Habari za Punde

Mjue Balozi Seif Ali Idd, Jemedari anayestaafu kwa heshima Zanzibar


Jina kamili alilopewa na wazee wake Tarehe 30 February siku ya Saba ya uzao wake ni Seif Alli Iddi. 

Amezaliwa tarehe 23 February 1942 huko Mgambo Jimbo la Kitope Wilaya ya Kaskazini B, Mkoa wa Kaskazini Unguja. 

Balozi Seif aliianza safari yake ya kielimu Skuli ya msingi Kinyasini 1949 hadi 1956. 

Mwaka wa 1957 alijiunga na masomo yake ya Sekondari katika Skuli ya Beit El Ras iliyopo Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja hadi 1962. Alifanikiwa kufaulu masomo yake ya Sekondari na kuchaguliwa kuwa miongoni mwa wanafunzi watakaojiunga na Elimu ya juu kipindi hicho. 

Januari 1963 alijiunga na chuo cha Ualimu Nkrumah kusomea Ualimu kwa ngazi ya diploma (Diploma in education).Alihitimu masomo yake Disemba 1964. 

Balozi Seif aliajiriwa katika serikali ya Mapinduzi Zanzibar baada ya Mapinduzi matukufu ya 1964, na kuwa Mwalimu.

Aliianza kazi yake ya Ualimu mwaka 1965 hadi 1968 ambapo alisomesha Skuli ya Kinyasini, Skuli aliyosoma akiwa msingi pia alifanikiwa kuwa Mwalimu Mkuu Skuli ya Sekondari ya Nungwi.

Mzee Hussein Machano Faki ni miongoni mwa Wanafunzi waliopata bahati kusomeshwa na Mh. Balozi anasema hatomsahau Balozi Seif, Mzee Hussein anasema nafikiri mwenyewe amesahau lakini mimi sitomsahau kitendo chake cha kuniteua mimi kuwa kiongozi darasani, mbali ya Uongozi huu Balozi Seif alikuwa akitoa pesa zake mfukoni na kunipa mm, wakati huo maisha kwetu yalikuwa magumu sana, umbali mrefu tuliokuwa tukitoka alikuwa akitupa moyo sana, Skuli nzima tulimpenda hadi kufikia kutoa machozi alipoondoka Skuli yetu nakumbuka ilikuwa mwaka 1968 km sikosei.

Balozi Seif pia alifanikiwa kuwafundisha watu mbali mbali mashuhuri akiwemo  Pereira Juma Silima Katibu wa NEC, Idara ya Oganaizesheni CCM Taifa. 

Mwaka 1968 baada ya kutoka Skuli kama Mwalimu, aliteuliwa kuwa "Foreign service officer  katika Ubalozi wa Tanzania Cairo Misri  hadi 1971. 

Mwaka 1973 alijiunga na Chuo Kikuu cha Taifa cha Australia (National University of Australia) akisomea kozi ya "International relation and Diplomacy" alifaulu vizuri na kuwa ni miongoni mwa Wanafunzi bora waliohitimu vizuri chuoni hapo.

Balozi Seif Ali Idd siku alipoteuliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein kuwa Makamo wa Pili wa Rais 2015. Kulia ni mke wa Balozi Mama Asha 

Punde alipomaliza ilimpelekea kuanza kushika nyadhifa mbalimbali za Kitaifa na Kimataifa. Alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Netherland mwaka 1989 hadi 1993, Balozi wa Tanzania nchini China 1993 hadi 1999, Naibu Waziri wa mambo ya nje 2005 hadi 2010, Mkurugenzi, Idara ya mambo ya nje Zanzibar 1999 hadi 2000, Mbunge wa Jimbo la Kitope, Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda na Makamo wa PILI wa Raisi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar nafasi ambayo anayo hadi Sasa.

Kisiasa Mheshimiwa Balozi nafasi kubwa aliyoshika ni Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar mwaka 2000 hadi 2002.

Wasaidizi wa karibu wa Mh. Balozi wanasema, Balozi ni mtu mcheshi, mchangamfu  na mwenye kupenda mzaha wakati ambao wa mzaha, ila ni mkali anapokupa kazi na usiifanye vile inavyotakiwa.

Mama Asha Sleman Iddi ni mke wa Mheshimiwa Balozi nae anamzungumzia Balozi ni mtu anaependa mzaha na ucheshi, anasema tofauti na watu wanavyomzungumza Balozi.

Balozi ni mcheshi na mchangamfu sana hadi wageni wengi wakija nyumbani hawaamini. Alisema Bi Asha. 

Wananchi na wakaazi wa Mahonda ambao ndio Muwakilishi wao, wanasema hawatoacha kumkumbuka Balozi kwa mambo aliyowafanyia, hapa tulipowahoji watu wa Mahonda walitupa orodha ndefu ya mambo ya Balozi aliyowafanyia na mengine ya kusaidia hadi watu binafsi (shida binafsi). Maji, umeme, barabara, kuwakwamua kina mama na vijana kujiajiri ambapo amesaidia vikundi vingi vya kina mama fedha taslim. 

Kwa kweli Kuna mambo mengi waliyofanyiwa wana Mahonda ndio maana wanasema JEMEDARI huyu jimboni kwetu atastaafu kwa heshima. Anastaafu bado tunamuhitaji. 

Kwa kumalizia historia hii Nami sitomsahau Balozi Seif Alli IDDI kwa kile kitendo Chake cha kujiweka karantini yeye na wasaidizi wake wote nyumbani kwake Kama, ambapo gharama yote ikawa juu yake (kula na kulala) kwa siku zisizopungua 14 wakati wa maambukizi ya COVID-19, waliporejea kutoka Cuba.

Kitendo hiki wafasiri wengi wa mambo tulikitafsiri ni kitendo cha kizalendo na ujasiri mkubwa kwa kiongozi huyu, ambapo kitendo Chake hiki ameifundisha jamii na jamii ya Viongozi kutokuwa na kiburi na majivuno hasa yanapokuja maamuzi ya Kitaifa juu ya jambo fulani. 

IMEANDALIWA NA
Ahmed Abuu Abdhar
Zanzibar

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.