Habari za Punde

Umoja wa Wawakilishi Wanawake Zanzibar (UWAWAZA) Wampongeza Mama Mwanamwema Shein Kwa Ushirikiano Wake Katiika Shughuli za Kijamii Zanzibar.UMOJA wa Wawakilishi Wanawake Zanzibar (UWAWAZA) umempongeza Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein kwa kushirikiana nao kikamilifu katika hafla ya kuvunjwa kwa Baraza la Tisa la Wawakilishi hivi karibuni.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wawakilishi Wanawake Zanzibar (UWAWAZA) ambaye pia ni Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi  Zanzibar Mgeni Hassan Juma akitoa pongezi kwa niaba ya Umoja huo huko Ofisini kwake Chukwani, Jijini la Zanzibar alisema kuwa wanampongeza Mama Shein kwa kuujali mwaliko waliompa na kuweza kushirikiana nao kikamilifu katika hafla hiyo.

Mwenyekiti huyo wa Umoja huo alieleza kuwa (UWAWAZA) pamoja na viongozi wengine wote wanaume wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar wamefurahishwa sana na ujio wa Mama Shein katika hafla hiyo adhimu na kusisitiza kuwa wanatoa pongezi zao za dhati kwa Mama Shein.

Alieleza kuwa Mama Shein amekuwa mstari wa mbele katika kushirikiana na Wajumbe wa Baraza hilo ukiwemo Umoja wa Wawakilishi Wanawake Zanzibar (UWAWAZA), ambao amekuwa akiuthamini pamoja na wajumbe wake wote.

Aliendelea kumshukuru na kumpongeza Mama Shein kwa ushirikia wake mkubwa katika shughuli mbali mbali za kimaendeleo zikiwemo za kijamii, kisiasa na kiuchumi Unguja na Pemba.

Aliongeza kuwa Mama Mwanawema amekuwa akishirikiana nao katika shughuli mbali mbali za kisiasa Unguja na Pemba ikwia ni pamoja na kushiriki kikamilifu katika kuwanga mkono akina mama katika Umoja wao wa Wanawake Tanzania (UWT) hapa nchini.

Aidha, alieleza kuwa Umoja huo unampongeza Mama Shein kwa misaada yake mbali mbali anayotoa kwa jamii na kusisitiza kuwa Umoja huo unathamini sana michango na misaada yake hiyo anayoitoa kwa jamii bila ya kujali rangi, dini, jinsia, itikadi wala wapi mtu anatoka.

Mwenyekiti huyo wa (UWAWAZA), kwa niaba ya viongozi wenziwe wa Umoja huo alimuelezea Mama Shein kuwa alikuwa kiungo kikubwa sana katika maendeleo ya Zanzibar yakiwemo ya kisiasa kwani amekuwa akimpa moyo sana Rais Dk. Shein katika shughuli zake mbali mbali za kisiasa.

Sambamba na hayo, Mwenyekiti huyo alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Shein kwa kumpongeza na kumshukuru Mama Mwanamwema Shein katika hotuba yake ya kuvunjwa kwa Baraza la Tisa la Wawakilishi aliyoitoa hivi karibuni huko katika ukumbi wa Baraza hilo, Chukwani nje kidogo ya Jijini Zanzibar.

Naibu Spika huyo wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja huo wa (UWAWAZA) alisisitiza kuwa akina mama wamekuwa na mchango mkubwa sana katika maendeleo ya wanaume na kumuelezea Mama Shein jinsi alivyoshirikiana na Rais Dk. Shein katika kipindi chake chote cha uongozi.

Alisisitiza kuwa katika uongozi wa Rais Dk. Shein maendeleo makubwa yamepatikana katika sekta zote za maendeleo zikiwemo zile za kiuchumi, kisiasa na kijamii na kueleza kuwa kiongozi huyo ameonesha mfano mkubwa wa kiongozi bora mwenye uongozi uliotukuka.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.