Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Hussein Ali Mwinyi hatimae ile ahadi yake aliyowaahidi wananchi walioathirika
na Kampuni ya Masterlife Microfinance Ltd iliyokuwa ikifanya kazi zake kinyume
na sheria ameanza kuitekeleza ambapo hivi leo wameanza kulipwa wananchi wa Mkoa
wa Kaskazini Unguja.
Zoezi hilo limeanza kutekelezwa leo huko katika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja ambapo mamia ya wananchi waalioathirika na Kampuni ya Masterlife walihudhuria kike kwa kiume ili kupata haki yao hiyo na kutoa pongezi kubwa kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa uwamuzi wake huo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao walimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa uwamuzi wake huo na kukiri kwamba kiongozi huyo anawajali, anawapenda na kuwathamini wananchi wake na kumuhakikishia kwamba wataendelea kumuunga mkono na kuzidi kumuombea dua ili azidi kupata afya na nguvu za kuwahudumia.
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Ayoub Mohammed Mahmoud alisema kuwa hatua hiyo ni ile ahadi aliyoitoa Rais Dk. Mwinyi dhinam hiyo aliibeba kwa dhamira ya kuleta utulivu katika nchi na kuwafanya wananchi wake kuendeleza katika shughuli mbali mbali za uchumi kupitia fedha zwalizoweka katika kampuni hiyo.
Alisema kuwa maamuzi ya Rais yalikuwa sahihi kwa sababu kulikuwa na wananchi wengi wanyonge walioguswa na kadhia hiyo, na kueleza kuwa utekelezaji wake wa kulipwa wananchi hao unakwenda kuwasaidia hasa wananchi wanyonge wa Mkoa huo kama alivyosema kwamba kila mwananchi atapata haki yake.
Aliongeza kwamba Mkoa wake utachukua juhudi za makusudi katika kuhakikisha inawasimamia wananchi wake hao vyema ili waweze kupata haki zao hizo za msingi.
Nae Kamishna wa Bajeti Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Saumu Khatib Haji alisema kuwa zoezi hilo kwa Mkoa wa Kaskazini Unguja litakuwa kwa siku tatu kuanzia leo Disemba 08 hadi Disemba 10 ambapo jumla ya wananchi walioathirika ni 1456 ambao ni kwa wale walioweka fedha kuanzia 100,000 hadi 1,000,000 na kusema kwamba zoezi linakwenda vizuri.
Sambamba na hayo, wananchi hao pia, walieleza masikitiko yao kwa kujitokeza baadhi ya matapeli ambao wamekuwa wakitumia maelekezo kupitia kwa baadhi ya benki hapa nchini kwa kuwapigia simu kwa lengo la kupelekea fedha zao huko jambo ambalo limepingwa na kupigwa vita sambamba na kutolewa maelezo na Mkuu wa Mkoa wa Kaskani Unguja Ayoub Mohammed Mahmoud pamoja na Kamishna wa Bajeti Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Saumu Khatib Haji.
Kwa nyakati tofauti Rais Dk. Mwinyi katika hotuba zake alikuwa akionesha jinsi tukio hilo la kuchukuliwa fedha zao wananchi walioathirika na Kampuni hiyo na kuwaahidi kwamba Serikali anayoiongoza itachukua juhudi za makusudi za kuhakaiksiha inawasaidia wananchi hao kwa kuwapa haki yao hiyo.
Hivi karibuni katika hotuba yake ya mwaka mmoja aliyoiotoa kwa wananchi huko katika hoteli ya Golden Tulip, iliyopo katika eneo la uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Rais Dk. Mwinyi aliwaahidi wananchi walioathirika na Kampuni ya Masterlife kwamba watasaidiwa kupatiwa fedha zao. “Nimeamua kubeba dhima hii ili kuwaondolea usumbufu wa maisha wananchi wanaoupata”,alisema Rais Dk. Mwinyi katika hotuba yake hiyo.
Aidha, mnamo tarehe 25 Mei 2021 alipokutana na kufanya mazungumzo na wawakilishi wa waathirika hao huko katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa kwa upande wake ana nia njema kwani ameapa kuwatendea haki wananchi wa Zanzibar na hayuko tayari kuona mwananchi hata mmoja anadhulumiwa.
Zoezi hilo litafanyika kwa muda wa siku tatu katika Mkoa huo wa Kaskazini na baadae kuendelea katika Mikoa mengine ya Unguja na Pemba ambapo litakwenda kwa awamu.
Kitengo cha Habari
Ikulu Zanzibar.
No comments:
Post a Comment