Habari za Punde

Serikali Yatenga Bilioni 45 Kutekeleza Anwani za Makazi Nchini. * Anwani za Makazi Kufanikisha Uchumi wa Kidijitali Tanzania.* Halmashauri 194 za Tanzania Bara na Zanzibar Kufikiwa.

 

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Ashatu Kijaji akitoa maelekezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi  Robert Gabriel (aliyevaa Miwani) wakati alipotembelea mtaa wa Hesawa jijini Mwanza kujionea uwekaji wa anuani za makazi katika nyumba mbalimbali pamoja na usimikaji wa nguzo zenye vibao vya majina katika mitaa 175 ya jiji hilo.

Na.Prisca Ulomi na Projestus Binamungu, Mwanza

Serikali imetenga shilingi bilioni 45 za kutekeleza mpango wa anwani za makazi na postikodi nchini kwa kujenga miundombinu ya anwani hizo kwenye halamshauri 194 nchi nzima zilizopo Tanzania Bara na Visiwani

Hayo yameelezwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wakati akiwa ziarani mkoani Mwanza kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mpango huo kwenye Halmashauri ya Jiji la Mwanza ikiwa ni eneo la mfano ili kujifunza kwa lengo la kufanikisha utekelezaji huo ili kuzifikia halmashauri zote 194 nchini ambapo halmashauri 184 ni za Tanzania Bara na halmashauri kumi ni za Tanzania Visiwani

“Lengo ni kuhakikisha kuwa kila mtaa unakuwa na jina lake na kila nyumba iwe na namba yake, hii inarahisisha utendaji kazi wa Serikali hata ndani ya jamii kwenye shughuli zetu za kiuchumi, tunaongelea kuwa na uchumi wa kidijitali, uchumi wa kidijitali hauwezekani bila kuwa tumekamilisha mfumo huu wa anwani za makazi, tunamshukuru Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutupatia shilingi bilioni 45 ndani ya Wizara yangu kwa zoezi hili tu,” amesema Dkt. Kijaji

Ameongeza kuwa dhamira ya Serikali ni kuwafikia wananchi kule walipo ili mwananchi anapopata tatizo, iwe ameunguliwa na moto pale alipo ni rahisi kuwapigia zimamoto na kuwaarifu mtaa na nyumba ulipo, au una mgonjwa unahitaji huduma ya gari ya wagonjwa, unaawarifu wanakufikia na kwa mwananchi aliyeagiza mzigo au kifurushi kutoka nje ya nchi hana sababu ya kwenda posta kufuata mzigo bali mzigo wako utaletwa mpaka ulipo ili wananchi watumie muda wao mwingi kujiletea maendeleo yao

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula amesema kuwa kazi hii ya utekelezaji wa anwani za makazi nchini nzima utatekelezwa na wananchi wenyewe waliopo kwenye maeneo hayo na itatoa ajira kwa wananchi hao na ametoa rai kwa wananchi kuwa tayari kujitokeza kutekeleza mpango huu wa anwani za makazi na postikodi

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel amesema kuwa wananchi wana kiu ya kujulikana kwa kuwa sasa mitaa yao ina majina na nyumba zao zina namba ambapo mwananchi analetewa mzigo wake pale alipo kwa kuwa sasa anatambulika mahali anapoishi

Diwani wa Nyamagana, Biko Kotecha akizungumza kwa niaba ya wananchi wake ameipongeza Serikali kwa utekelezaji wa mpango wa anwani za makazi kwa kuwa mradi huu una tija kwa wananchi, wananchi wake wamefurahi kwa kuwa mwananchi akipata ajali anaeleza moja kwa moja mahali alipo na anapata huduma

Mwenyekiti wa Kamati ya Wataalam wa Anwani za Makazi na Postikodi, Hlamashauri ya Jiji la Mwanza ndugu Moses Seleki amesema kuwa jumla ya nyumba 108,000 zimefungwa namba za nyumba, nguzo 5,800 zimewekwa zenye vibao vya majina ya mitaa na nyumba 98,000 zimeingizwa kwenye mfumo wa anwani za makazi wa simu ya mkononi

Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Zainab Chaula akitoa maelezo ya namna Wizara yake ilivyotekeleza uwekaji anuani za Makazi katika jiji la Mwanza wakati wa ziara ya Waziri wa Wizara hiyo, Dkt. Ashatu Kijaji (kulia) kwenye mtaa wa Hesawa jijini Mwanza kujionea uwekaji wa anuani za makazi. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi  Robert 

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi  Robert Gabriel akimwelezea Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Ashatu Kijaji (wa kwanza kulia) namna Jiji la Mwanza linavyotekeleza uwekaji wa anuani za makazi na usimikaji wa nguzo zenye vibao vya majina ya mitaa katika mitaa 175 ya jiji hilo, wakati alipotembelea mtaa wa Hesawa jijini Mwanza kujionea uwekaji wa anuani hizo.

Diwani wa Kata ya Nyamagana Jijini Mwanza Mhe. Biko Kotecha akizungumza kwa niaba ya wakazi wa Mtaa wa Hesawa Jijini Mwanza wakati wa ziara ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Ashatu Kijaji (wa kwanza kulia) Jijini humo kujionea utekelezaji wa anuani za makazi wakati alipotembelea mtaa huo.Wa pili kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula na wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Mkoa huo, Mhandisi  Robert Gabriel.

Mwonekano wa nyumba zilizowekewa namba za nyumba katika jiji la Mwanza ikiwa ni utekelezaji wa anuani za makazi katika jiji hilo ambapo jumla ya nyumba 108, 000 tayari zimewekwa namba kwenye mitaa 175.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.