Habari za Punde

BILIONI 3.2 ZALIPWA FIDIA KWA WANANCHI WA CHONGOLEANI



 Na Hamida Kamchalla, TANGA.

WANANCHI wa kijiji cha Chongoleani wilayani Tanga waliopitiwa na mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta linalotokea Uganda hadi Tanzania kupitia maeneo mbalimbali nchini leo wamekabidhiwa hundi zao za malipo ya fidia kiasi cha shilingi bilioni 3.2 na mkuu wa mkoa wa Tanga Martine Shigela.

Tukio la kukabidhiana hundi hizo limefanyika katika jengo la mkuu wa Mkoa ambapo kumefanyika kikao na kuwakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa mkoa, Wilaya, halmashauri, wakuu wa idara na taasisi pamoja na wananchi na viongozi wa kijiji cha Chongoleani.

Kabla ya makabidhiano hayo Mkurugenzi mtendaji wa shirika la mafuta la Taifa James Mataragio alisema kuwa shirika limepewa dhamana ya kuhakikisha linatoa huduma za mafuta kwa wananchi kwa ukaribu hivyo wanahakikisha wanatimiza lengo lililokusudiwa kwa kuwakaribia wananchi na kuyoa huduma hiyo.

Mataragio alieleza kwamba wakati wa mchakato wa kutafuta eneo la kuweka mradi huo jumla ya watu 395 walikubali kuhama na kupisha ujenzi huo na kwamba TPDC imekabidhi kiasi hicho cha redha kwa mkuu wa mkoa kwa ajili ya malipo ya fidia zao.

"Siku ya leo tutafanya mambo makuu mawili, moja ni kutoa taarifa kuhusu fidia kwa wananchi hawa na la pill ni kukabidhiana hundi ya mfano wa malipo kwa wananchi 395 na leo tunakabidhi kiasi cha shilingi bilioni 3.2 kwa mkuu wa mkoa naye atakabidhi kwa wananchi hawa" alisema.

Naye Injini Zena Saidi kutoka wizara ya nishati alieleza kwamba mara baada ya kukamilisha taratibu zote mradi huo utaanza kutekelezwa rasmi miezi mitatu ya awali kwa mwaka 2021.

Saidi aliwataka wananchi mkoani hapa kuchangamkia fursa wakati wa ujenzi huo utakapoanza kwa kuzingati uhitaji kwa walengwa kwani mambo madogo madogo yanaweza kuwakosesha nafasi badala ya kuacha watu wanaotoka mikoa mingine kuja kuzi.

"Huu mradi ulishaanza kufanyiwa tathmini hivyo na kuna kazi ilianza kufanyika, watu walishindwa kuuza nyama maana kulitakiwa nyama ya kukausha kwenye friji wao walipeleka fresh kwahiyo walijikuta wakikosa soko, vitu vidogo vidogo vinaweza kumikosesha fursa wazawa na wengine kuja kuziwania fursa hizo" alisema.

Naye mkuu wa mkoa Martine Shigela alisema kuwa mradi huo ulikuwa ukisubiriwa siku nyingi na wananchi na kama unaanzwa kutekelezwa ni wazi wananchi watarudisha imani yao kwa serikali kwa ni ilifika wakati wananchi hao walikata tamaa.

Aidha Shigela aliiomba serikali kutoa fursa katika ununuzi wa maligafi za ndani ya mkoa kwa wale watakaopatikana kufanya kazi wasitoke nje ya mkoa kununua mahitaji yatakayohitajika katika ujenzi huo huku akiwataka wananchi waliopatiwa fidia zao kutumia fedha hizo katika matumizi yatakayowaletea tija.

"Niombe kwa wale watakaopatikana kuja kufanya hivyo kazi waje watumie maligafi zetu ndani ya mkoa, lakini pia niwaase wale wanaolipwa fidia zao kwenda kuweka mipango mizuri ya biashara ya fedha mtakazolipwa ili zilete tija" alisisitiza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.