Muakilishi wa Shirika la la Afya duniani WHO Ghirmay Andemichael wapili kutoka kushoto akitoa maelekezo ya vifaa mbali mbali vilivyotolewa msaada kwa Wizara ya Afya huko Mnazimmoja Zanzibar.
Na Khadija Khamis –Maelezo Zanzibar 23/10/2020
WAZIRI wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed amelitaka Baraza la Wataalam wa Maabara ya Tiba kusimamia maadili ili kuhakikisha huduma zinazotolewa katika maabara au taasisi nyengine zina ubora unaokubalika
Akiyasema hayo katika Uzinduzi wa Baraza la wataalam wa Maabara ya Tiba Zanzibar katika ukumbi wa Wizara ya Afya Mnazimmoja.
Alisema kusimamia maadili kwa wafanyakazi kutasaidia kutekeleza majukumu ya watendaji ili kukidhi kiwango bora cha utekelezaji
Waziri huyo alisema Baraza la Wawakilishi Zanzibar lilipitisha na kuidhinisha sheria nambari 10 ya Wataalam wa Maabara za Tiba Zanzibar mnamo Mei 11, 2020 .
Alifahamisha kuwa chombo hicho kina majukumu ya kutambua wataalamu sahihi wa maabara za Tiba na kusimamia haki zao .
“Wataalamu wawe na kiwango cha ujuzi kutokana na kuwa wanashughulikia maisha ya watu” alisema Waziri Hamad.
Alieleza sambamba na majukumu hayo pia chombo kimepewa uwezo wa kuwajibisha watendaji pale ambapo watakapo kwenda kinyume na sheria iliyopo.
Aidha alisema huduma za maabara ni moja kati ya huduma za uchunguzi wa maradhi mbali mbali unaofanyika Maabara (laboratories) kwa kutumia sampuli za kila aina zinazopatikana kutoka kwa binaadamu ambazo huduma hizo hutolewa katika Hospitali za Serikali na za binafsi.
Waziri Hamad alisema kuwepo kwa sheria ya wataalam wa maabara za tiba Zanzibar itasaidia wataalam hao kusajiliwa hapa Zanzibar baada ya Tanzania bara na pia kudhibiti watu wasiostahiki kupima vipimo vya maabara na kutoa majibu yasio sahihi ambayo huhatarisha matibabu na usalama wa wagonjwa.
Nae Mwenyekiti wa Baraza la Wataalamu wa Maabara za Tiba Zanzibar Dkt Salum Seif Salum alisema jukumu la baraza hilo ni kuhakikisha wanatoa leseni na vyeti na kufuatilia taarifa zozote zinazohusiana na usajili pamoja na kubadilisha cheti na leseni iiliyothibitika kuibiwa au kupotea.
Pia alisema kusimamia viwango vya utendaji wa wataalamu wa Maabara ya Tiba na kuhakikisha umahiri wa Wataalamu wa Baraza za Tiba .
Alieleza kuwa Baraza lina jukumu la kushughulikia malalamiko yaliyowasilishwa dhidi ya Wataalamu wa Mabaraza ya tiba na kumshauri Waziri juu ya mambo yanayohusiana na utoaji huduma .
No comments:
Post a Comment