewe kwa wakati kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo na kuwafanya wawekezaji kukamilisha miradi yao kama walivyokusudia.



Kutokana na changamoto ya ugonjwa wa Corona unaoikabili Dunia, uliopelekea baadhi ya vifaa vinavyohitajika kwa ajili ya ukamilishaji wa ufungaji wa mitambo mgodini hapo kutokupatikana kwa wakati, Naibu Waziri Nyongo alisema, changamoto hiyo inaelekea ukingoni kwani nchi ya China ambako ndiko vilikiagizwa vifaa hivyo tayari viwanda mbalimbali vimefunguliwa na vinazalisha hivyo watarajie ukomo wa changamoto hiyo ndani ya muda mfupi.



Kwa upande wake Mkurugenzi na mwekezaji wa migodi ya Busolwa Mining, Baraka Ezekiel alisema wameshakusanya mchanga wa dhahabu utakaoweza kuchenjuliwa katika mgodi wao mpya wa Misungwi kwa muda wa mwaka mmoja na kubainisha kuwa, kwa sasa wanasubiri kukamilika kwa ujenzi wa mradi huo uliokwamishwa kwa kiasi kikubwa na mlipuko wa janga la corona duniani.



Akifafanua suala hilo, Baraka alisema, baadhi ya vipuri vya kukamilisha ufungaji wa mitambo katika mgodi huo ulisimama kutokana na uzalishaji wa vipuri, hivyo nchini China kusimama, lakini pia wataalamu waliokuwa wakisaidia ufungaji wa mitambo hiyo hawakuweza kurudi mara baada ya kusherehekea sikukuu za mwaka mpya wa Kichina kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa corona uliopelekea mipaka nchini humo kufugwa.



Pamoja na hayo ameeleza changamoto nyingine kuwa ni pamoja na ucheleweshwaji wa kutoa mizigo bandarini, umeme mdogo kwa ajili ya kuendeshea mitambo yao, na mgogoro wa eneo baina yake na mwananchi anayedai kutaka kuchimba madini katika eneo la leseni hiyo.



Akizungumzia suala la ajira, Baraka alisema mgodi huo unatarajia kuajiri watumishi wa kudumu wapatao 88 miongoni mwao saba watatoka nje ya nchi kwa ajili ya kusaidia kuelekeza wazawa namna ya kuendesha mitambo hiyo na pia itatoa ajira zisizo rasmi kwa watu 200 hivyo kufungua fursa za ajira kwa watanzania.



Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Juma Sweda ameiomba Serikali kufungua soko la madini wilayani humo na kubainisha kuwa tayari ofisi yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Madini wamekwisha andaa jengo kwa ajili ya soko hilo na kubainisha kuwa kinachokosekana ni mashine za kupimia purity ya madini ya dhahabu sokoni hapo.



Sweda alisema, kufunguliwa kwa soko hilo kutaisaidia Serikali katika suala zima la ukusanyaji wa mapato, lakini pia kuwapa fursa wachimbaji wadogo waliopo katika eneo hilo kuuza madini yao sokoni hapo kuliko kusafiri mpaka Mwanza jambo ambalo linahatarisha usalama wao.



Akijibu hoja hiyo ya Mkuu wa Wilaya Sweda, Naibu Waziri Nyongo alimwagiza Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mwanza kuhakikisha soko hilo linawezeshwa mapema na kufunguliwa ili kuwezesha biashara ya madini wilayani hapo kufanyika sokoni hapo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.