Habari za Punde

Tanzania Yaendelea Kufanya Vizuri Afrika Mashariki Udhibiti Mfumuko wa Bei

 

Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii Ruth Minja akieleza jinsi Tanzania inavyoendelea kudhibiti mfumuko wa bei ili kukuza uchumi na ustawi wa wananchi leo Julai 8, 2021 Jijini Dodoma wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu mfumuko wa bei wa mwezi June, 2021.

Na Mwandishi wetu- Dodoma.                                                                                                                    

Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika kudhibiti mfumuko wa bei wa Taifa ikilinganishwa na  nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kipindi cha mwezi June , 2021.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii, Ruth Minja leo Julai 8, 2021 Jijini Dodoma ambapo amesema mfumuko huo kwa  hapa nchini  kwa mwezi Juni umefikia asilimia 3.6 kutoka asilimia 3.3 mwezi Mei, Kenya 6.32 kutoka 5.87 ya mwezi Mei, 2021 na Uganda 2.0 kutoka 1.9 mwezi Mei,  2021 .

“Ongezeko dogo la Mfumuko wa Bei hapa nchini kwa mwaka unaoishia Mwezi Juni, 2021 unamaanisha kuwa, kasi ya mabadiliko ya bei na huduma kwa mwaka unaoishia mwezi Juni, 2021 imeongezeka kidogo ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo mwaka ulioishia mwezi Mei, 2021 na  kwa nchi za Afrika Mashariki Tanzania  bado inafanya vizuri”, alisisitiza Minja

Akifafanua amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuchukua hatua za kudhibi mfumuko wa bei ili kuwawezesha wananchi kuendelea  kuchangia  katika kukuza uchumi na shughuli nyingine za maendeleo.

Baadhi ya bidhaa zilizoongezeka bei kwa mwezi June ni; vitambaa vya nguo kwa asilimia 8.5, nguo za wanawake kwa asilimia6.3, viatu vya wanawake kwa asilimia 6.3, viatu vya wanaume kwa asilimia 6.2, kodi ya  pango asilimia 4.9, vyakula kwenye migahawa asilimia 5.6 na gharama za malazi kwenye nyumba za kulala wageni kwa asilimia 5.7

Kwa upande wa bei za vyakula na vinywaji Baridi kwa mwaka ulioishia mwezi June, 2021 umepungua hadi asilimia 4.7 kutoka asilimia 4.9 kwa mwaka unaoishia mwezi Mei , 2021.

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ni Taasisi ya Serikali iliyoanzishwa kwa sheria ya Takwimu Sura 351 na yenye mamlaka ya kutoa, kusimamia na kuratibu upatikanaji na usambazaji wa Takwimu rasmi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.