Habari za Punde

WAZIRI NDAKI ATAKA KUPUUZWA KWA UZUSHI WA WINGI WA MAYAI KUTOKA NJE YA NCHI

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki amewataka watanzania kuupuuza uzushi uliojitokeza kutokana na kusambazwa kwa ujumbe wenye taarifa za kupotosha kuhusu kuingizwa kwa mayai nchini kutokea nchi jirani na kusababisha soko la mayai yanayozalishwa nchini kushuka bei.


Akizungumza leo (17.06.2021) ofisini kwake katika Mji wa Serikali Jijini Dodoma, Waziri Ndaki alisema baada ya kuona ujumbe huo Juni 15 Mwaka huu,  Wizara ya Mifugo na Uvuvi ilifanya uchunguzi kwenye makao makuu ya mikoa yote 26 nchini na baadhi ya wilaya ili kujiridhisha juu ya upatikanaji wa mayai, bei ya trei ya mayai na soko lake kwa ujumla.

Hatua hiyo inatokana na uwepo wa ujumbe unaozunguka kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kuingia kwa mayai mengi nchini kutoka nje ya nchi kiasi cha kusababisha kushuka kwa bei ya mayai mpaka kufikia Shilingi 4,000/= kwa trei.

Ujumbe huo ulikuwa na kichwa cha habari kinachosomeka “SOKO LA MAYAI DSM KITENDAWILI”.

Alisema njia zilizotumika kukusanya taarifa ni pamoja na kuongea na wafugaji wakubwa wa kuku wa mayai, wafanyabishara wakubwa na wadogo wa mayai.

Alisema pia walilazimika kufika sehemu za masoko wanakouza mayai na kujionea hali halisi ikiwa ni pamoja na kujua bei ya trei la mayai, upatikanaji wake na hali ya soko kwa ujumla.

Waziri huyo alisema pia walitumia fursa ya kuongea na maafisa mifugo wa mikoa, majiji, manispaa na halmashauri ili kupata taarifa juu ya bei ya trei la mayai, upatikanaji wake na hali ya soko la mayai kwenye maeneo yao ya kiutawala.

Akizungumzia matokeo ya uchunguzi huo, Waziri Ndaki alisema mayai yanayozalishwa nchini ni kidogo kiasi kwa sababu ya uhaba wa vifaranga wa kuku wa mayai na tatizo la uhaba wa vifaranga limekuwepo tangu mwaka 2020 kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa COVID 19 duniani uliosababisha uingizaji nchini wa vifaranga wa kuku wazazi kupungua sana.

Alisema hali hiyo imesababisha idadi ya kuku wa mayai wanaotaga kwa sasa kuwa wachache na kusababisha kuwepo na uhaba wa mayai nchini huku matokeo zaidi ya uchunguzi yanaonesha kwamba bei ya trei la mayai katika ngazi ya mfugaji ni kati ya Shilingi 6,500/= mpaka 9,000/=.

“Vilevile bei ya trei la mayai sokoni ni Shilingi 6,800/= katika baadhi ya mikoa mpaka Shilingi 12,000/= kwa mikoa ukiwemo wa Katavi lakini bei ya yai moja sokoni au madukani ni kati ya Shilingi 250/= mpaka 500/=” Alisema

Alisema mtu aliyezusha taarifa hizi za uongo ana nia ovu na tasnia ya ufugaji kuku Tanzania na ameleta taharuki kubwa kwa wafugaji wa kuku na jamii yote ya Tanzania, suala la uhaba wa vifaranga linafanyiwa kazi na kufikia mwezi wa Septemba, 2021 hali itakuwa imesharudi kama kawaida.

“Wizara inakanusha vikali taarifa zinazonguka kwenye mitandao ya kijamii kuwa hakuna wingi wa mayai uliosababisha kushuka kwa bei ya mayai katika ngazi ya mfugaji na sokoni kinachoonekana zaidi ni kuwa kuna upungufu mkubwa wa mayai nchini uliosababisha bei kupanda mpaka kufikia Shilingi 12,000/= kwa teri” Alisema Waziri huyo.

Alisema taarifa zilizosambazwa ni uzushi mtupu na hazina ukweli wowote kutokana na kwamba serikali ilishazuia uingizwaji wa kuku na mazao yake kutokana na uwepo wa tishio la ugonjwa wa mafua makali ya ndege Duniani.

Aidha, Wizara imekuwa ikitoa vibali maalum vya kuingiza vifaranga na mayai ya kutotolesha ya kuku wazazi na kumekuwa na matukio machache ya uingizaji wa mayai nchini kwa njia za panya lakini wizara imekuwa ikidhibiti hali hiyo.

Hata hivyo alisema mwezi Aprili mwaka huu chama cha wafugaji wa kuku kiliomba makampuni ya kuku yaruhusiwe kuingiza vifaranga wa kuku wa nyama, vifaranga wa kuku wa mayai na mayai ya kutotolesha kutokana na uhaba mkubwa wa vifaranga nchini na serikali imeruhusu kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Juni mpaka Agosti 2021 na Tayari makampuni kadhaa yameshaanza kuingiza nchini vifaranga na mayai ya kutotolesha na hivi karibuni tatizo hili litafikia ukomo.

Katika hatua nyingine waziri huyo, akizungumzia hali ya ugonjwa wa homa ya nguruwe na jitihada zinazochukuliwa kukabiliana na tatizo hilo alisema wizara ilitoa taarifa kwa umma kupitia vyombo vya habari juu ya kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa wa homa ya nguruwe (African Swine Fever) katika maeneo ya mikoa ya Mwanza, Kagera, Shinyanga na Dodoma.

Alisema katika taarifa yake aliwaagiza wakuu wa Mikoa, wakuu wa Wilaya na wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kusimamia kikamilifu utekelezaji wa masharti ya karantini zilizokuwa zimewekwa na wataalamu wa mifugo hasa kwa vile ugonjwa huo hauna chanjo wala tiba na walisimamia vyema zoezi hilo.

Aidha alisema wizara imekuwa ikifanya juhudi kubwa kudhibiti ugonjwa huu na mpaka kufikia mwishoni mwa Mwezi Aprili, 2021 sehemu nyingi za nchi hakukuwa na matukio ya ugonjwa huo.

“Mnamo tarehe 01/06/2021 katika Manispaa ya Morogoro kulijitokeza matukio ya nguruwe 14 kufa na uchunguzi wa kimaabara ulionesha ugonjwa wa homa ya nguruwe “Alisema

Alieleza kwamba tayari juhudi kubwa za kuudhibiti zinaendelea ambazo ni pamoja na kuweka zuio (karantini) ya kuingiza na kutoa nguruwe na mazao yake katika Manispaa ya Morogoro tangu tarehe 03/06/2021 na elimu kwa wafugaji na wadau wengine wa nguruwe njia za kukinga ugonjwa usiingie kwenye mabanda ya nguruwe.

Alieleza kwamba mpaka kufikia tarehe 17/06/2021 hali ya ugonjwa katika Manispaa ya Morogoro ulikuwa umedhibitiwa na hakuna kifo tena kilichotokea kwa nguruwe.

Hata hivyo alisema Juni 9 mwaka huu wizara ilipata taarifa juu ya uwepo wa ugonjwa wa homa ya nguruwe katika Jiji la Dar es Salaam.

Alisema baada ya kufanya uchunguzi katika mashamba ya nguruwe, ilibainika kuwepo kwa taarifa za nguruwe 298 kufa katika mashamba mawili kwa kile kilichodhaniwa ni ugonjwa wa homa ya nguruwe.

Alieleza baada ya kuchunguza kwa kina kwa wanyama waliokuwa wamebaki kwenye mashamba hayo pamoja na kuchukua sampuli na kuzipima katika maabara, ilibainika kuwa ilikuwa sio ugonjwa wa homa ya nguruwe.

Aliongeza kwamba ufuatiliaji zaidi ulifanyika kwenye sehemu zote za machinjio ya nguruwe Dar es Salaam na kuchunguza nguruwe wanaochinjwa, hapakuwa na viashiria vyovyote vya ugonjwa wa homa ya nguruwe.

Wizara kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo inaendelea na juhudi za kudhibiti kabisa ugonjwa huu nchini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.