Habari za Punde

Jamii yaaswa kuwa na utamaduni wa kufanya mazoezi ili kuepusha vichocheo vya maradhi yasiyoambukiza

 Na Khadija Khamis - Maelezo Zanzibar    29/12/2020

 

Meneja wa Kitengo cha Maradhi yasioambukiza kutoka Wizara ya Afya Zanzibar  Omar Ali Abdalla ameitaka jamii kuwa na utamaduni wa kufanya mazoezi ili kuepuka vichocheo vya maradhi yasioambukiza.

 

Akizungumza na Waandishi wa Habari katika Ofisi ya Jumuiya ya Watu wanaoishi na maradhi yasioambukiza Zanzibar iliopo Mpendae alisema janga la maradhi hayo linatokana na vichocheo mbali mbali ikiwemo kukosekana mlo kamili na kutofanya mazoezi .

 

Alifahamisha kuwa iko haja wananchi kufanya mazowezi  angalau kwa dakika 30 kwa siku ili kupunguza uzito jambo ambalo litasaidia kuondosha vichocheo vya maradhi yasioambukiza yakiwemo Shindikizo la Damu, Kisukari na Msongo wa Mawazo.

 

“Kinga ni bora kuliko tiba, ukipata maradhi yasioambukiza si rahisi kupoa bali utapewa ushauri nasaha wa utaratibu wa kuishi.” Alisema Meneja Omar.

 

Aidha alisema imebainika kuwa idadi ya wananchi wengi wa Zanzibar wanashiriki kufanya mazoezi lakini wengi wao hawafikii malengo na wengine hawafanyi kabisa.

 

Hata hivyo amefahamisha kwamba kwa wale wenye matatizo  wakiwemo Wajawazito na watu wanaoishi na maradhi yasioambukiza ni vyema kufuata ushauri wa daktari .

 

Alieleza kuwa si lazima kufanya mazoezi ya kukimbia lakini hata kutembea kwa mwendo wa haraka kunasaidia .

 

 Pia amewataka Wazazi na Walimu wa michezo kuhamasisha wanafunzi kufanya mazoezi ili kuweza  kuwa wachangamfu kimwili na kiakili .

 

Alifafanua kuwa mazoezi husaidia kujenga mwili na  kukua kiakili,sambamba na kuondosha maradhi mbalimbali ikiwemo yasioambukiza na msongo wa mawazo.

 

Akizitaja changamoto zinazojitokeza katika kufanya mazoezi alisema kuwa ni pamoja na ukosefu wa elimu sahihi ya ufanyaji wa mazoezi, hasa kwa watu wenye ulemavu.

 

Hivyo ameiomba Idara ya  Mipango Miji kuendelea kuzilinda sehemu za wazi ili jamii iweze  kuzitumia kwa Mazoezi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.