Habari za Punde

Bilioni 21 kutumika kusaidia kaya masikini na TASAF


Muwezeshaji kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {Tasaf} Mecy Mandawa akitoa Mada kwenye Mafunzo ya Watendaji wa kusimamia uhakiki wa Kaya Maskini Zanzibar.
Msimamizi Mkuu wa Tasaf Zanzibar ambae pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Shughuli za Serikai SMT na SMZ Nd. Khalid Bakar Amran akisisitiza umuhimu wa uadilifu kwa washiriki hao wakati wa kutekeleza majukumu yao.
Muwezeshaji kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {Tasaf} Mecy Mandawa akitoa Mada kwenye Mafunzo ya Watendaji wa kusimamia uhakiki wa Kaya Maskini Zanzibar.

Watendaji mbali mbali watakaoshiriki katika zoezi kuhusu kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu ya Tasaf na uhakiki wa Kaya Maskini wakifuatilia Hotuba ya ufunguzi wa Mafunzo yao hapo katika Katika Kampas ya Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar {SUZA} iliyopo Beit El Ras.

Picha na OMPR

Na Othman Khamis, OMPR


Zaidi ya Shilingi Bilioni 21 zinatarajiwa kutumika kwa walengwa wa Kaya Maskini ndani ya kipindi cha Mwaka ikiwa ni ongezeko kubwa  baada ya Miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Nchini Tanzania {TASAF} kufanya vizuri katika Awamu Mbili za awali Visiwani Zanzibar.

Ongezeko hilo ni kutoka Shilingi Bilioni Kumi na Mbili { 12,000,000,000/-}katika Awamu zilizopita baada ya Zanzibar kushamiri kwenye utekelezaji wa Miradi mbali mbali ya Tasaf Awamu Mbili za kwanza.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania |TASAF} Nd. Ladislaus Mwamanga amesema hayo wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uelewa watendaji mbali mbali watakaoshiriki katika zoezi kuhusu kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu ya Tasaf na uhakiki wa Kaya Maskini.

Nd. Mwamanga amewataka washiriki hao kufanyakazi ya uhakiki kwa uadilifu mkubwa ili kwenda na agizo la Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli la kuwataka Watendaji kufanya kazi hiyo ili kuweza kufikia malengo ya Serikali katika matumizi mazuri ya fedha za Umma.

Alisema ni jukumu la Watendaji na washiriki hao kuhakikisha kwamba wanawaandikisha walengwa wa Kaya Maskaini wenye sifa zilizokusudiwa na kuacha ubadhirifu kwa kutumia fursa hiyo kuwaingiza Watu wasiohusika na sifa kwa maslahi binafsi huku wakizingatia kanuni za Afya katika kujikinaga na Corona.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Shughuli za Serikai SMT na SMZ Nd. Khalid Bakar Amran amesema katika zoezi hilo la uhakiki wa Kaya Maskini, Tasaf imeamua kuwatumia Watendaji wa Serikali ili kuwaongezea ufanisi utakaoleta udhibiti katika utekelezaji wa kazi hiyo ili ifanyike vyema.

Ndugu Khalid ambae pia ni Msimamizi Mkuu wa Tasaf Zanzibar amewataka Watendaji hao kuacha muhali katika utekelezaji wa majukumu yao na Serikali haitosita kumchukulia hatua Mtendaji ye yote atakayekwenda kinyume na utaratibu uliopangwa.

Aidha maewakumbusha Washiriki hao kujitahidi kutumia Lugha nzuri watakapokuwa katika sehemu zao za Kazi kwani Walengwa wengi watakaowafikia wamekuwa na uelewa tofauti.

Alisema zoezi la Uhakiki la kuzitambua Kaya Maskini kwa upande wa Zanzibar linatarajiwa kuanza Alhamis ambapo jumla ya Kaya Elfu 32,661 zinatarajiwa kufanyiwa uhakiki huo.

Nao Washiriki wa Mafunzo hayo wameupongeza Uongozi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {Tasaf} kwa kuwapatia Taaluma hiyo itakayowasaidia kutekeleza vyema jukumu walilopangiwa.

Pamoja na mambo mengine washiriki hao wamependekeza pamoja na mfumo Mpya wa Kieletroniki uliobuniwa lakini kuna haja ya kuweka utaratibu mbadala endapo kutajitokeza changamoto wakati kazi ikiendelea.

Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mfuko huo wa Maendeleo ya Jamii {Tasaf}imejipangia kutumia Jumla ya Shilingi Trilioni 2.03 zilizotolewa Mkopo na Benki ya Dunia katika kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu ya Tasaf ndani ya Miaka Minne ijayo.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.