Habari za Punde

Ziara ya Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa Wilayani Ruangwa

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Nambilanje wilayani Ruangwa akiwa katika ziara ya kikazi, Juni 23, 2020.

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli imedhamiria kufikisha huduma ya umeme katika vijiji vyote nchini vikiwemo na vijiji 25 vya wilaya ya Ruangwa ambavyo bado havijafikiwa na umeme.

Kufuatia hatua hiyo, Waziri Mkuu amewataka wananchi walio katika vijiji ambavyo bado havijaunganishiwa nishati ya umeme wafanye maandalizi kwa sababu maeneo mengine tayari wakandarasi wameshapatikana.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumanne, Juni 23, 2020) wakati alipozungumza na wananchi katika vijiji vya Nanjaru, Nambilanje, Mkaranga, Namichiga na Mbekenyera akiwa kwenye ziara yake ya kikazi wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi.

Amesema wilaya ya Ruangwa ina jumla ya vijiji 90 kati yake vijiji 25 tu ndio bado havijafikiwa na huduma ya umeme lakini tayari mkandarasi ameshapatikana na ameshaanza kazi, hivyo aliwataka wananchi wajiandae kuunganisha umeme kwenye nyumba zao za makazi na biashara.

“Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli anataka kuona kila nyumba ya Mtanzania inawaka umeme na amepunguza gharama za kuunganisha umeme kutoka sh. 380,000 hadi sh. 27,000 ili kila mwananchi aweze kumudu gharama hizo.”

Waziri Mkuu ameongeza kuwa licha ya gharama za kuunganishiwa umeme kupunguzwa, pia wananchi hatolazimika kulipia gharama za nguzo pamoja na gharama za fomu za maombi ya kuunganishiwa umeme kwani tayari zimeshalipiwa na Serikali.
      
Vilevile, Waziri Mkuu amesema Serikali imeboresha huduma za afya kwa kuhakikisha kuwa dawa na vifaa tiba vinapatikana katika maeneo yote ya kutolea huduma za afya na kwamba haitaki kuona mwananchi anakwenda maeneo hayo na kukosa huduma.

“Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli alipoingia madarakani aliongeza bajeti ya dawa kutoka sh bilioni 31 na kufikia sh. bilioni 269, hatutarajii kusikia mgonjwa amekwenda zahanati akaandikiwa cheti na kisha akaelekezwa kwenda kununua dawa kwenye maduka ya watu binafsi.”

Waziri Mkuu amesema ni lazima dawa zipatikane katika maeneo yote ya kutolea huduma za afya kulingana na hadhi ya eneo husika kama zahanati lazima dawa zinazotakiwa kuwepo kwenye zahanati ziwepo, kadhalika kituo cha afya na hospitali.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akitazama magunia ya ufuta wakati alipotembelea ghala la  Chama cha Ushirika cha msingi cha Nanjaru wilayani Ruangwa
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokelewa kwa nyimbo wakati alipowasili kwenye kijiji cha Nanjaru akiwa katika ziara ya kikazi wilayani Ruangwa
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokelewa kwa nyimbo wakati alipowasili kwenye kijiji cha Nanjaru akiwa katika ziara ya kikazi wilayani Ruangwa, Juni 23, 2020. 
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.