Habari za Punde

Jeshi la Polisi Lakaa na Viongozi wa Vyama vya Siasa Kuzungumzia Amani na Utulivu Wakati wa Kampeni na Uchaguzi

Na Hamida Kamchalla, TANGA.
JESHI la polisi kwa kushirikiana na Vyama vya siasa mkoani Tanga wamekaa kikao cha pamoja na kukubaliana kuweka taratibu za kuuweka mkoa huo katika hali yake ya amani kipindi cha kampeni na hata baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu.

Akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake Kamanda wa polisi mkoa wa Tanga Blasius Chatanda alisema kuwa jeshi hilo limekutana na kamati yake ya ulinzi na usalama ya mkoa pamoja na vyama vyote vya mkoa na kuweka mikakati itakayohakikisha waa huo wanakuwa katika hali ya amani kama ilivyo sasa. 

Chatanda alibainisha kwamba wamekubaliana kwamba kampeni zifanyike za kistaarabu ambazo hazitakuwa na lugha za matusi wala uchochezi na kuendelea kuilinda amani na utulivu vilivyopo kila mmoja akiwajibika kwa nafasi yake bila kuleteana madhara ya kupigana mabomu 

"Kama mlivyoona muda mfupi uliopita nilikuwa na kikao na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa na wagombea pia, tumekubaliana Tanga ya sasa iwe hii hii hata baada ya kumalizika kwa uchaguzi, tuhakikishe kwamba mmoja awajibike kwa nafasi yake na tumekubaliana kwamba Tanga hatupigani mabomu" alisema.

Hata hivyo Chatanda alieleza kwamba endapo kutatokea changamoto ya baadhi watu watakaokwenda kinyume na makubaliano hayo na kusababisha uvunjifu wa amani jeshi hilo halitasita kumchukulia hatua Kali za kisheria mtu huyo.

Alibainisha kwamba katika kuelekea kampeni hadi uchaguzi mkuu na matokeo yake jeshi hilo limejipanga vizuri sana kuhakikisha zoezi hilo linakwenda vizuri na kuisha salama huku akiwahakikishia wananchi kuondoa hofu kwani hakuna mtu yeyote atayeleta vurugu au uhalifu wowote kabla hajadhibitiwa na jeshi hilo.

"Jeshi tumejipanga vizuri kuhakikisha zoezi linakwenda kwisha salama na niwahakikishie wananchi wa Tanga kwamba watakuwa salama katika kipindi chote cha kuanzia kampeni mpaka baada ya uchaguzi hakuna yeyote atakayeleta uvunjifu wa amani katika mkoa huu, tuna silaha za kutosha na tumejipanga kimwili hadi kiakili" alibainisha.

"Lakini siku zote changamoto hazikosekani, kama kuna watu watajitokeza kuufanya uchaguzi huu uonekane haufai, kwa yule atakayejaribu kuchafua zoezi hili kwa namba moja au nyingine nafasi hiyo haipo kwani tutamshuhulikia ipasavyo, kukosekana kwa amani baada ya uchaguzi kwetu tutakuwa tumefeli, sote kwa pamoja tunaweza kuifanya Tanga iwe salama" aliongeza.

Hata hivyo Kamanda aliwataka wananchi na wanachama wa vyama vya upinzani kuondoa imani potofu waliyojijengea kwamba jeshi la polisi lipo kwa ajili ya kukisaidia chama tawala pekee na badala yake wajenge imani kwamba jeshi hilo lipo kwa ajili ya kusimamia sheria tuu na siyo vinginevyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa ACT Wazalendo mkoani hapa ambaye pia ni Mgombea kiti cha ubunge wa jimbo la Tanga mjini Rashidi Jumbe alisema kuwa kikao walichokaa na kamanda wa jeshi la polisi na kamati yake wamekubaliana kuendesha kampeni za kistaarabu ikiwa ni suala zima la kudumisha amani.

Jumbe alibainisha kwamba wao wakiwa vyama pinzani wamemtaka kamanda na kuwaasa viongozi na wanachama wa chama cha mapinduzi kuacha kutengeneza mazingira ya uchochezi yatakayopelekea mtafaruku jijini humo kutokana na maandamano yanayofanyika wakati wa kwenda na kuchukua na kurudisha fomu za uteuzi.

"Kamanda alituambia tusifikie mahali tukapigana mabomu, sisi hatupendi kupigwa mabomu lakini ikibidi itakuwa hivyo kwani tunaona wenzetu wa CCM wameshaanza shamra shamra mjini hapa wakati muda huo bado, hii inaashiria uchochezi wa uvunjifu wa amani" alisema Jumbe.

Naye katibu wa wazazi mkoani hapa Elisante Msuya akimkaimu Mwenyekiti wa CCM Mkoani hapa alisema kuwa kamanda wa polisi alifanya jambo la busara kuvishirikisha vyama vyote vya siasa pamoja na kamati ya ulinzi na usalama kwani itasaidia na kuweka msisitizo kwa yeyote atakayekuwa na nia mbaya ya kuchafua amani katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi.

"Nimpongeze kamanda kwa busara zake za kutuita na kutaka tulinde amani kwani mara nyingi hawa wenzetu wa upinzani wamezoea kusema kuwa polisi wanapendelea CCM jambo ambalo sio la kweli, kwa kikao tulichokaa leo na mikakati tuliyopanga hakuna mtu atakayeweza kuleta uvunjifu wa amani katika kipindi hiki" alisema.

Katika kikao hicho Kamanda Chatanda aliwashirikisha viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa vikiwemo CCM, ACT Wazalendo, NCCR Mageuzi, UDP, CUF, TLP na CHADEMA.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.