Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Ali Mohamed Shein Amewatunuku Kamisheni Maofisa wa Idara Maalum za SMZ Zanzibar.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein akiwatunuku Kamisheni Maofisa wa Vikosi vya Idara Maalum za SMZ,baada ya kumaliza mafunzo yao hafla hiyo imefanyika katika Viwanja vya Kambi ya KMKM Kama Wilaya ya Magharibi "A" Unguja.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo amewatunuku Kamisheni Maofisa wa Idara Maalum za SMZ na kuwapongeza kwa kufanikiwa katika mafunzo hayo.

Dk. Shein aliwatunuku Kamisheni hizo Maofisa hao huko katika viwanja vya Chuo cha KMKM Kama, Wilaya ya Magharibi A, katika Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Mara baada ya kuwasili katika viwanja hivyo vya KMKM Kama, Rais Dk. Shein alipokea salamu za heshima pamoja na kupokea Gwaride kutoka kwa Askari wa vikosi vya Idara ya SMZ.

Baada ya tukio hilo, Rais Dk. Shein ambaye pia ni Kamanda Mkuu wa vikosi vya Idara Maalum za SMZ aliwatunuku Kamisheni Maofisa hao kutoka Idara hiyo na baadae walikula kiapo cha utii.

Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Haji Omar Kheri alitumia fursa hiyo kumkaribisha Rais Dk. Shein katika hafla hiyo pamoja na kumpongeza kwa kuiendeleza na kuilea vyema Idara Maalum za SMZ katika uongozi wake wote.

Waziri Kheri alisema kuwa ndani ya miaka kumi ya uongozi wa Rais Dk. Shein mafanikio makubwa ya kupigiwa mfano yamepatika katika Idara hizo Maalum za SMZ.

Nae Mwenyekiti wa Idara Maalum za SMZ Commodore Hassan Mussa Mzee alisema kuwa Maofisa hao waliohitimu mafunzo hayo hivi leo ni weledi, wachapakazi, jasiri, waaminifu na wazalendo kwa Serikali yao kutokana na mafunzo waliyoyapata.

Aidha, alieleza kuwa Maofisa hao waliotunukiwa Kamisheni wako tayari kusimamia ulinzi, na usalama wa nchi yao sambamba na kuhakikisha hali ya amani na utulivu inaendelea kudumu hapa Zanzibar.

Kwa niaba ya Maofisa hao Commodore Mzee alitoa shukurani kwa Rais Dk. Shein kwa uongozi wake bora na maelekezo yake mazuri kwa Idara Maalum za SMZ.

“Hakuna anaeweza kupinga kwamba katika uongozi wako Rais Dk. Shein Idara Maalum za SMZ zimeweza kupiga hatua kubwa ya maendeleo katika nyanja mbali mbali”, alisema Commodore Mzee.

Mapema Mshauri wa Mafunzo ya Idara Maalum za SMZ Meja Jenerali S.S.Omar alieleza namna ya mafunzo hayo yalivyotekelezwa kwa wahitimu hao wa mafunzo mbali mbali ambayo yameendeshwa huko katika chuo cha KMKM Kama pamoja na mafunzo yaliyoendeshwa katika chuo cha KVZ   Pangatupu.

Meja Jenerali huyo alieleza kuwa mpango wa mafunzo uliotolewa na Wizara hiyo unaelendea vizuri ambao tayari umeshaendesha kozi mbali mbali kwa mafanikio makubwa ambapo pia zipo nyengine zinatarajiwa kuendeshwa hapo baadae.

Katika hafla hiyo viongozi mbali mbali wa Serikali walihudhuria akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambae pia, ni Mgombea wa Urais wa Zanzibar kupitia CCM Hussein Ali Hassan Mwinyi pamoja na viongozi na Makamanda wa vikosi vya ulinzi vya SMZ na SMT na wanafamilia.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.