Habari za Punde

Watumishi wa Umma kuanza kuneemeka

 Mwashungi Tahir,       Maelezo        

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imejikita katika kutatua kilio cha muda mrefu cha watumishi wa umma cha kutokuwepo utaratibu wa kuwapandisha madaraja na kutokuwepo kwa utofauti wa kimaslahi baina ya mtumishi aliyeajiriwa zamani na watumishi walioingia  kazini karibuni.


Akizungumza na waandishi wa habari huko katika ukumbi wa Katiba na Sheria uliopo Mazizini Waziri Ofisi ya Rais , Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala bora Haroun Ali Suleiman wakati alipokuwa akitaja mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka mmoja cha Uongozi wa Serikali ya Awamu ya nane na kutaja mipango inayotarajiwa kufanyika  katika Wizara hiyo.


Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya awamu ya nane imeweka  mikakati ya Wizara katika kuimarisha uwajibikaji na ufanisi katika utumishi wa umma, kudhibiti rushwa  na uhujumu wa uchumi, kuimarisha upatikanaji wa haki za wananchi na msaada wa kisheria na kuimarisha utawala bora.


Hivyo akiyataja mafanikio ni pamoja uhakiki wa watumishi hewa unaoendelea kwa lengo la kudhibiti upotevu wa fedha za umma kutokana na mishahara wanaolipwa ambao hawapo, zoezi hilo tayari liko katika hatua ya mwisho kukamilika na taarifa itatolewa rasmi kwa umma .


Waziri Haroun amesema katika kipindi cha mwaka mmoja Novemba 2021 Serikali imeanzisha Skuli ya Sheria kwa kuanza kuteuliwa kwa Mkuu wa Skuli , Mwenyekiti wa Baraza la Skuli ya Sheria  pamoja na watendaji  ambapo michoro ya jengo jipya  la Skuli  hiyo tayari imefikia hatua nzuri katika utayarishaji wake.


Pia amesema Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu na huduma katika Chuo cha Utawala wa Umma (IPA)kiliopo Tunguu pamoja na kuendeleza Tawi la Chuo lilioko Pemba , juhudi mbali mbali zinaendelea kuchukuliwa na Serikali katika kukiimarisha Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar kwa kukipatia vifaa na Wakufunzi ili kuhakikisha kuwa Chuo kinaendelea na  mafunzo ya Shahada ya kwanza na mafunzo mafupi yatakayoendeleza watumishi wa umma na viongozi kwa ufanisi mkubwa.


Vile vile amesema ili kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya Ofisi kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022 malengo na mikakati inaendelea kutekelezwa ni pamoja kuimarisha misingi ya utawala bora na maadili katika utendaji wa shughuli za Serikali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.