Habari za Punde

Maadhimisho ya Elimu Bila Malipo Kufanyika Kisiwani Pemba Septemba 23,2021.

Na.Maulid Yussuf WEMA  PEMBA.

Tamsha la Elimu bila malipo kisiwani Pemba limezinduliwa rasmi leo, kwa kufanyika matembezi ya hiari yaliyoanzia Skuli ya Sekondari Fidel Kastro  na kuishia katika viwanja vya Vitongoji Mkoa wa kusini Pemba.

Akizungumza baada ya kupokea matembezi hayo, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mhe Matar Zahor Masoud amesema, ikiwa Zanzibar inasherehekea miaka 57 ya Elimu bila malipo ni vyema viongozi kutafakari kwa nini Serikali tokea mwaka 1964 inaendelea kusherehekea sherehe hizo kwa kutafakari wanapotoka katika suala la elimu.

Amesema huko nyuma wazee hawakupata fursa ya kusoma  na elimu ilikuwa ikitolewa kwa watu maalum na hata majengo yalikuwa ni machache mno, lakini hivi sasa kuna majengo  mengi ya Skuli na ya kisasa mpaka vijijini ambapo amessma hali hiyo ni kuashiria kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha na huduma bora za elimu nchini.

Amesema hayati Karume alikuwa na dhamira ya kuhakikisha kila mtu anasoma kwa mujibu wa ukomo wa akili yake na sio uwezo wa wazazi wake na huduma zote bure ikiwemo vitabu.

Amewataka kuendelea na dhamira hiyo kwa kuwataka Wanafunzi kuendelea kusoma kwa bidii ili kuweza kuoata taifa lililo bora na lenye wasomi ambao ndio nguvu ya kuweza kuukuza uchumi wa nchi.

Amesema Taifa bora litajengwa na viongozi bora huku akiwataka kuendelea kudumisha nidhamu kwa kuwasikiliza Wazazi na Walimu wao ili waweze kufanikiwa katika maisha yao pamoja na kuwataka Walimu kuwasimamia vyema wanafunzi hao.

Hata hivyo amewahakikishia kuwepo kwa ulinzi na usalama wakati wote wa sherehe ndani ya Mkoa huo na kuwataka nao kushindana kwa amani na upendo ili kuendeleza umoja wa Zanzibar.

Nae Afisa Mdhamini Wilaya ya Elimu mwalimu Mohammed Nassor, amesema ikiwa elimu bila malipo inatimiza miaka 57 ya Elimu bila malipo, Zanzibar kupitia Wizara ya Elimu, inaendelea kuienzi kauli ya Rais wa kwanza wa Zanzibar hayati Abeid Amani Karume juu ya kutekeleza azma hiyo.

Amesema Wizara ya Elimu imeazimia na imejipanga kila mwaka kuadhimisha Tamasha hilo la elimu bila malipo ambapo kwa mwaka huu vijana zaidi ya Elfu mbili wapo kisiwani Pemba kwa ajili ya kushiriki michezo mbalimbali ya ngazi ya  Kitaifa ili kuadhimisha sherehe hizo.

Amesema visiwa vya Zanzibar kabla ya Mapinduzi matukufu ya mwaka 1964 elimu ilikuwa ikitolewa kwa matabaka ambapo wanyonge hawakupewa nafasi ya kusoma.

Kilele cha maashimisho ya Elimu bila Malipo, kinatarajiwa kufanyika tarehe 23 septemba katika Uwanja wa Gombani Mkoa wa kusini Pemba, ambapo Kauli mbiu ya mwaka hu ni "Matumizi Sahihi ya Tehama katika mazingira ya uviko 19 yatarahisisha Elimu bila Malilo".

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.