RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la MapinduziDk.
Hussein Ali Mwinyi ametoa pongezi kwa Watendaji wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar
pamoja na Wadau wote wa Uchaguzi kwa kufanikisha vyema Uchaguzi Mkuu uliopita wa
Oktoba 28, mwaka 2020.
Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar mara baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Jaji Mstaafu Hamid Mahmoud Hamid kumkabidhi Rais Ripoti ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 uliofanyika tarehe 28 Oktoba, 2020 kwa kumchagua Rais wa Zanzibar, kuwachagua Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi pamoja na Madiwani na kuvihusisha vyama 19 vya siasa.
Katika pongezi hizo, Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba kuna kila sababu ya kutoa pongezi kwa wadau wote wa Uchaguzi wakiwemo Tume husika, Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Asasi za Kiraia pamoja na wananchi wote kwa Ujumla kutoka na kwenda vyema kwa zoezi la uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, 2020.
“Nachukua fursa hii ya pekee kutoa shukurani zangu za dhati kwa Tume ya Uchaguzi na Wadau wote wa Uchaguzi kutokana na zoezi la Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28,2020 kwenda vyema”,alisema Dk. Mwinyi.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itahakikisha inafanya kila liwezekanalo ili kuepuka changamoto zisije kutokea tena katika chaguzi zijazo kwani lengo la Serikali ni kuzifanyia kazi changamoto zilizopo.
Alisisitiza kwamba mafanikio makubwa yameweza kupatikana katika zoezi hilo kutokana na Tume hiyo kwenda na wakati kwa kutumia mfumo mpya wa uandikishaji wa kisasa wa TEHAMA.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alitoa pongezi zake kwa Tume hiyo kwa kufanikisha kuchapisha kura zilizotumika katika Uchaguzi Mkuu hapa hapa Zanzibar na sanjari na kukamilisha kuhesabu kura na kutangaza matokeo ya Uchaguzi ndani ya masaa 24 baada ya zoezi la upigaji kura kukamilika.
Rais Dk. Mwinyi alitoa pongezi kwa Tume hiyo ya Uchaguzi kwa kazi kuwa iliyofanya ikiwa ni pamoja na kukabidhisha ripoti hiyo huku akisisitiza kwamba juhudi za makusudi zitachukuliwa na Serikali katika kuhakikisha kwamba changuzi zijazo zinakuwa bora zaidi.
Mapema Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Jaji Mstaafu Hamid Mahmoud Hamid kabla ya kumkabidhi Rais Dk. Mwinyi Ripoti hiyo, alimueleza kwamba Ripoti hiyo imegawanyika katika Sura Saba na imezingatia hatua za mzunguko mzima wa Uchaguzi hivyo imezingatia hali ilivyokuwa kabla ya Uchaguzi, wakati wa Uchaguzi na baada ya Uchaguzi.
Mwenyekiti hiuyo wa Tume ya Uchaguzi alitoa shukurani za dhati kwa Serikali ya Mapainduzi ya Zanzibar kwa kuweza kugharamia Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa mwaka 2020 kwa kiwango cha asilimia mia moja ya gharama zote za uchaguzi na fedha zote hizo kupatikana kwa wakati muwafaka.
Alisema kuwa hatua hiyo ya Serikali ndiyo iliyowezesha Tume hiyo ya Uchaguzi kuendesha na kusimamia Uchaguzi huo kwa ufanisi mkubwa zaidi.
Aidha, Mwenyekiti huyo alitoa shukurani kwa viongozi na watu wote waliojitokeza kuwania nafasi mbali mbali za uongozi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, jambo lililopelekea uchaguzi huo kuonekana kuwa huru na wa haki.
Jaji Hamid pia, alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba uchaguzi huo Mkuu wa 2020 ulifanyika kama ulivyopangwa bila ya kutokezea hitilafu yeyote iliyosababisha kurejewa au kufunguliwa mashtaka ya kupinga matokeo.
Alisema kuwa kura ya mapema iliweza kufanyika kwa mara ya kwanza na iliwarahisishia walengwa waliotajwa katika sharia ya Uchaguzi kufanya kazi siku ya Uchaguzi wa pamoja kwa ufanisi zaidi.
Alifahamisha kwamba Tume imeweza kuwapata wataalamu wazawa waliofanikiwa kutengeneza mfumo mpya wa uandikishaji wa kisasa wa TEHAMA pamoja na kutayarisha mifumo myengine ya Uchaguzi iliyoiwezesha Tume kutekeleza zoezi la Uchaguzi kwa usiri na kwa ufanisi bila ya kuingiliwa.
Pia, Mwenyekiti huyo wa Tume alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba Tume imeweza kuchapisha kura zilizotumika katika Uchaguzi Mkuu hapa hapa Zanzibar na kwa mara ya kwanza katika historia ya Zanzibar Tume imeweza kukamilisha kuhesabu kura na kutangaza matokeo ya Uchaguzi ndani ya masaa 24 baada ya zoezi la upigaji kura kukamilika.
Mwenyekiti huyo wa Tume ya Uchaguzi ambaye alifuatana na Wajumbe wake pia, alitumia fursa hiyo kumueleza Rais Dk. Mwinyi baadhi ya changamoto ambazo Tume ilizikabili katika zoezi zima la Uchaguzi huo wa Oktoba 28, 2020.
Kutokana na maelezo ya Mwenyekiti huyo wa Tume kwa mujibu wa kifungu cha 27 cha sheria ya kuanzisha Ofisi ya Tume ya Uchaguzi namba 1 ya mwaka 2017, kila unapomalizika Uchaguzi Mkuu, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar inatakiwa kutayarisha Ripoti na kuiwasilisha kwa Rais ndani ya miezi 12.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk.
No comments:
Post a Comment