RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Mhe Dk. Hussein Ali Mwinyi akitembelea Soko la Kimataifa la Dagaa
Kasenda akiwa katika ziara yake Mkoani Geita Wilaya ya Chato na (kushoto kwa
Rais) Waziri wa Uvuvi na Mifugo Mhe. Mashimba Ndaki na Makamu wa Kwanza wa Rais
wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa ziara yake ya kulitembelea soko
la samaki la Kimataifa la Kasenda Wilayani Chato, amejifunza mambo mengi ambayo
wananchi wa Zanzibar wanaweza kuanzishiwa ili na wao wakaweza kuuza bidhaa zao
za uvuvi na kupata tija.
Rais Dk. Hussein Mwinyi ameyasema hayo leo
wakati akiwasalimia wananchi na viongozi wa Kitongoji cha Kasenda na
vijiji vya jirani Wilayani Chato, Mkoa wa Geita mara baada ya kulitembelea soko
lao la samaki la Kimataifa la Kasenda ambapo aliungana pamoja na Makamo wa
Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad.
Katika maelezo yake, Rais Dk. Mwinyi alisema
kuwa amefurahishwa na hatua hiyo kwa kuanzisha soko la Kimataifa kama hilo hasa
ikizingatiwa kwamba hata kwa upande wa Zanzibar wapo wafanyabiashara kama hao
wa dagaa wanaouza bidhaa hiyo huko Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Zanzibar
imeanza Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambapo vyama vimeungana na kuunda Serikali
kwa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho ndio chama chake na Chama
cha ACT Wazalendo chama cha Maalim Seif Sharif Hamad.
Aliongeza kwamba wananchi wa Zanzibar wamo
katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa na hivi sasa tofauti za kisiasa
zimeondolewa kwani wameona umuhimu wa kuunganisha watu na hivi sasa Wazanzibari
wote wamekuwa wamoja na wako tayari kuchapa kazi ili wajiletee maendeleo.
Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kumshukuru
Rais Magufuli kwa kusimamia na kuhakikisha hilo limewezekana kwa upande wa
Zanzibar kwani yeye kama Mwenyekiti wa (CCM) alikuwa tayari kushirikiana naye
katika kuhakikisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa inaundwa na kuweza kuunga mkono
juhudi hizo.
Alifahamisha kuwa baada ya kukamilisha Serikali,
Zanzibar imekuja na Sera ya uchumi wa buluu ambapo hivi sasa uchumi utajikita na
mambo yanayohusiana na bahari ambapo moja katika kazi hizo ni uvuvi, ufugaji wa
samaki, utalii pamoja na utafutaji wa mafuta na gesi asilia.
Alisema kwamba Sera hiyo mpya italeta maendeleo
makubwa hasa ikizingatiwa kwamba hivi sasa wananchi wa Zanzibar wameona
haja ya kuachana na malumbano ya kisiasa.
Rais Dk. Mwinyi aliwatakia kila la heri wananchi
wa Chato katika kufanikisha uendelezaji wa soko lao hilo kwa miundombinu mipya
inayotarajiwa kuwekwa huku akisisitiza kwamba Watanzania wote ni ndugu
hivyo aliwakaribisha wananchi wa Mkoa wa Geita kuja Zanzibar huku akisisitiza
kwamba juhudi za kuimarisha biashara zitaendelezwa ili kuwasaidia wananchi
kujikwamua kimaisha.
Katika ziara hiyo ya kulitembelea soko hilo la
Kimataifa la Kasenda Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi alishiriki
ambapo pia, Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad alipata
fursa ya kuwasalimia wananachi.
Mapema, Waziri wa Mifugo na Uvuvi wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mashimba Ndaki alisema kuwa sekta ya uvuvi kwa Tanzania
Bara ni moja wapo ya sekta zinazochangia katika kukuza uchumi na kupunguza
uamasikini.
Alisema kuwa uzalishaji wa samaki katika Mkoa wa
Geita umekuwa ukiongezeka kila mwaka ambapokatika wmaka 2015 kiasi cha tani
18,535.05 za samaki zikiwa na thamani ya TZS Bilioni 76.9 zilivunwa
ikilinganishwa na tani 21,188.03 zilizovunwa mwaka 2019 zikiwa na thamani ya
TZS Bilioni 102.7.
Aliongeza kuwa katika mwaka 2020 jumla ya mazao
ya uvuvi tani 5,755 yenye thamani ya TZS Bilioni 7.3 yalisafirishwa nje ya
nchi.
Alisema kuwa soko la Kasenda lina ukubwa wa mita
za mraba 11,322 na lilianzishwa mwaka 1995 ambalo ni la pili kwa ukubwa kati ya
masoko yote ya samaki yaliopo Ukanda wa Ziwa Victoria ambapo pia, soko hilo
lilipandishwa hadhi mnamo mwaka 2017.
Sambamba na hayo, Waziri Ndaki alisema kuwa
biashara ya samaki katika soko hilo inahusisha masoko ya ndani ya nchi na yale
ya nje ya nchi katika nchi za Rwanda, Uganda, Burundi, Congo DRC, Zambia na
Malawi.
Alisema kuwa mazao makuu yanayosafirishwa kwenda
nje ya nchi kupitia soko hilo ni dagaa wa ziwa Victoria, furu na sangara
waliokaushwa kwa chumvi (kayabo) ambapo biashara kati ya nchi hizo inachangia
kuiingizia Serikali mapato kupitia mrahaba wa mauzo ya samaki nje ya nchi.
Aliongeza kuwa soko hilo linanufaisha watu
wapatao 12,528 ambao hufanya shughuli zao katika maeneo yanayozunguka Wilaya ya
Chato Ukanda wa Ziwa Victoria wakiwemo wafanyabiashara. Huku akieleza mikakati
ya kuliboresha soko hilo.
Mapema Waziri wa Nishati Medard Kalimani ambaye
pia ni Mbunge wa Chato alimueleza Rais Dk. Mwinyi pamoja na Makamo wa Rais wa
Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad hatua zinazochukuliwa katika kuimarisha
biashara hiyo ya samaki Wilayani humo.
Waziri Kalimani alisema kuwa siku hii ni ya
kihistoria ambapo italipa hadhi zaidi soko hilo la Kimataifa kutokana na
kutembelewa na viongozi hao kutoka Zanzibar huku akimpongeza Rais Magufuli kwa
kuendelea kulipa hadhi soko lao hilo.
Aidha, Waziri huyo alieleza matumaini yake
kwamba ziara hiyo itazaa mahusiano na mashirikiano ya kibiashara kati ya
wafanyabiashara wa soko hilo na wale wa Zanzibar pamoja na wananchi wa Zanzibar
kuweza kutumia samaki hao kutoka soko hilo.
Mapema Rais Dk. Mwinyi pamoja na Makamo wa
Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad walipata maelezo kutoka kwa
Mwenyekiti wa soko hilo Suleiman Mohammed Said na kumueleza kwamba soko hilo ni
la pili katika ukanda huo baada lile la Kirumba Mwanza.
Mwenyekiti huyo alieleza jinsi ya shughuli za
soko hilo zinavyokwenda na kueleza maeneo wanayouza samaki wao ndani na nje ya
Tanzania huku wakieleza furaha zao kwa kufikiwa na ugeni huo kutoka Zanzibar.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
No comments:
Post a Comment