Habari za Punde

Kuapishwa kwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan Ikulu Jijini Dar es Salaam.

 

JAJI Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof Ibrahim Hamis Juma akimuapisha Mhe Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Dar es Salaam leo 19-3-2021

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan leo ameapishwa kuliongoza Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar-es-Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Tukio hilo limefanyika baada ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dk. John Pombe Magufuli kilichotokea Machi 7, 2021 jijini Dar es Salaam.

Akiwahutubia wananchi mara baada ya kula kiapo hicho, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliwasihi Watanzania kuwa na moyo wa subira , kujenga umoja na mshikamano katika kipindi hichi kigumu cha msiba.

Rais Samia aliwahakikishia wananchi kuwa viongozi wako imara kama Taifa na wamejipanga vizuri kuhakikisha kuwa wanaendelea pale alipoishia Hayati Rais Dk. John Pombe Magufuli.

“Nikiri kuwa si jambo ambalo nilikuwa nimejiandaa nalo wala kulitizamia , ni jambo ambalo hatujawahi hata kuwa na uzoefu wala rejea nalo katika historia ya nchi yetu”, alisema Rais Samia Suluhu Hassan.

Aidha, Rais Samia amewataka Watanzania kusimama pamoja na kushikamana katika kipindi hiki cha maombolezo na kusisitiza kwamba huu ni wakati wa kuzika tofauti zao na kuwa wamoja kama Taifa.

Alisema kuwa huu ni wakati wa kufarijiana, kuoneshana upendo, udugu, kudumisha amani, kuenzi utu wao na utamaduni wao na kueleza kwamba huu si wakati wa kutizama mbele kwa mashaka bali ni kwa matumaini na kujiamini.

Alisisitiza kwamba huu si wakati wa kutizama yaliyopita bali ni kutizama yajayo na wala si wakati wa kunyosheana vidole, bali ni wakati wa kushikana mikono na kusonga mbele.

“Huu ni wakati wa kufutana machozi na kufarijiana ili tuweke nguvu zetu pamoja na kujenga Tanzania mpya ambayo mpendwa wetu Rais Magufuli alitamani”,alisema Rais Samia.

Sambamba ha yao, Rais Samia alieleza kwamba kiapo alichokula ni tofauti na viapo vyote alivyowahi kula kaytika maisha yake na tofauti na viapo vya awali ambavyo alivila kwa faraja, nderemo, vifijo na bashasha tele.

Aliongeza kuwa leo (Machi 19/2021) amekula kiapo cha juu kabisa katika nchi yake ya Tanzania akiwa na majonzi tele na nchi ikiwa imetandwa na wingu jeusi la simanzi kubwa.

“Nimekula kiapo katika siku ya maombolezo mtaniwia radhi kuwa nitaongea kwa uchache na kwa ufupi, tutatafuta wasaa hapo baadae tusemezane, tukumbushane na tuwekane sawa juu ya mambo mengi yanayohusu Taifa letu, mustakbali wake na matarajio yetu ya siku za usoni”alisema Rais Samia.

Aidha, aliwashukuru viongozi wa mihimili muhimu ya Bunge na Mahakama kwa mashirikiano waliomuonesha katika kipindi hiki na kumshukuru Rais Dk. Mwinyi na mihimili yake kwa kuwa nae bega kwa bega katika kipindi hichi cha msiba pamoja na kuwashukuru viongozi wote wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama.

Alitumia fursa hiyo kwa mara nyengine tena kutoa salamu za rambirambi kwa Mama Janeth Magufuli, Mjane wa Hayati Rais John Maguuli, Mama Susan Magufuli, watoto na familia, ndugu, jamaa na marafiki kwa kuondokewa na kipenzi chao na mhimili muhimu wa familia.

Rais Samia pia, alieleza ratiba ya mazishi ya Hayati Rais John Pombe Joseph Magufuli pamoja na tarehe za kuagwa mwili wa Hayati Magufuli ambapo pia,Rais Samia alieleza kwamba tarehe 22 na tarehe 25 ambayo ni siku ya mazishi tarehe hizo zitakuwa ni siku za mapumziko.

Mapema Rais Samia mara baada ya kula kiapo alipata heshima zote za Kitaifa kwa kupokea salamu za heshima za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) pamoja na kupigiwa mizinga 21.

Wakati huo huo, Rais Samia aliendesha kikao cha Baraza la Mawaziri akiwa Mwenyekiti wa Baraza hilo huko Ikulu Jijini Dar es Salaam. 

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.