Habari za Punde

Ufunguzi wa Masjid Muhamad Khaula Alqaaz Kisauni Wilaya ya Magharibi "B" Unguja leo.15-10-2021.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akiufungua rasmi Masjid Muhamad Khaula Alqaaz uliopo Kisauni Wilaya ya Magharibi "B" Unguja akiondoa kipazia, akiwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi.
Katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Khalid Mfaume akiwakumbusha waumini na viongozi wa Masjid Muhamad uliopo Kisauni kuepuka mizozo na migogoro isiokuwa na tija kufuatia kufunguliwa kwa mskiti huo.    
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na waumini wa Masjid Muhamd Kisauni mara baada ya kuteleza ibada ya Sala ya Ijumaa iliooambatana na hafla ya ufunguzi ambapo amewataka wasimamizi wa Mskiti huo kuendesha mafunzo ili kuwajenga vijana kuwa na Akhalki njema.
Na.Kassim Abdi.OMPR.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Al-haji Dk. Hussein Ali Mwinyi ametoa wito kwa waislamu kujitokeza Zaidi kusaidia harakati za kuunga mkono masuala ya dini ili kuijenga jamii yenye maadili mema.

Makamu wa Pili wa Rais alieleza hayo wakati akimuwakilisha Rais Dk. Mwinyi wakati akifungua rasmi masjid Muhamad Khaula Alqaaz uliopo Kisauni Wilaya ya Magharibi “ B” Unguja.

Mhe. Hemed aliwataka wasimamizi wa Masjid Muhamad katika kuendesha mskiti huo kuna haja ya kutoa mafundisho mema kwa vijana yatakayowajenga kifikra, kitabia na kiakhlaki kwa lengo kufikia lengo lililokusudiwa.

Aliwakumbusha viongozi kuutunza mskiti huo sambamba na kuendeleza Amani, Utulivu na mshikamano miongoni mwa waumini jambo litakalosaidia kustawisha Imani na maenedeleo Nchini.

Aidha, Makamu wa Pili wa Rais aliwahakikishia waumini hao kuwa Rais Dk. Mwinyi ataendelea kutoa ushirikiano kwa kuzingatia taratibu na miongozo katika kuendeleza mskiti huo.

Nae, Katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Khalid Mfaume aliwataka waumini hao kuepuka migogoro isiokuwa na tija katika uwendeshaji wa mskiti huo.

Sheikh Khalid alisema mskiti ni nyumba ya M/mungu hivyo ofisi ya Mufti haitapenda kuona katika nyumba hiyo kunajitokeza mizozo itakayosababisha mitafaruki miongoni mwa waumini.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Islamic Foundation Samahatu Sheikh Arif Naad alisema taasisi hiyo itaendelea kutoa ushirikiano wake katika kuendesha harakati za kuhuwisha huduma za jamanii ikiwemo ujenzi wa miskiti pamoja na huduma nyengine muhimu.

Sheikh Arif Naad aliomba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuipatia taasisi hiyo eneo maalum kwa ajili ya kujenga Ofisi zake zinakazopelekea kufanya kazi zake kwa ushirikiano wa karibu na Ofisi ya Mufti Zanzibar.

Mapema Mhe. Hemed alijumuika pamoja na waumini wa Masjid Muhamad Khaula Alqaaz katika ibada ya sala ya Ijumaa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.