Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais afanya mazungumzo na Viongozi wa Vyama vya Kisiasa Nchini

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Sueiman Abdulla akizungumza na Viongozi wa Vyama Tisa vya Kisiasa waliwemo wale waliogombea Urais wa Zanzibar hapo Afisini kwake Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar.
Mwenyekiti wa Viongozi hao wa Nd. Hamad Mohad Ibrahim kwa niaba ya wenzake akielezea kuridhika kwao na kasi ya Serikali katika kuwaletea Maendeleo Wananchi wake ndani ya kipindi kifupi baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mikuu.

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Sueiman Abdulla akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo yake na Viongozi hao wa Vyama vya Kisiasa Nchini.

Picha na – OMPR – ZNZ.


Na Othman Khamis, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alisema utayari uliyoonyeshwa na Viongozi wa Vyama vya Kisiasa Nchini wa kuwa tayari kushirikiana na Serikali katika kuwaletea Maendeleo Wananchi wote umeleta faraja kubwa.

Alisema utayari huo unaokwenda sambamba na azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuendelea kutekeleza wajibu wake ndani ya Mfumo wa Maridhiano ya Umoja wa Kitaifa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984 utaongeza kasi ya uwajibikaji kutoka kwa Viongozi wa Serikali na Taasisi za Kisiasa.

Mheshimiwa Hemed Suleiman ameeleza hayo wakati akizungumza na Viongozi wa Vyama Tisa vya Kisiasa Nchini wakiwemo waliogombea nafasi ya Urais wa Zanzibar kwenye Uchaguzi Mkuu uliomalizika waliofika kwa lengo la kuipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kasi yake ya kuimarisha Uchumi na Ustawi wa Jamii.

Alisema mchango na mawazo ya Viongozi wa Vyama vya Kisiasa katika Kujenga Nchi hauna mjadala kwa vile unatoa fursa pana Zaidi ya kuimarisha Umoja na Mshikamano miongoni mwa Jamii kwa vile unatoa nafasi kwa kila Mwananchi kuwa na haki na wajibu wa kutoa mchango wake.

Mheshimiwa Hemed Suleiman aliwathibitishia Viongozi hao wa Kisiasa kwamba Serikali Kuu itaendelea kutoa ushirikiano wakati wowote katika kuona huduma za Kijamii zinawafikia Watu wote na pale inapotokea athari ndani ya utekelezaji huo  isipuuzwe na ni vyema ikaripotiwa panaohusika.

Akizungumzia suala la Amani ya Taifa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema mchango wa Viongozi wa Kisasa ni muhimu katika kusimamia hali ya Amani na Usalama wa Nchi.

“ Kuna kila sababu  kwa Viongozi wa Vyama vya Kisiasa kuendelea kusimamia suala la Amani na Utulivu kutokana na kuwa na sauti na mvuto wa kukubalika na jamii ninayowazunguuka”. Alisisitiza Mheshimiwa Hemed.

Aliwapongeza Viongozi wa Kisiasa wa vyama mbali mbali vilivyokuwemo ndani ya mchakato wa Uchaguzi Mkuu kutokana na umahiri wao uliopelekea vugu vugu la Kisiasa Visiwani Zanzibar kumalizika ndani ya muda mfupi baada ya Uchaguzi Mkuu.

Alifahamisha kwamba kwa vile maisha baada ya uchaguzi Mkuu yanaendelea ni vyema kila Mwananchi akaendelea kutekeleza wajibu wake huku akiwataka wawe na subra katika kipindi hichi ambacho Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr Hussein Ali Mwinyi anaendelea kujiandaa kuchukuwa maamuzi magumu ya kujenga Nchi.

Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alibainisha kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamua kudhibiti mapato yake ya ndani kwa lengo la kukidhi mahitaji ya kuwahudumia Wananchi wake.

Mapema Viongozi hao walisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanya jambo kubwa la kuridhia kuendelea kutumia mfuko wa Umoja wa Kitaifa utakaosaidia Wazanzibar kuendeleza Utamaduni wao wa kuishi katika misingi ya Ushirikiano na mshikamano unaoharakisha kasi ya Maendeleo.

Walisema ule uhasama unaotokea kabla na baada ya Uchaguzi umefifia katika kipindi kifupi kutokana na muono mkubwa  wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane kuifanyia utafiti hitilafu hiyo na badaae kuamua kuipatia suluhu mapema.

Viongozi hao wa Vyama vya Siasa Tisa Nchini wamemthibitishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba tayari wameona mabadiliko ya haraka ya kauli za Viongozi wa Serikali jinsi yanavyotekelezwa na Watendaji pamoja na Wananchi Mitaani na sehemu za Kazi wakitolea mfano suala la kuendeleza usafi wa Mazingira Mitaani.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.