PICHA NA FAUZIA MUSSA -MAELEZO ZANZIBAR
Na Sabiha Khamis Maelezo. 16/08/2021
Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Nassor Ahmed Mazrui ameahidi kudumisha ushirikiano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamuhuri ya watu wa China ili kuinua Uchumi wa Nchi.
Akizungumza na Balozi Mdogo wa China aliopo Zanzibar na ujumbe wake, wakati akipokea msaada wa Dawa kutoka Serikali ya Jamuhuri ya watu wa China Mh. Mazroui alisema Serikali hizi mbili ni marafiki wa muda mrefu hivyo wataendeleza ushrikiano huo ili kuwapatia wananchi huduma bora za afya.
Aidha amesema Serikali ya Zanzibar inaishukuru Serikali ya Jamuhuri ya watu wa China kwa kushirikiana nao kwa kila hali pamoja na kuwapatia misaada mbali mbali ikiwemo Dawa, Madaktari na Chanjo ya UVIKO-19.
“Tunaishukuru Serikali ya Jamuhuri ya watu wa China wamekuwa wakishirikiana na sisi kwa kila hali hususani Wizara ya Afya kwa kutupatia madaktari kila mwaka na misaada mbali mbali ambayo husaidia katika kutoa huduma kwa wananchi” alisema Waziri.
Mapema Waziri Mazrui alifafanua kuwa Wizara yake imepokea Dawa 165 zenye thamani ya takribani Shilingi Milioni 120 kwa Unguja ambazo ni idadi sawa na Dawa zilizotolewa Kisiwani Pemba.
Kwa upande wake Balozi Mdogo wa China aliopo Zanzibar Zhan Zhisheng amesema Serikali ya watu wa China inaahidi kuendelea kuisaidia Zanzibar kwani tayari wameshajaza mkataba wa kujenga nyumba za wafanyakazi katika Hospitali ya Abdalla Mzee iliopo Mkoani Pemba.
Hata hivyo Balozi Zhan amefurahishwa na mashirikiano yaliyopo baina ya madaktari wa Zanzaibar na madaktari kutoka China katika utendaji wa kazi unaopelekea kubadilishana Ujuzi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Makabidhiano hayo ya Dawa baina ya Wizara ya Afya Zanzibar na Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China yalifanyika katika Ukumbi wa mikutano Hospitali ya Mnazi Mmoja Mjini Unguja.
No comments:
Post a Comment