Habari za Punde

DKT GWAJIMA AZINDUA BARAZA LA TAIFA LA MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI (NACONGO)

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt.Dorothy Gwajima akizungumza na viongozi wa Baraza la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NACONGO) wakati wa uzinduzi wa Baraza hilo jijini Dodoma.

Na Mwandishi Wetu Dodoma.                                                                                 

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amezindua Baraza jipya la Mashirika Yasiyo ya kiserikali linalojumisha wajumbe kutoka mikoa 26 ya Tanzania Bara na wawakilishi wa makundi mbalimbali. 

 

Dkt.Gwajima amezindua Baraza hilo leo Juni10, 2021 jijini Dodoma mara baada ya kukamilika kwa uchaguzi wa viongozi wa Baraza uliosimamiwa na Kamati ya mpito iliyoteuliwa na Waziri huyo June 07 2021.

 

Waziri Dkt. Gwajima amesema kuwa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ni chombo cha uwakilishi na kiungo muhimu kati ya Mashirika na Serikali, hivyo uwepo wa Baraza hili utasaidia utekelezaji wa majukumu kwa mujibu wa Sheria.

 

“Niliamua kutekeleza Sheria kwa kuteua Kamati ya Mpito ya uchaguzi wa Baraza hili kwa sababu mimi kama msimamizi wa Sheria na Kanuni za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nisingeweza kuvumilia vitendo vya ukiukwaji wa Sheria na Kanuni hizo” alisema Waziri Dkt. Gwajima.

 

Pia Waziri Dkt. Gwajima ametoa wito kwa viongozi wa wajumbe wote wa Baraza kufanya kazi kwa weledi, uadilifu, na uzalendo wa hali ya juu kwa sekta ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na Taifa kwa ujumla ili kuhakikisha Sekta hiyo inafanya kazi kwa kuzingatia Sheria na Kanuni zilizopo.

 

“Uchaguzi umeshaisha sasa nendeni mkafanye kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo ilioyopo ili kukidhi matarajio ya waliochagua na jamii ya Watanzania kwa ujumla” alisema Waziri Dkt. Gwajima

 

Aidha, Dkt .Gwajima ameliahidi Baraza hilo kutekeleza mapendekezo yao na kuwataka wajitoe kwa hali na mali kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha yale yaliyopendekezwa yanafanyiwa kazi kwa kasi na weledi.

 

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto,Idara kuu ya Maendeleo ya jamii Dkt.John Jingu  amesema matarajio ya Wizara ni kuhakikisha NaCoNGO inafanya kazi kwa waledi na kusaidiana na Serikali katika kutatua changamoto za watanzania katika maendeleo .

 

Kwa upande wake Mwenyekiti mpya wa Baraza la Mashirika yasiyo ya kiserikali Dkt. Lilian Badi amesema uongozi mpya utahakikisha panakuwa na uwajibikaji, na kuzingatia maadili katika utekelezaji wa majukumu wa Baraza hilo na kujenga mahusiano na taasisi zingine pamoja na kuzingatia Sheria zilizowekwa.

 

Akitoa maelezo ya uchaguzi Mwenyekiti wa Kamati ya mpito ya uchaguzi wa Baraza la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Wakili Flaviana Charles amesema mchakato wa uchaguzi ulifanywa kwa kuzingatia kanuni na demokrasia na imewezesha kupata viongozi kuanzia ngazi ya Wilaya hadi taifa.

 

Aidha ameainisha mapendekezo kwa Baraza jipya kuwa ni pamoja na kuweka ratiba mapema ya chaguzi zijazo, uwiano wa uwakilishi, kuwa na data base, kuwajengea uwezo zaidi watumishi wa NaCoNGO na kupitia kanuni zilizopitwa na wakati  pamoja na kuwepo bajeti toshelezi ili kuweza kuendesha Baraza hilo kwa ufanisi

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.