Habari za Punde

Taasisi za Kijamii Ziwe za Kitaifa na Kimataifa Kuendelea Kuungana na Serikali Katika Kutoa Taaluma Kwa Jamii

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Shaaban Seif Mohamed Kulia akipokea Hundi ya Shilingi Milioni 8,400,000/- kutoka kwa Uongozi na Wanachama wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Kuweka na Kukopa Zanzibar {ZASCU}.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Shaaban Seif Mohamed akizungumza na Uongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Kuweka na Kukopa Zanzibar {ZASCU}mara baada ya makabidhiano hayo.
Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Kuweka na Kukopa Zanzibar Nd. Rajab Haji Dawa akifafanua uamuzi wa Wanachama wake kujitolea kuchangia mfuko Akaunti ya Corona katika mapambano dhidi ya Maradhi yanayosababishwa na Virusi vya COVID – 19.   
Picha na – OMPR – ZNZ.         
Na.Othman Khamis.OMPR.
Taasisi za Kijamii zile za Kitaifa na Kimataifa bado zina wajibu wa kuendelea kuungana na Serikali katika kutoa Taaluma ya kina kwa Jamii jinsi Taifa linavyoweza kufanikiwa kuvuka vyema kwenye mapambano yake dhidi ya Maradhi yanayosababishwa na Virusi vya Corona {COVID – 19}.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Shaaban Seif Mohamed alitoa kauli hiyo wakati akipokea mchango wa Shilingi Milioni 8.400,000/- ambazo tayari zimeshaingizwa kwenye Akaunti ya Mfuko wa Corona zilizotolewa na Wanachama wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Kuweka na Kukopa { ZASCU } hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Nd. Shaaban alisema juhudi zinazochukuliwa na Viongozi Wakuu wa Serikali zote Mbili Nchini Tanzania Bara na Zanzibar katika kukabiliana na Janga liliopo hivi sasa lazima ziungwe mkono huku Wananchi hasa Wafanyakazi wakazingatia umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii ili Taifa lisonge mbele Kiuchumi na Maendeleo.
Alibainisha wazi kwamba Ugonjwa unaosababishwa na Virusi vya Corona bado upo na kumgusa moja kwa moja kila Mwanajamii. Lakini suala la kuchapa kazi ni wajibu kwa kila Mwananchi awe katika Sekta ya Umma na hata zile za Ujasiri Amali.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwashukuru Wanachama na Viongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Kukopa na Kuweka kwa wazo lao la kusaidia nguvu za Serikali na bado Taasisi yoyote iko huru na wazi kukaribishwa kuchangia Mfuko wa Corona Nchini.
Akitoa maelezo yaTaasisi hiyo ya Biashara kuamua kuchangia harakati za Mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Kuweka na Kukopa Nd. Rajab Haji Dawa alisema janga la Corona linawagusa moja kwa moja kwa vile asilimia kubwa ya Wanachama wake ni Wafanyabiashara wanaozunguuka sehemu tofauti ndani na nje ya Nchi.
Nd. Dawa alisema Wanaushirika hao walihamasishana na kufikia hatua ya kuwagaia Maski Wananchi katika maeneo mbali mbali Nchini, na pale Serikali Kuu ilipofungua milango ya Michango ndipo walipokuja la wazo la kuwasilisha Mchango wao huo wa Fedha Taslim.
Mapema Mkurugenzi wa Vyama vya Ushirika Zanzibar Nd. Khamis Daudi Simba aliyeshuhudia tukio hilo la makabidhiano ya mchango huo alisema Kanuni ya Saba ya Kimataifa ya Vyama vya Ushirika imeweka wazi kwa Vyama au Vikudi vya Ushirika kujali ustawi wa Jamii unaovizunguuka  Vyama hivyo.
Nd. Daudi alisema Uamuzi wa Wanachama wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Kuweka na Kukopa Zanzibar unapaswa kupongezwa kwa vile umezingatia Kanuni hiyo hasa kipindi hichi ambacho Jamii imekumbwa na Maradhi yanayosababishwa na Virusi vya Corona Nchini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.