Habari za Punde

Dkt.Saada Mkuya Amezindua Kongamano la Kupinga Ukatili na Udhalilishaji

Wasanii kutoka Tuongee Faraja Club (T.F.C) wakisoma utenzi uliobeba Ujumbe wa udhalilishaji katika kongamano la kupinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji  lililoandaliwa na klabu hiyo huko Skuli ya Faraja Kilima hewa Unguja.
Wasanii kutoka Tuongee Faraja Club wakisherehesha kwa Ngonjera iliyobeba Ujumbe wa umuhimu waelimu kwa  mtoto wa kike na Udhalilishaji  katika kongamano la kupinga vitendo vua udhalilishaji na ukatili lililoandaliwa na klabu hiyo huko Skuli ya Faraja Kilima hewa Unguja.
Mkurugenzi wa Udhibiti na Uchunguzi Tume ya Dawa za Kulevya Juma A. Zidikheyr akielezea athari za Madawa ya Kulevya  katika kongamano la kupinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji  lilofanyika Skuli ya Faraja Kilima hewa Unguja.
Afisa kutoka Tume ya Ukimwi Zanzibar Halima Ali Mohamed akitoa ufafanuzi juu ya ugonjwa wa ukimwi wakati wa Kongamano la kupinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji  lilofanyika Skuli ya Faraja Kilima hewa Unguja.
Mwakilishi wa Mahkama ya Kadhi Abdul-rahman Omar Bakar akichangia mada kuhusu kujikinga na kuepuka vikundi viovu wakati wa Kongamano la kupinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji  lilofanyika Skuli ya Faraja Kilima hewa Unguja.
Waziri  Nchi  (OMKR) Dk.Saada Mkuya salum akizungumza kuhusu udhalilishaji wakati wa kongamano la kupinga vitendo vya Ukatili na Udhalilishaji liliandaliwa na  Tuongee Faraja Club huko Skuli ya Faraja Kilima hewa Unguja.
Washiriki mbalimbali wakifuatilia Kongamano la kupinga Vitendo vya Udhalilishaji na Ukatili Lililofanyika Skuli ya Faraja Kilima hewa Unguja. 
PICHA NA FAUZIA MUSSA – MAELEZO ZANZIBAR.

Na Sabiha Khamis Maelezo  17/08/2021

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dk. Saada Mkuya Salum amewataka wazazi na walezi kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha watoto wanapata malezi bora ili kuwajenga katika msingi wa maadili mema.

Akizungumza na wanafunzi pamoja na wajumbe katika Kongamano la Tuongee Faraja Club (TFC) lilioandaliwa na walimu na wanafunzi wa Skuli ya Faraja  katika ukumbi wa Skuli hiyo amesema wazazi wasiridhike na matokeo wanayopata watoto maskulini bali wafuatilie na mienendo yao.

Amesema kuwa, uanzishwaji wa Club hiyo utasaidia kushajihisha wanafunzi kuwa na maadili mema ambao ndio msingi wa maendeleo ya jamii pamoja na kusaidia kupunguza vitendo vya udhalilishaji nchini.

“Vitendo vya udhalilishaji ni vingi katika jamii yetu ni vyema tukiwa mstari wa mbele katika kuwalea watoto katika maadili mema pamoja na kupingana na ukatili huu, nawapongeza walimu na wanafunzi kwa kuanzisha Clubu hii ambayo ina lengo la kupinga vitendo vya udhalilishaji” alisema Waziri huyo.

Aidha aliwaasa wanafunzi wa Skuli ya hiyo kuwa watiifu kwa walimu wao na kuiendeleza Club hiyo yenye lengo la kuisaidia Serikali katika kupinga na Vitendo vya Ukatili na Udhalilishaji wa kijinsi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Udhibiti na Uchunguzi Tume ya Dawa za Kulevya Juma Abdul-rahman Zidikheiry ameitaka jamii ijiepushe na vitendo hivi vya matumizi ya madawa ya kulevya ili kuilinda nguvu kazi ya taifa isipotee.

Aidha amesema Serikali inaendelea kupanga sheria madhubuti ya kudhibiti dawa za kulevya ili kutokomeza uhalifu huu, kwani ni kosa kujihusisa na ushiriki wa aina yoyote ikiwa kwa kuvuta, kuuza, kununua na mengineyo.

Akizungumzia kuhusu maambukizi ya virusi vya Ukimwi Mwakilishi kutoka Tume ya Ukimwi, Halima Ali Mohamed amesema vijana wengi kuanzia umri wa miaka 15 hadi 35 wamekuwa ni waathirika wakubwa wa maradhi ya Ukimwi kutokana na kujihusisha na vitendo ya uasharati katika umri mdogo.

Alieleza kuwa kushamiri kwa vitendo vya ulawiti, matumizi ya dawa za kulevya pamoja na mporomoko wa maadili unachangia kwa kiasi kikubwa katika kusababisha maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.

Aliwashauri wazazi na walezi pamoja na walimu kuwa karibu na wanafunzi ili kuweza kutatua changamoto zinazowakabili wanapokuwa nje ya mazingira ya nyumbani au Skuli ili kuepusha uwezekano wa kupata magonjwa ikiwemo Ukimwi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.