Habari za Punde

Waziri wa Afya Zanzibar Mhe Nassor Ahmed Mazrui Akizungumzia Miradi Mbalimbali Itayotekelezwa Kwa fedha za IMF Kupitia Wizara ya Afya .

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Wazee Jinsia na Watoto Zanzibar Mhe.Nassor Ahmed Mazrui akisisitiza jambo wakati wa mkutano wake na  Waandishi wa Habari wa Vyombo mbalimbali vilioko Zanzibar, kuzungumzia uboreshaji na kuimarisha maendeleo ya utoaji wa huduma ka Jamii.

Na Khadija Khamis – Maelezo ,12/11/2021.

Wizara ya Afya ,Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto imepatiwa kiasi cha shiling bilioni 69  kutoka katika mfuko wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia mkopo wa fedha  wa Shirika la fedha duniani (IMF) ili kuimarisha maendeleo ya utoaji wa huduma kwa jamii .


Hayo ameyasema Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii. Wazee .Jinsia na Watoto Nassor Ahmed Mazrui  katika Hotel  ya Verde wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu miradi mbali mbali itayotekelezwa kwa fedha za  IMF kupitia Wizara ya Afya .


Amesema miradi hiyo ni kuimarisha miundombinu ya afya pamoja na upatikanaji wa vifaa tiba  ambavyo vitasaidia maendeleo  ya afya za wananchi.


Akielezea miradi hiyo ni pamoja na kuimarisha  miundombinu ya afya ikiwemo ujenzi wa hospitali mpya ngazi ya Mkoa wa Mjini Magharibi katika eneo la Lumumba itakayokuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 200 kwa wakati mmoja hospitali hiyo ya mkoa itakuwa na ghorofa tano huduma za wagonjwa wa nje (OPD) na watakaolazwa (IPD).


Aidha alisema hospitali hiyo itakuwa na huduma za kisasa za MRI,CT Scan na kutoa huduma zote za kitaalamu huduma za sikio,pua na koo,- macho,meno,kliniki na wodi za kulaza wagonjwa mbalimbali ili kuongeza wigo ili kupunguzia mzigo Hospitali ya Mnazimmoja.


Alisema kuhusu Hospitali ya Abdalla Mzee Wizara ya Afya inatarajia kujenga chumba cha wagonjwa mahtuti (ICU),chumba cha kuhifadhia maiti pamoja na kuweka vifaa vya kisasa vya uchunguzi  digital X  ray’,huduma za figo,vifaa vya chumba cha upasuaji na kuweka mtambo wa gesi tiba ambayo itasambaza moja kwa moja kwenye kitanda cha mgonjwa.   

                               

Waziri Mazrui alisema Wizara ya Afya  inawajibu wa kusimamia upatikanaji wa haki kwa makundi yenye mazingira magumu kwa kuimarisha mifumo ya hifadhi ya jamii na huduma kwa wazee ,watoto na wanaoishi katika  mazingira magumu zaidi .


“ Jukumu letu ni kuhakikisha tunawapatia wananchi wote wa Zanzibar huduma bora za kinga na tiba bila ya ubaguzi wa aina yoyote .alisema Waziri Mazrui”.


Alifahamisha kuwa kuratibu na kusimamia utekelezaji wa haki za wanawake na watoto katika kukabiliana na vitendo vyote vya udhalilishaji ikiwa ni pamoja na kusimamia utekelezaji wa sera, sheria zinazohusu maendeleo ya wanawake na watoto pamoja na kuwaendeleza wanawake hao kwa kuzingatia Mipango ya Kitaifa Mikataba ya Kimataifa na Kikanda .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.