Habari za Punde

Wiki ya Kilele cha Maadhimisho ya Kupinga Matumizi ya Dawa za Kulevya

Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti Dawa za Kulevya Zanzibar Luteni Kanal Burhani Zuberi Nassor, akizungumza na Waandishi wa habari wa vombombalimbali vilioko zanzibar kuhusiana na matayarisho ya Siku ya Maadhimisho ya Kupinga Matumizi ya Dawa za Kulevya. 

 

Na.Raya Hamad – OMKR  22/06/2020

Wazanzibari wasipokuwa wazalendo wa kupinga matumizi ya Dawa za Kulevya na kuyadhibiti yasiingie nchini baada ya miaka 20 kila nyumba itakuwa na mteja anaetumia Dawa za Kulevya na Taifa litateketea

Vijana wanaotegemewa ndio waathirika wakubwa wa matumizi ya dawa za kulevya hali hii isipodhibitiwa na kushirikiana pamoja Taifa litateketea

Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti Dawa za Kulevya Zanzibar Luteni Kanal Burhani Zuberi Nassor ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika wiki ya kilele cha maadhimisho ya kupinga matumizi ya Dawa za Kulevya

Luteni Kanal Burhani amesema katika kukabiliana na janga hili hatua madhubuti zinachukuliwa na Tume ili kuhakikisha wanawadhibiti waingizaji, wauzaji na wasambazaji pamoja na watumiaji wa dawa za kulevya nchini

Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya imejipanga vyema na wanahakikisha wale wote wanaojihusisha na Dawa  za kulevya wanapelekwa kwenye vyombo vya sheria

Luteni Kanal Burhani amewahakikishia wananchi kuwa mikakati mipya imeandaliwa na sheria inafanyiwa marekebisho ili kuweza kuchunguza, kupeleleza, kukamata na kupeleka mahakamani.

‘Tunahakikisha tunatoka hapa tulipo na kubadilisha Sheria pamoja na Muundo badala ya Tume iliyopo inabadilika na kuwa Mamlaka kamili ili kuweza kuzisimamia vyema sheria kwani Zanzibar bila ya dawa za kulevya inawezekana iwapo sote tutashirikiana’

Pia amesisitiza kuwa na dhamira thabiti ya kuchukia na kuondoa dawa za kulevya jambo ambalo litalipelekea Taifa hili kufika mbali kiuchumi hivyo ni wajibu wa kila mmoja kusimamia sheria kuanzia viongozi, wananchi,shehia, Halmashauri, vyombo vya ulizi na usalama, Wilaya na Mkoa kwa kutii sheria bila shuruti

Ameeleza kuwa wahalifu wanaishi ndani ya shehia zetu hivyo lazima kuwepo na mashirikiano na jamii ili kuwaibuwa wanaoliangamiza Taifa hili kwa kuondoa muhali na kutoa taarifa za uhalifu wa dawa za kulevya.

‘Tukithubutu kushirikiana na kubadilisha mifumo ya maisha ambayo tunaishi ya usasa ni wazi suala la matumizi ya madawa ya kulevya hapa kwetu litakuwa ni historia, wazazi na walezi pia tuwewadadisi watoto wetu na kufatilia mwenendo wao, mtoto anakuja na vespa au pikipiki mzazi huulizi anarudi usiku huulizi anavitoa wapi vitu vya thamani hizi ni dalili mbaya na turudi kwenye malezi ya asili’ alisisitiza

Akitoa takwimu Mkurugenzi Uchunguzi na Udhibiti Ndugu Juma A. Zidikheri kupitia ripoti ya kitengo cha Polisi cha Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kipindi cha miaka 9 iliyopita 2012-2020 jumla ya watuhumiwa 3,810 wakiwemo wanaume 3,577 na wanawake 233 wamekamatwa nchini wakijihusisha na Dawa za Kulevya

Aidha katika kipindi hicho jumla ya kilo 51.5 za heroini, kilo 2,946 za bangi, kilo 5.4 za Valium na kilo 19.71 za kokeni zilizokamatwa

Mkutano na waandishi wa habari umefanyika kwenye ukumbi wa mkutano Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais pia umehudhuriwa na wakurugenzi kutoka ofisi hio akiwemo Mkurugenzi Mipango, Sera na Utafiti Bi Daima M. Mkalimoto na Mkurugenzi Uendeshaji na Utumishi Ndugu.Juma Ali Simai

Mkutano wa Kilele cha Maadhimisho ya wiki ya kupinga Matumizi ya Dawa za Kulevya utafanyika siku ya Jumamosi tarehe 26/06/2021 katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni na mgeni rasmini Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe Dk. Hussein Ali Mwinyi

Ujumbe wa Mwaka huu ni ‘Sema Ukweli juu ya athari za Dawa za Kulevya Okoa Maisha’

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.