Habari za Punde

Shirika la Maendeleo la World Vission Latoa Msaada wa Vifaa Tiba, Thamani yake Sh Milioni 31, Katika Hospitali ya Wilaya ya Handeni.

Mkuu wa Wilaya ya Handeni Bi.Siriel Mchembe akiwafariji wagonjwa aliowakuta katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni wakisubiri kupatiwa huduma ya matibabu hospitalini hapo.

Na Hamida Kamchalla, HANDENI.

MKUU wa Wilaya ya Handeni Siriel Mchembe amekabidhi vifaa tiba vyenye thamani ya sh milioni 31 kwa Halmashauri ya Wilaya hiyo vilivyotolewa na Shirika la maendeleo la World Vision Tanzania. 

Vifaa hivyo ambavyo vimekabidhiwa kwa Mganga mkuu wa hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ni pamoja na vitanda vya kujifungulia, Kiti cha mgonjwa wa meno na mashine za kupima presha.

Wakati akikabidhi vifaa hivyo Mchembe ameishukuru serikali kupitia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha wanawake wa Handeni wanajifungua kwenye mazingira salama.

"Na kupitia juhudi zake ameanzisha kaulimbiu ya tuwavushe ili kuondoa changamoto zinazowakabili wanawake wakati wa kujifungua na kupitia fedha za tozo zitokanazo na miamala ya simu Halmashauri ya Wilaya ya Handeni imepokea kiasi cha sh milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya Sindeni na kwasasa kituo chetu kipo hatua ya upauaji" alisema.

"Katika kuunga mkono juhudi za serikali kwa kuweka mazigira mazuri na salama kwenye sekta ya afya, Shirika la World Vision Tanzania limetoa vifaa hivi kwa ajili ya zahanati za Kwamsisi, Kwandugwa, Pozo, Mkalamo na Kwasunga, alibainisha Mchembe.

Aidha mkuu huyo amwongeza kuwa "serikali inatambua mchango wa Shirika la World Vision Tanzania kwani ni wadau wakubwa wa sekta ya afya Handeni".

Naye Mganga Mkuu wa Halmashauri  ya Wilaya ya Handeni Dkt. Kanansia  Shoo ametoa shukurani zake kwa Shirika hilo kwa mchango wao kwenye sekta ya afya kwa halmashauri ya Handeni na kueleza kuwa zahanati ya Kwamsisi itaanza kutoa huduma za wagonjwa wa meno huku akiahidi kuvitunza vifaa hivyo ili viweze kukidhi mahitaji ya wananchi.

Kwaniaba ya Mkurugenzi Dkt Kanansia alitoa cheti maalum cha shukrani kwa Shirika la World Vission kwa kutambua mchango wao kwenye sekta ya afya wanavyotekeleza kwenye Halmashauri ya Handeni.

Kwa upande wake Meneja wa World Vision kanda ya Mashariki Daniel Chuma ameeleza "shirika letu linaunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha maisha ya wananchi kwa kutoa elimu za kuelimisha jamii kuhusu afya kwa kutumia vikundi mbalimbali vya sauti za umma, kuwapa semina wataam wa afya na kutoa vifaa kwaajili ya zahanati zote za tarafa Kwamsisi".
Mkuu wa Wilaya ya Handeni Bi.Siriel Mchembe na Watumishi wa sekta ya Afya katika hospitali ya halmashauri ya Wilaya ya Handeni, akizungumza na Wafanyakazi wa Hospitali hiyo na Wananchi kabla ya kukabidhi Vifaa mbalimbalim kwa ajili ya kutolea huduma za Afya katika Hospitali hiyo,vilivyotolewa na Shirika la maendeleo la World Vision Tanzania. 
Baadhi ya Watumishi wa hospitalini ya Halmashauri ya Wilaya Handeni wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Handeni Bi.Seriel Mchembe (hayupo pichani) wakati wa hafla ya kukabidhi Vifaa vya Huduma ya Afya kwa Hospitali hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni Siriel Mchembe mwenye shati jeupe pamoja na Mganga mkuu wa hospitali ya halmashauri ya Wilaya ya Handeni Dkt. Kanansia Shoo wakiwa wamekalia vitanda vya wakina mama kwa ajili ya kujifungulia baada ya makabidhiano.

Sehemu ya vifaatiba vilivyokabidhiwa katika hospitali hiyo ambavyo ni pamoja na mashine za kupimia mapigo ya moyo na kiti kimoja cha mgonjwa wa meno.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.