Habari za Punde

Mafanikio ya ya Utekelezaji wa Haki za Binaadamu na Utawala Bora Zanzibar Azma ya Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964.Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Uongozi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Tanzania, ukiongozwa na Mwenyekiti wa Tume hiyo (kulia kwa Rais) Jaji Mstaaf Mathew Paua Mhina, Makamu Mwenyekiti Mhe. Mohammed Khamis Hamad,Kamishna Mkaazi Zanzibar.Mhe. Khatib Mwinyichande na Kamishna Nyanda Shuli, walipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amesema kuwa mafanikio ya utekelezaji haki za binaadamu na utawala bora Zanzibar yanatokana na utekelezaji wa azma ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964.

Hayo aliyasema leo, Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na ujumbe wa uongozi wa Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora ukiongozwa na Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mstaafu Mathew Pauwa Muhina Mwaimu, wakati ujumbe huo ulipofika Ikulu kwa ajili ya kujitambulisha.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Shein alisema kuwa Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964 yalikuwa na azma katika kuhakikisha wananchi wa Zanzibar wanapata hali zao za msingi ikiwemo elimu bure, afya bure pamoja na ardhi, mambo ambayo kabla ya Mapinduzi yalitolewa kwa ubaguzi.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa Zanzibar ina historia kubwa  katika kupambana na juhudi za kuhakikisha wananchi wake wanapata haki zao za msingi pamoja na kuwepo kwa utawala bora tokea kupatikana kwa uhuru wa Zanzibar.

Rais Dk. Shein alisema kuwa hatua hizo zimeipelekea Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hadi hivi leo kuendeleza haki za binaadamu sambamba na utawala bora na kupelekea kuipaisha Zanzibar kidemokrasia.

Hivyo, Rais Dk. Shein alisisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haiko tayari kukeuka vifungu vya Katiba na Sheria zilizopo katika suala zima la haki za binaadamu na utawala bora na badala yake itaendelea kufuata taratibu zilizopo kwa ajili ya manufaa ya nchi na wananchi wake wote.Rais Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepata mafanikio makubwa katika sekta za elimu na  afya  hiyo ni kutokana na kutekeleza vyema lengo na azma ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964 katika kuhakikisha wananchi wanapata haki zao za msingi ambazo hapo mwanzo hawakuzipata.

Aliongeza kuwa hatua hiyo ndiyo iliyoipelekea Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba baada ya kuingia madarakani chini ya uongozi wake baada ya uchumi kuimarika kuendeleza azma ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964 ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu bila ya malipo ikiwemo afya na elimu.

Aidha, Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuipongeza Tume hiyo kwa kufanya kazi zake vyema na kusisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Tume hiyo ili iweze kufikia malengo iliyoyakusudia.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alieleza kuwa Zanzibar haina utamaduni wa kuvunja haki za binaadamu na badala yake imekuwa ni nchi yenye kufuata na kutekeleza haki za binaadamu, utawala bora  pamoja na demokrasia kwa vitendo.

Kwa upande wa mafanikio yaliopatikana nchini katika kupambana na janga la COVID-19, Rais Dk. Shein alisema kuwa Jamhuri ya Muungano ikiwemo Zanzibar imeweza kupata mafanikio makubwa kutokana na mikakati maalum iliyoiweka hali iliyopelekea kupungua kwa janga hilo kwa kiasi kikubwa.

Rais Dk. Shein aliongeza kuwa Serikali zote mbili zitaendelea na mikakati hiyo iliyoiweka ikiwa ni pamoja na kutoa elimu juu ya janga hilo kwa wananchi wake bila ya kuiga wala kufuata taratibu na mipango ya wengine na badala yake itafuata taratibu ilizoziweka bila ya kushurutishwa.

Mapema  Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora Jaji Mstaafu Mathew Paua Muhina Mwaimu alieleza kuwa Rais Dk. Shein katika uongozi wake amefanya mambo mengi mazuri kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa Zanzibar ukiwemo utekelezaji wa haki za binaadamu na utawala bora kwa vitendo.

Alieleza kuwa hali ya kisiasa imeendelea kuwa shwari zaidi lakini jitihada za Rais Dk. Shein zimeonekana dhahiri katika kulinda na kukuza haki za binaadamu kama zilivyoorodheshwa katika Katiba ya Zanzibar hasa haki za kijamii.

Aliongeza kuwa wameshuhudia kuwepo skuli nyingi pamoja na vituo kadhaa vya afya ambavyo vyengine vinaendelea kujengwa hali inayoonesha dhahiri kwamba Serikali anayoiongoza Rais Dk. Shein imetilia mkazo katika kuendeleza haki ya afya na wananchi kupata elimu bora.

Kiongozi huyo alieleza kuwa anamatumaini makubwa kuwa kutokana na jinsi Rais Dk. Shein anavyoongoza nchi vizuri katika kipindi cha kuelekea miaka kumi hivi sasa, uchaguzi mkuu ujao utakuwa wa amani.

Aidha, kiongozi huyo alieleza kuwa Tume hiyo inafurahia na kuunga mkono uwepo wa haki za binaadamu katika Katiba ya Zanzibar ambapo haki zilizopo katika Katiba hiyo ni zile zile zilizopo katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na pia katika mikataba mbali mbali ya Kimataifa.

Tume hiyo ilieleza kuwa kuwepo kwa Wizara yenye dhamana na haki za binaadamu na Wizara yenye dhamana ya masuala ya utawala bora ni hatua muhimu katika kuhakikisha kwamba haki za binaadamu zinalindwa na kukuzwa na misingi ya utawala bora inazingatiwa kwa madhumuni ya kuwafanya wananchi wafurahie haki zao za Kikatiba na waishi kwa amani.

Pamoja na hayo, Tume hiyo waliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kufanya jitihada za pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika vita dhidi ya janga la Corona.

Hata hivyo, Tume hiyo imepongeza hatua za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kulegeza baadhi ya masharti ili shughuli mbali mbali ziendelee zikiwemo za kiuchumi ikiwemo sekta ya utalii ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa Zanzibar.

Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora ni Taasisi ya Muungano ambayo iliianzishwa mwaka 2000 kupitia Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ambapo kwa upande wa Zanzibar Tume hiyo ilianza rasmi kufanya kazi zake mwaka 2007.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.