Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein Amefungua Mradi wa Nyumba za Mji Mpya wa Kwahani leo 12/10/2020. Jijini Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein Shein, akiondoa kipazia kuashiria kuweka Jiwe la Msingi la Ufunguzi wa Mradi wa Nyumba za Kisasa za Mji Mpya wa Kwahani Jijini Zanzibar, na (kushoto kwa Rais) Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Mhe.Balozi Mohammed Ramia Abdiwawa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi, wakishiriki katika kuondoa kipazia, hafla hiyo imefanyika leo 12/10/2020. 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema ujenzi wa nyumba za Mji mpya wa Kwahani, umeakisi dhamira ya chama cha Afro Shirazi (ASP) katika kuwapatia makaazi bora wananchi wa Zanzibar.

Dk. Shein amesema hayo katika Uzinduzi wa Nyumba za Mji mpya wa Kwahani, hafla iliyofanyika eneo la Kwahani, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Alisema katika Uchaguzi wa mwaka 1961, Chama cha Afro Shirazi kiliazimia kufanya mambo makubwa manne, endapo kingefanikiwa kushinda katika uchaguzi na kubainisha mambo hayo kuwa ni pamoja na kuimarisha afya, elimu, ardhi kuwa mali ya wananchi wote pamoja na kujenga  makaazi mapya kwa wananchi wa Zanzibar.

Alisema baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964, kiongozi wa Chama hicho Marehemu mzee Abeid Amani Karume aliwaelezea wananchi azma ya Serikali ya kujenga nyumba za maendeleo katika maeneo mbali mbali nchini, ambapo eneo la Kikwajuni likawa la mwanzo kuhusika na hatua hiyo mnamo Agosti 17,1964, Kilimani (Januari 16, 1966), Bambi mwaka 1966, Michenzani (Mei 5, 1970), pamoja na Gamba na Makunduchi mwaka 1971.

Dk. Shein alinukuu kauli ya Marehemu mzee Abeid Amani Karume wakati wa Ufunguzi wa nyumba za Kilimani mnamo mwaka 1971, kwa kusema ‘Lengo letu ni kuendelea mbele katika kila hali ya maisha bora mpaka tufike hatua za kuwawezesha watu kuishi maisha ya kibinadamu na kujitegemea wenyewe………’.

Alieleza katika kuendeleza dhamira hiyo, wazo la kuanza  ujenzi katika eneo la Kwahani lilikuja kutokana na matokeo ya mafuriko makubwa yaliolikumbuka eneo hilo na kujirejea kwa nyakati tofauti.

Alisema Ilani ya Uchagizi ya CCM ya mwaka 2015-2020 imebainisha uendelezaji wa ujenzi wa nyumba za kisasa ili kuiwezesha nchi kupiga hatua za maendeleo na kusema miji 14 ya Unguja na Pemba inahusishwa na ujenzi huo.

Aidha, Rais Dk. Shein alisema Serikali ilifanya uamuzi wa makusudi wa kuupandisha hadhi Mji wa Zanzibar na kuwa Jiji kamili chini ya kifungu namba 18 cha Sheria namba 7 ya mwaka 2014 ya Sheria ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa na kumteua Mkurugenzi wa Jiji hilo pamoja na Meya, baada ya kukidhi vigezo na mahitaji ya msingi,  yakiwemo ya kuwa na Manispaa zaidi ya mbili.

Alisema Serikali kwa kushirikiana na kampuni ya Bakhresa Group of Company’ imefanikiwa kuweka historia kwa kaunzisha mji mpya wa kisasa katika eneo la Fumba pamoja na kuweka miundombinu yote muhimu.

Katika hatua nyengine, Dk. Shein aliwapongeza wananchi wa Kwahani kwa kukubali kupisha ujenzi wa nyumba hizo na kusema uamuzi wao huo ni wa busara, hivyo akawataka kuzitunza nyumba hizo kwa kufanya matumizi sahihi.

Aidha, aliupongeza uongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), kwa kufanikisha ujenzi huo na kuitaka taasisi hiyo kuendelea na uwekezaji katika miradi mkubwa ya maendeleo kama hiyo.

Alichukua fursa hiyo kuipongeza kampuni ya  Estim Construction Company Limited kutoka Dar es Salaam kwa kutekeleza mradi huo kwa haraka na umahiri mkubwa pamoja na kampuni ya Arques Africa, sambamba na Bodi ya Wakandarasi ya Zanzibar kwa ushauri mzuri kwa Serikali pamoja na Wakala wa Majengo Zanzibar kwa uangalizi bora.

Mapema, Mgombea wa kiti cha Urais kupitia CCM, ambae pia Mbunge wa Jimbo la Kwahani aliemaliza muda wake, Dk. Hussein Mwinyi alimpongeza Dk. Shein kwa kazi nzuri na kubwa katika uongozi wake wa miaka kumi na kuleta mafanikio makubwa katika sekta mbali mbali, ikiwemo elimu, afya na makaazi.

Alisema kwa takriban wiki moja sasa Chama cha Mapinduzi kimekuwa kikizindua miradi mbali  mbali ya maendeleo, ikiwemo huo wa makaazi katika eneo la Kwahani na kubainisha kuwa  hatua hiyo ni utekelezaji wa Ilani ya CCM.

Alisema endapo Wazanzibari watampa ridhaa ya kuongoza Serikali, ataendeleza maono ya kuendeleza dhamira ya mtangulizi wake kwa kuendeleza ujenzi huo na kuunganika hadi eneo la Michenzani.

Aidha, alitoa shukurani kwa wananchi wa Kwahani kwa utayari wao wa kupisha ujenzi huo na hivyo kupata makaazi yalio  bora zaidi katika maisha yao.

Nae, Waziri wa Fedha na Mipango, Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa, alisema tangu Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, Serikali imekuwa ikiendeleza ujenzi wa nyumba za kisasa za makaazi katika maeneo tofauti, kwa lengo la kuwapatia makazi bora na yenye hadhi wananchi wake.

Alisema uzinduzi wa jengo hilo umefungua milango kwa majengo kadhaa kuenea katika eneo la Kwahani na maeneo mengine ya jirani hadi Kariakoo na hivyo kubadili mandhari ya eneo hilo.

Alimhakikishia Rais Dk. Shein kuwa nyumba hizo ni nzuri ndani na nje na kuwepo kwake kutafanya mandhari ya kupendeza , kiasi ambacho watu wengi wamekuwa wakihitaji kupata ramani yake.

Alisema serikali ilifanya maamuzi sahihi ya kujenga nyumba hizo na kubainisha kipaumbele chake  katika kuendeleeza ujenzi huo kupitia bajeti yake ya kila mwaka.

Aidha, Katibu Mkuu Wizara Fedha na Mipango, Khamis Mussa Omar alisema ujenzi wa nyumba za mji mpya wa Kwahani ni Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2015-2020 Ibara ya 36 (c) inayoelekeza uanzishaji wa miji mipya  ya kisasa.

Alisema mradi huo unaohusisha majengo matano kwa ajili ya Familia 70, umeendeshwa na Kampuni ya ‘Estim Construction Company Limited’ ya Jijijini Dar es Salaam kwa gharama ya shilingi Bilioni 20, ikiwa ni mkopo wa ZSSF kwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Alisema mradi wa ujenzi wa nyumba hizo ulianza Oktoba 2, 2019, ambapo  ulitarajiwa kukamilika Septemba 30, mwaka huu,  lakini kutokana na athari za Ugonjwa wa Covid-19 ulioikumba dunia, ujenzi huo umefikia asilimia 90 hivi sasa.

Katibu Mkuu huyo alisema mazungumzo yanaendelea kati ya Wizara ya Fedha na Mipango na ile ya Ardhi, Nyumba, Makaazi ili kupata eneo la ardhi litakalojengwa nyumba kama hizo kisiwani Pemba.

Alimpongeza Rais Dk. Shein kwa kuja na wazo la kufanyika kwa ujenzi wa nyumba hizo katika eneo la Kwahani, sambamba na kuzishukuru taasisi zote zilizofanikisha ujenzi huo, ikiwemo Wizara ya Ardhi, ZAWA,ZECO,ZSSF pamoja na Chuo Kikuu cha Ardhi Dar es  Salaam.

Nao, wananchi wa Kwahani  katika Risala yao iliosomwa na Amina Hassan Abas wameipongeza Serikali ya Awamu ya saba, chini ya Uongozi wa Dk. Shein kwa kubadili maisha hao kufuatia hatua ya ujenzi wa nyumba mpya za kisasa.

Katika hafla hiyo ambayo pai ilihuduriwa pia na Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali idd, Rais Dk. alikabidhi funguo kwa wananchi watatu wenye nyumba hizo kwa niaba ya wenzao, akiwemo Ali Hamad Haji, Hamida Mwinyi Mmadi pamoja na Abdi Ameir Ali.

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 

 E-mail: abdya062@gmail.com

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.